Na Benton Nollo na Bernard Magawa DMC, Chidete
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Chidete wameaswa kutojifeshilisha katika mitihani yao ya mwisho na badala yake wametakiwa kusoma kwa bidii ili kutimiza ndoto zao za baadaye.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Darasa la Sita shuleni hapo kutokana na kuibuka kwa baadhi ya wazazi kuwatishia watoto wenye uwezo mzuri darasani kufanya vibaya makusudi kwa kigezo cha kwamba hawana uwezo wa kuwasomesha pindi watakapofaulu.
Munkunda ameyasema hayo alipotembelea shule hiyo kukagua ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na nyumba moja ya mwalimu tarehe 01 Desemba 2020 ambapo aliridhishwa na ujenzi huo na kuagiza fundi wa madirisha ya vioo kukamilisha haraka.
“Wanangu kumekuwa na baadhi ya wazazi wenu wanawadanganya kwamba wakati mitihani ya taifa hasa wa Dara la Saba msifaulu kwa kuwa hawana uwezo wa kuwasomesha, msikubali hata kidogo Serikali yenu kwa sasa inatoa elimu bure kuanzia chekechea mpaka Kidato cha Nne hivyo hakuna kisingizio cha nyinyi kufanya vibaya.” Amesema Munkunda na kuongeza;
“Ndiyo maana hapa Chidete Serikali ya Awamu ya Tano imeleta shilingi milioni 85 kujenga miundombinu hii ambapo shilingi milioni 25 zimetolewa na Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo – EP4R na shilingi milioni 60 zimetolewa na Taasisi ya Elimu Tanzania – TEA.”
Munkunda amewasisitiza wanafunzi hao kuzingatia masomo na kuacha utoro ili waweze kunufaika na elimu inayotolewa na serikali bila malipo.
“Watoto wazuri Serikali yetu inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli inawapenda watoto wote nchini ndiyo maana inaendelea kujenga miundombinu bora hadi vijijini ili muweze kufurahia mazingira mazuri ya kujifunzia hivyo, someni kwa bidii ili mfaulu na kufikia malengo yenu.” Amesema Munkunda.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake Mwanafunzi wa Darasa la Sita shuleni hapo, Paulina Motonyi ameishukuru Serikali kwa kuwajali na kuwajengea madarasa mazuri yaliyowekwa vioo na vigae hali inayowafanya wafurahi na kuona serikali yao inawajali na haina ubaguzi.
“Tunamshukuru sana Rais Magufuli kwa kujenga madarasa mazuri hadi shuleni kwetu…mwanzo madarasa kama haya tulikuwa tunayaona kwenye video kwa wenzetu mjini lakini leo na sisi tunayatumia.” Amesema Motonyi huku akifurahi.
Aidha, Munkunda pamoja na kufurahishwa na maendeleo ya ujenzi huo aliiagiza kamati ya shule kwa kushirikiana na walimu waliopo kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa asilimia 100 ili majengo hayo yaweze kutumika kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (wa kwanza kulia) akizungumza na wanafunzi wa Darasa la Sita wa Shule ya Msingi Chidete wakati wa ziara yake alipotembelea shuleni hapo kukagua ujenzi wa madarasa manne na nyumba moja ya mwalimu tarehe 01 Desemba 2020.
Mkaguzi wa Polisi, Edward Kazungu akiwatia moyo kusoma kwa bidii baadhi ya wanafunzi wa Darasa la Sita wa Shule ya Msingi Chidete ambao nao walisema wanatamani kuwa Askari wa Jeshi la Polisi kama alivyo yeye.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (wa pili kulia) akiwaagiza kamati ya shule kushirikiana na walimu waliopo kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa asilimia 100 ili majengo hayo yaweze kutumika kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa