Rais Dkt. John Pombe Magufuli amewaambia Watanzania kuwa Uchaguzi Mkuu umekwisha na sasa kinachotakiwa ni kuchapa kazi ili kuleta maendeleo ya Tanzania na kwamba ahadi zote ambazo amezitoa kwa wananchi wakati wa kampeni zitatekelezwa.
Akizungumza leo tarehe 05 Novemba 2020, baada ya kuapishwa Dkt. Magufuli ameanza kwa kueleza siku kama ya leo ya Novemba 5 mwaka 2015 aliapishwa kuwa Rais na leo ameapishwa tena.
Amesema mwanzoni aliapishwa katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam lakini sasa ameapishwa Uwanja wa Jamhuri Mjijini Dodoma ambako ndiko yalipo Makao Makuu ya Serikali, hivyo amemshukuru Mungu.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Magufuli ameweka wazi Uchaguzi Mkuu sasa umekwisha.
"Uchaguzi sasa umekwisha, uchaguzi umekwisha, nasema uchaguzi umekwisha, sasa jukumu lililopo mbele yetu ni kuendeleza jitihada za kuleta maendeleo ya nchi yetu."
"Kiapo ambacho nimeapa mimi na Makamu wa Rais tutaendelea kukilinda kwa nguvu zote.Tutaendelea kulinda amani, umoja na mshikamano, tutaendelea kuulinda Muungano na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar." Amesema Dkt. Magufuli.
"Nawashukuru watanzania kwa kuniamini na kunichagua tena kwa miaka mitano kuongoza nchi, Ushindi ambao nimeupata mimi na Chama changu ni Watanzania wote. Pia, nawapongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi - NEC kwa kusimamia na kuendesha Uchaguzi Mkuu vizuri." Amesema Dkt. Magufuli na kuongeza;
"Pia nawashukuru viongozi wa dini kwa maombi, dua na sala katika kipindi chote cha mchakato wa Uchaguzi Mkuu. Navipongeza vyombo vya ulinzi na usalama na watanzania wote kwa kufanikisha uchaguzi kwa amani."
Dkt. Magufuli amefafanua kuvuka salama Uchaguzi Mkuu mwaka huu ni uthibitisho wa namna ambavyo Mungu analipenda Taifa la Tanzania na Watanzania. Uchaguzi Mkuu ulikuwa mtihani mwingine kwa nchi yetu, tunashukuru tumevuka salama, nchi nyingine zimeingia kwenye machafuko kwa sababu tu ya uchaguzi.
Kuhusu ahadi ambazo wamezitoa wakati wa kampeni, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 yenye kurasa 303 zote anazikumbuka na zote watazitekeleza. Pia, amesema wataendelea kutatua kero na changamoto ambazo zinawakabili Watanzania na kuhakikisha nchi inaendelea kupiga hatua kimaendeleo na amesisitiza kuendelea kusimamia rasilimali za nchi na kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi.
Dkt. Magufuli ameeleza kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka huu mwanzo wa maandalizi ya uchaguzi mkuu mwingine. Kuhusu watu waliojitokeza uwanjani hapo kushuhudia tukio la kuapishwa kwake, amesema anawashukuru wote waliofika na wanaofuatilia tukio hilo na kwamba atahakikisha unajengwa uwanja mkubwa Dodoma ambao utachukua watu wengi, kwani leo watu wengi wamekuwa nje kutokana na udogo wa uwanja.
Wakati huo huo, baadhi ya marais waliohudhuria tukio hilo wamempongeza Dkt. Magufuli kuchaguliwa tena kuwa Rais kwa awamu ya pili ambapo Rais wa Uganda Yoweri Museven amesema;
“Kwa niaba ya wananchi wa Uganda tunatoa hongera kwa Rais Magufuli kushinda uchaguzi, pili tunatoa pongezi kwa CCM kwa kupata ushindi, tena kwa amani.”
“Pia, nawapongeza watanzania kwani miezi mitatu nyuma wameingia uchumi wa kati. Hata hivyo, wakati wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu nilikuwa nafuatilia muelekeo wa CCM maana hao wengine (wapinzani) sijui muelekeo wao.”
"Chama Cha Mapinduzi kimebeba maana halisi ya ukombozi wa Afrika hasa baada ya Uhuru kwani ni viongozi wachache sana hasa Mwalimu Nyerere aliyebaki na uzalendo wa kweli na Kaunda na wengine wachache sana”. Amesema Rais Museven.
Amesema uwepo wa viongozi mbalimbali wa Afrika katika sherehe hizo, ni uthibitisho wa kweli unaotoa picha halisi ya Mwalimu Nyerere na wale viongozi wachache.
" Waasisi wetu walisimamia mambo manne ambayo ni ukombozi wa Bara la Afrika, Ustawi wa Maendeeleo ya Wananchi, Usalama wa Chakula na Undugu." Amesema Museven.
Kwa upande wake, Rais wa Zimbabwe Emmason Mnangwaga amesema Wazimbabwe wanatoa pongezi nyingi sana kwa Rais Magufuli, na wanaitazama Tanzania kama baba na mama wa Uhuru wao na Mwalimu Nyerere wanamuangalia kama mzalendo wa kweli. Rais Mnangagwa anasema;
"Wakati wa kutafuta Uhuru nchi za Afrika zilikuwa hapa Tanzania."
Pia, amesema Zimbabwe wanamshukuru Dkt. Magufuli kwani alipokuwa Mwenyekiti wa SADC aliitaka Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kuondoa vikwazo vya kiuchumi.
"Tunakushukuru Rais Magufuli kwa tamko lile, lakini tunakumbuka ziara yako ulivyokuja Zimbabwe kwani pamoja na mambo mengine mlitusaidia msaada wa mahindi." Amesema Rais Mnangagwa aliyeonekana akizungumza kwa hisia kali.
Wakati Rais wa Comoro, Azan Othman ametumia nafasi hiyo kuwapongeza Watanzania kwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu, pia amempongeza Rais Magufuli kwa kuchaguliwa tena kuiongoza Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akikagua Gwaride la Heshima lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ kabla ya kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano katika Muhula wa pili katika sherehe zilizofanyika leo tarehe 05 Novemba 2020 kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa amesimama Jukwaa Kuu la Viongozi wakati ukiimbwa Wimbo wa Taifa katika hafla ya kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma tarehe 5 Novemba 2020.
Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi akipunga mkono wakati Rais Mteule wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akiwasili katika Uwanja wa Jamuhuri Dodoma kwa ajili ya kuapishwa, baada ya kushinda Uchaguzi Mkuu wa Tanzania uliofanyika mwezi Oktoba 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli (kulia) akifurahi jambo wakati akizungumza na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi (kushoto) muda mfupi mara baada ya sherehe za Uapisho wake zilizofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma tarehe 05 Novemba 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli (kulia) akipongezwa kwa furaha na Rais wa Zimbabwe, Emerson Mnangagwa (kushoto) mara baada ya sherehe za Uapisho wake zilizofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma tarehe 05 Novemba 2020.
Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni akizungumza katika sherehe za Uapisho wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 05 Novemba 2020 katika sherehe zilizofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Rais wa Zimbabwe Emerson Mnangagwa akitoa salamu za Wananchi wa Zimbabwe katika sherehe za Uapisho wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 05 Novemba 2020 katika sherehe zilizofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa