Na Benton Nollo na Bernard Magawa DMC, Makanda
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amekabidhi Kompyuta tano pamoja na mashine moja ya kuchapisha (printa) zenye thamani ya shilingi milioni 10.8 katika Shule ya Sekondari CHONAMA iliyopo Kata ya Makanda wilayani Bahi mkoani Dodoma.
Munkunda amekabidhi vifaa hivyo wakati akiwa kwenye ziara yake ya siku moja katika kata hiyo na kufika shuleni hapo kukagua shughuli za maendeleo ya kitaaluma tarehe 01 Desemba 2020.
Amesema ameamua kutoa vifaa hivyo kwa Shule ya Sekondari CHONAMA kama motisha kutokana na shule hiyo kufanya vizuri kitaaluma katika Wilaya ya Bahi na kwamba kwa kufanya hivyo itawarahisishia Walimu katika shughuli zao za ufundishaji na kuongeza ufaulu zaidi kwa wanafunzi.
“Nimewaletea kompyuta tano na printa moja kama motisha kwa shule yenu kwa kuwa mmekuwa mkifanya vizuri katika mitihani ya Kidato cha Nne Kiwilaya.” Amesema Munkunda na kuongeza kuwa:
“Naamini vifaa hivi vitawasaidia katika kuchapisha mitihani mbalimbali ikiwemo ile ya kuwapima watoto walau kila wiki”.
Pamoja na kuwapongeza walimu wa shule hiyo kwa juhudi zao, Munkunda amesema bado haridhishwi na kiwango cha ufaulu wanachokipata ukilinganisha na idadi ndogo ya wanafunzi waliopo shuleni hapo hivyo aliwaagiza waalimu hao kuongeza bidii ili waweze kufaulu zaidi kuliko sasa.
“Kulingana na idadi ndogo ya wanafunzi mlionao bado mnayo nafasi ya kufaulisha zaidi hivyo, ongezeni juhudi ikibidi hata kutumia ‘table teaching’ ili muwe na ufanisi zaidi katika matokeo yenu.” Amesema Munkunda.
Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo Mkuu wa Shule Msaidizi wa Shule ya Sekondari CHONAMA, Titus Yosea amemshukuru kiongozi huyoa kwa kuthamini mchango wao kitaaluma na kuahidi kuwa vifaa hivyo vitatumika ipasavyo ili kuinua zaidi kiwango cha taaluma shuleni hapo na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya kwa niaba ya Walimu wenzangu na Manafunzi wa Shule ya Sekondari CHONAMA nakushukuru sana kwa kutuletea vifaa hivi, nasi tutavitumia kwa maandalizi mbalimbali ya masomo na mitihani ya mara kwa mara hivyo tunaamini kwa kufanya hivyo kiwango cha ufaulu katika shule yetu kitaongezeka.” Amesema Mwalimu Yosea.
Shule ya Sekondari CHONAMA ni mwiongoni mwa shule za sekondari 21 wilayani Bahi na imekuwa ndiyo shule pekee inayofanya vizuri katika matokeo ya Kidato cha Nne katika wilaya na Mkoa wa Dodoma.
Matukio katika Picha:
Pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda wakati akikabidhi vifaa hivyo.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa