Benton Nollo, Bahi
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani S. Jafo (Mb) ameupongeza Uongozi wa Wilaya ya Bahi kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za Afya unaoendelea katika Halmashauri hiyo.
Akizungumza katika ziara yake ya kikazi wilayani hapa Jafo ameonyesha kuridhishwa kwake na wakati anapokea taarifa ya Wilaya ya Bahi kuhusu maendeleo ya ujenzi wa miradi ya Afya na kisha kutembelea ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambayo ipo katika hatua ya lenta.
“Hakika Bahi mmefanya kazi nzuri mmejenga kwa kasi ya ajabu huku ubora ukizangatiwa katika majengo yote na bado mmesimamia matumizi mazuri ya fedha za mradi kwa kuwapa vibarua kazi hii ya ujenzi". Alisema Jafo na kuongeza.
"Niseme wazi kuwa Bahi mmenifurahisha kwa sababu mmeweza kutafsiri vizuri mfumo wa ujenzi pasipo kutumia Mkandarasi yaani “Force Account” ambao unatumia fedha kidogo na mmeweza kutumia nguvu kazi mliyonayo ya vijana wa mgambo kufyatua matofali na vibarua ambao ni vijana kutoka hapa hapa Bahi kujenga majengo ya Afya hongereni sana kwa hili” Alisema Jafo.
Pamoja na kuwapongeza viongozi hao pia aliwataka kumaliza tofauti zilizopo kati ya Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo na Mbunge kwa kuwasisitiza kila mmojawao kutekeleza majukumu yake pasipo kuingiliana wala kukwamishana.
“Lengo letu sote ni kuleta maendeleo kwa Wananchi kwa hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri tekeleza majukumu yako pasipo kumuingilia Mbunge na Mbunge naye aendelee kutekeleza majukumu yake ya Kibunge tena anafanya vizuri sana na miradi yote hii mnayopata ni jitihada zake Bungeni kwa hiyo msimkwamishe mpeni ushirikiano wa kutosha” Alisema Jafo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Belinith Mahenge amemueleza Waziri Jafo kuwa Wilaya ya Bahi ni moja kati ya Wilaya za Dodoma zinazofanya vizuri katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mhe. Mwanahamisi Munkunda amesema kuwa ujenzi wa vituo vitatu vya Afya umeshakamilika na vitafunguliwa hivi karibuni wakati Hospitali ya Wilaya ikiwa katika hatua ya lenta.
“Pamoja na changamoto chache ambazo tunakutana nazo katika utekelezaji wa miradi hii kama vile ushiriki mdogo wa wananchi katika kuchangia nguvu kazi, kukosekana kwa Mhandishi wa Halmashauri lakini tumeweza kukabiliana nazo na kuhakikisha hazikwamishi ujenzi wa miradi yetu ya Afya” Alisema Munkunda.
Ujenzi wa Hospitali za Wilaya unaondelea kote nchini na unatarajiwa kukamilika Juni 30, 2019.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani S. Jafo (Mb), akiwasili katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bahi tarehe 08 Mei, 2019.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani S. Jafo (Mb), akiongea na viongozi pamoja na wataalam mbalimbali waliojitokeza wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bahi tarehe 08 Mei, 2019.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani S. Jafo (Mb), akiiendelea na ukaguzi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bahi tarehe 08 Mei, 2019.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani S. Jafo (Mb), akiangalia matofali maalum kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mionzi ambayo yamefyatuliwa na vijana wa Jeshi la Akiba ambao wamepewa kazi hiyo kwa lengo la kurahisisha kazi ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bahi wakati wa ziara yake tarehe 08 Mei, 2019.
Muonekano wa Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD) ambalo ni miongoni mwa majengo saba yanayoendelea kujengwa katika Hospitali ya Wialaya ya Bahi.
Muonekano wa Jengo la Utawala ambalo ni miongoni mwa majengo saba yanayoendelea kujengwa katika Hospitali ya Wialaya ya Bahi.
(Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa