Na Benton Nollo na Bernard Magawa (DMC), Bahi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), Selemeni Jafo (Mb) amefurahishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Bahi.
Waziri Jafo ameeleza furaha yake alipotembelea wilayani humo kukagua miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa kwa shule za msingi na sekondari zinazojengwa na Serikali kupitia programu ya Lipa Kulingana na Matokeo – EP4R tarehe 31 Desemba 2020 ambayo mingi ipo katika hatua za umaliziaji.
Katika ziara hiyo Waziri Jafo aliyeambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge ambapo ametembelea ujenzi wa madarasa Shule ya Bahi Sokoni, Msingi Bahi Misheni, na Hospitali ya Wilaya ya Bahi ambayo kwa sasa imeanza kufanya kazi.
Kwa nyakati tufauti wakati akikagua miradi hiyo, Waziri Jafo ameshindwa kuizuia furaha yake na kupongeza kwa dhati ubora wa miradi hiyo ambayo ameiita kuwa ni ya mfano katika miradi mbalimbali inayoendelea hapa nchini huku akiwapongeza viongozi wa wilaya hiyo kwa ushirikiano na mshikamano mkubwa katika kutekeleza miradi hiyo.
“Bahi mnafanya vizuri sana katika mambo mengi hata katika miradi hii niliyoikagua leo yote imenifurahisha kwa kweli mmejipanga na mnashirikiana katika mambo yote hususan katika utekelezaji wa miradi hii.” Amesema Jafo na kuongeza;
“Nikiwa Chemba jana niliagiza katika zile fedha za madarasa hakikisheni katikati ya madarasa mawili mnaweka ofisi pamoja na vigae kwenye madarasa badala ya sementi lakini kumbe tayari Bahi mmeshajiongeza na mmefanya hongereni sana.”
Akizungumza mara baada ya kuwasili katika Hospitali ya Wilaya ya Bahi ambayo tayari huduma zimeanza kutolewa kwa wananchi, Waziri Jafo amefurahishwa na kuridhishwa na kiwango cha huduma zinazotolewa hospitalini hapo na kutoa cheti cha heshima cha Waziri wa Nchi OR - TAMISEMI kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dkt. Kasimu Kolowa kwa kusimamia vizuri shughuli za afya na kumuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma Mganga kumpatia shilingi laki moja kama motisha kwake.
“Ndugu zangu naiona Bahi mpya inakuja, mna hospitali nzuri ya mfano katika nchi, niwasifu sana viongozi pamoja na watendaji mmefanya vizuri sana, nimeambiwa hata katika elimu mmekuwa wa kwanza kimkoa katika matokeo ya Darasa la Saba mwaka huu (2020) hongereni kwa kupata viongozi wazuri.” Amesema Jafo.
Baada ya kukamilisha kukagua miradi Waziri Jafo alipata fursa ya kuzungumza na Watumishi wa Taasisi mbalimbali za Serikali zilizopo Bahi ambapo amewasihi kupendana na kufanya kazi kwa ushirikiano katika majukumu yao ili kwa pamoja waweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, amewaonya Wakuu wa Idara na viongozi kwa ujumla kuacha viburi katika kuwasimamia watumishi kwani kwa kufanya hivyo wanaondoa ari ya kazi na furaha kwa watumishi.
“Watumishi shirikianeni, pendaneni na kila mtumishi ahakikishe anawajali walio chini yake ili kila mmoja aweze kutimiza wajibu wake, acheni viburi ninyi mnaowasimamia watumishi shirikianeni katika kuwahudumia watu.” Amesema Waziri Jafo.
Pia, Waziri Jafo ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhama katika mfumo wa kuendesha vikao vya kisheria kwa kudurufu makabrasha na badala yake vitumike vishikwambi (Tablets) kama Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ilivyofanya kununua vishikwambi 50 kwa gharama ya shilini milioni 47 ambapo kwa kufanya hivyo imeokoa shilingi milioni 303 kati ya shilingi milioni 350 ambazo awali zilikuwa zikitumika kudurufu makabrasha ya vikao
“Niwatake Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini waone namna ya kuhama kutoka kwenye makaratasi kwenda kwenye TEHAMA, Bahi niwapongeze kwa kuwa wa kwanza nchini kuanza kutumia vishikwambi na wengine waje wajifunze kwenu nami kila natakapopita nitaendelea kuhimiza hili.”
Pamoja na pongezi nyingi alizozitoa kwa halmashauri ya Bahi, Waziri Jafo hakusita kuelezea dosari ya ukusanyajoi wa mapato na kusema baadhi ya watendaji wamekuwa wakitumia fedha hizo bila ya kuziingiza katika mfumo na kuagiza Mkurugenzi kusimamia jambo hilo kikamilifu.
Awali, akimkaribisha Waziri katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amemshukuru Waziri jafo kwa kufanya ziara hiyo na kumuahidi kuyasimamia vema maelekezo mbalimbali aliyoyatoa wakati akikagua miradi.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Bahi, Kenneth Nollo (Mb) amemshukuru Waziri Jafo na kuwapongeza Mkuu wa Wilaya ya Bahi na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kwa namna wanavyoshikamana katika kusimamia miradi ya maendeleo.
Akitoa neno la shukrani kwa Waziri Jafo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Donald Mejiti ameahidi kusimamia vema suala la ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha kila mtendaji anatimiza wajibu wake.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), Selemeni Jafo (Mb) akizungumza mara baada ya kusomewa taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Bahi wakati wa ziara yake aliyoifanya wilayani humo tarehe 31 Desemba 2020.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), Selemeni Jafo (Mb) akizungumza wakati akikagua miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo katika Shule za Msingi Bahi Misheni na Bahi Sokoni wakati wa ziara yake aliyoifanya wilayani humo tarehe 31 Desemba 2020.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), Selemeni Jafo (Mb) (kushoto) akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Msingi Bahi Misheni wakati wa ziara yake aliyoifanya wilayani Bahi tarehe 31 Desemba 2020.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), Selemeni Jafo (Mb) (katikati) akiwasili katika Jengo la Wagonjwa wa Nje - OPD la Hospitali ya Wilaya ya Bahi kwa ajili ya kujiridhisha na huduma za afya ambazo tayari zimeshaanza kutolewa, wakati wa ziara yake aliyoifanya wilayani humo tarehe 31 Desemba 2020.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), Selemeni Jafo (Mb) (aliyevaa suti nyeusi) akizungumza na baadhi ya wagonjwa waliofika Hospitali ya Wilaya ya Bahi kwa ajili ya kupata huduma za afya, wakati wa ziara yake aliyoifanya wilayani humo tarehe 31 Desemba 2020.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), Selemeni Jafo (Mb) akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na taasisi zote za Serikali wakati wa ziara yake aliyoifanya wilayani humo tarehe 31 Desemba 2020.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge akimkaribisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), Selemeni Jafo (Mb) (hayupo pichani) ili aweze kuzungumza na watumishi wa Wilaya ya Bahi wakati wa ziara iliyoifanywa na waziri huyo wilayani humo tarehe 31 Desemba 2020.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda akizungumza awali wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), Selemeni Jafo (Mb) (hayupo pichani) aliyoifanya wilayani humo tarehe 31 Desemba 2020.
Mbunge wa Jimbo la Bahi, Kenneth Nollo (Mb) akizungumza kwa niaba ya wananchi wa jimbo hilo wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), Selemeni Jafo (Mb) aliyoifanya tarehe 31 Desemba 2020.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Donald Mejiti akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), Selemeni Jafo (Mb) aliyoifanya tarehe 31 Desemba 2020.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI), Selemeni Jafo (Mb) (wa pili kulia) akimpongeza na kumkabidhi fedha taslimu shilingi laki mbili Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Bahi, Kassim Kolowa (kushoto) ambayo aliagiza itolewe na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi kama motisha kwa mtumishi huyo kwa utendaji wake mzuri. (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa