Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli (pichani), Ijumaa tarehe 13 Novemba 2020, atafungua rasmi Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kulihutubia Taifa kupitia Bunge hilo, Bungeni jijini Dodoma.
Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai amewaambia wabunge katika kikao cha tatu, kilichofanyika leo tarehe 12 Novemba 2020, kwamba Rais Dkt. Magufuli ataanza kutoa Hotuba yake saa 4:00 asubuhi na kuwataka Wabunge kuhakikisha kila mmoja ameingia Bungeni Saa 3:00 asubuhi ili kuwa tayari kwa hotuba hiyo.
"Waheshimiwa Wabunge, sasa naahirisha kikao hiki cha Bunge ili kupisha maandalizi ya ukumbi huu kwa ajili ya ugeni huu wa Mheshimiwa Rais, na ninawaombeni kesho mjitahidi kuwahi kufika Bungeni saa 3:00 asubuhi kwa sababu shughuli hiyo ya kesho ni muhimu sana.” Amesema Spika Ndugai.
Mapema Bungeni leo, Spika wa Bunge alipokea barua kutoka kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya pendekezo la jina la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo baada ya kuifungua alimtangaza Mbunge wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi, Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) kuwa ndiye aliyependekezwa na Rais Dk. Magufuli.
Kufuatia pendekezo hilo la Rais Dkt. Magufuli, Bunge lilifanya uchaguzi uliompitisha Majaliwa kwa kura 354 zilizopigwa na wajumbe wa Bunge (MB) na kumfanya Majaliwa kuwa amepita kwa asilimia 100.
Baadaye ulifanyika Uchaguzi wa Naibu Spika ambapo Dkt. Tulia Akson aliyekuwa mgombea pekee, naye alipigiwa kura na Wajumbe ambapo amechaguliwa kwa kura 350 kati ya kura 354 zilizopigwa.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa