Na Benton Nollo na Bernard Magawa (DMC), Bahi
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga (Mb) ameagiza ujenzi wa vyuo vyote vya VETA unaoendelea nchi nzima kukamilika kabla ya tarehe 31 Machi 2021 ili majengo hayo yaanze kutumika mwaka huu.
Kipanga ametoa agizo hilo tarehe 20 Januari 2021 alipotembelea na kukagua ujenzi wa chuo cha VETA Wilaya ya Bahi ambapo hakuridhishwa na kasi ya ujenzi wa chuo hicho ambao unasimamiwa na Uongozi wa Chuo hicho kwa kutumia Force Account kwa gharama ya shilingi bilioni 1.6.
“Binafsi niseme wazi sijaridhishwa kabisa na mwenendo wa ujenzi wa chuo hiki na namna mlivyoandaa mpangilio wa kazi zenu, nitarudi tena hapa baada ya wiki moja na nitakapo kuja nikute kila jengo lina fundi wake na wanafanya kazi vinginevyo tusilaumiane kwani siwezi kuacha uzembe huu uendelee.” Amesema Kipanga na kuongeza;
“Niagize wale wote wanaosimamia miradi ya ujenzi wa vyuo vya VETA nchini kuhakikisha wanakamilisha miradi hii kabla ya tarehe 31 Machi 2021, na viongozi wa maeneo hayo simamieni kikamilifu ujenzi huo ili majengo hayo yaweze kufunguliwa na kuanza kazi mapema mwaka huu.”
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri huyo, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda ameahidi kusimamia kwa ukaribu na kuhakikisha ujenzi huo unakamilika haraka iwezekanavyo.
“Ujenzi umekuwa wa kusuasua sana, hata mimi sifurahishwi wala siridhishwi na ujenzi wa chuo chetu cha VETA Bahi, tuna watoto wengi mitaani ambao hawakufaulu kuendelea na masomo mengine na hatuna pa kuwapeleka zaidi ya VETA, sielewi tatizo liko wapi labda kwa sababu mamlaka haipo Halmashauri ipo wizarani.” Amesema Munkunda na kuongeza;
“Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kweli hili linatuchafua sisi kama Wilaya kwa sababu mambo haya hatujazoea, sisi tumekuwa tukifanya vizuri katika miradi mingine ambayo fedha zilipita Halmashauri.”
Naye, Makamu Mkuu wa Chuo cha VETA Mkoa wa Dodoma, Stanslaus Ntibala amesema kusuasua kwa ujenzi huo kunatokana na changamoto mbalimbali ikiwemo vifaa vya ujenzi kuchelewa kupelekwa na wazabuni ilhali tayari walishalipwa.
Ujenzi wa chuo cha VETA Bahi unaojumuisha ujenzi wa majengo 17 ulianza mwezi Mei 2020 na ulitakiwa kukamilika mwezi Desemba 2020.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa