Wilaya ina vituo 43 vya kutolea huduma za afya, vikiwemo Vituo vya Afya 6 na Zahanati 37, kati ya zahanati hizi 2 zinamilikiwa na mashirika ya dini. Wilaya inaendelea na ujenzi wa zahanati 2 katika vijiji vya Chonde na Mayamaya. Pia, Wilaya inapanua Kituo cha Afya Bahi ili kuweza kutoa huduma za upasuaji wa dharura. Huduma za afya zinatolewa kwa kuzingatia maeneo muhimu ya afya ya Uzazi na Mtoto, Afya ya Kinga (Udhibiti na Kinga ya Magonjwa kwa Jamii), Udhibiti wa magonjwa ya eneo husika (maalum) kama vikope na kichocho. Uimarishaji wa huduma za kiutawala, miundombinu, vifaa na dawa (tiba). Wilaya imefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi kutoka 9 mwaka 2000 hadi kufikia vifo 4 mwaka 2016. Pia, katika kipindi hiki, Wilaya imefanikiwa kupunguza vifo vya watoto chini ya miaka mitano kutoka vifo 40 hadi kufikia vifo 12 mwaka 2016.
Aidha, sekta ya afya bado ina upungufu mkubwa wa watumishi kulingana na ikama. Hadi sasa kuna jumla ya watumishi 369 kati ya 779 wanaohitajika na hivyo kuwa na upungufu wa watumishi 410.
Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) Wilaya inaupa kipaumbele ili kuboresha afya za wakazi wake na ilijiwekea lengo la kusajili kaya 15,269 (31%) kati ya kaya 49,554 za Wilaya kwa miaka mitatu (2015 hadi 2017) chini ya mradi wa Tuimarishe Afya (HPSS). Katika kipindi hicho Wilaya imefanikiwa kusajili kaya 8,190 (54%) ya lengo, ambapo shilingi 184,270,000.00 zimekusanywa. Umuhimu wa kujiunga na mfuko huu bado utaendelea kuwa ajenda ya kudumu katika vikao vya Kiserikali, vituo vya Afya na Zahanati.
Elimu ya mapambano dhidi ya UKIMWI inatolewa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikisisitiza njia mbalimbali za ueneaji, jinsi ya kujikinga pamoja na umuhimu wa mabadiliko ya tabia kwa jamii hasa vijana ambao ndio waathirika wakubwa katika jamii yetu. Kampeni dhidi ya UKIMWI inaendeshwa kwa kutoa elimu na upimaji wa VVU wakati wa matukio ya sikukuu za kitaifa na kimataifa ikijumuisha sikukuu ya wakulima, siku ya UKIMWI duniani.
Makundi maalum yanashirikishwa katika kampeni, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa baa, wakunga wa jadi, viongozi wa dini, kisiasa na wasanii (vikundi vya ngoma). Wazazi hupatiwa elimu siku za kliniki ya mama na mtoto. Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ni wadau muhimu katika kutoa elimu na huduma dhidi ya UKIMWI. Viongozi wa dini wanatoa elimu kwa waumini, pamoja na viongozi wa kisiasa na jamii yote kupitia mikutano ya hadhara.
Wananchi waliopima kwa hiari kati ya Januari hadi Desemba, 2015 ni 15,435 (Me 5,893 na Ke 9,542). Waliogundulika kuwa na maambukizi ya VVU ni 377 (Me 143, Ke 234) sawa na 2.4%. Wilaya ina vituo 5 vinavyotoa huduma ya dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV’s), ambapo wagonjwa 1,420 wanahudumiwa kati ya wagonjwa 2,000 walioandikishwa. Vituo hivyo ni Babayu, Bahi, Chipanga, Mtitaa na Mundemu. Mpango wa kuongeza vituo vingine unaendelea, huduma mseto za Kifua Kikuu na UKIMWI zimeanzishwa na kuimarishwa ambapo kati ya wagonjwa 91 wa Kifua Kikuu 11 wamegundulika kuwa na maambukizi ya VVU katika kipindi hicho.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa