Na Benton Nollo na Bernard Magawa (DMC), Bahi
Naibu Waziri wa Kilimo, Husein Bashe ameagiza kuanzishwa kwa kilimo cha zao la ngano wilayani Bahi baada ya wataalamu wa kilimo kufanyia utafiti eneo hilo na kuonekana kuwa linafaa kwa kilimo cha zao hilo.
Bashe ameyasema hayo Desemba 15, 2020 alipofanya ziara ya siku moja wilayani humo kwa lengo la kupokea taarifa ya matokeo ya utafiti wa majaribio ya kilimo cha ngano na kuona ngano iliyovunwa katika mashamba ya mfano.
Bashe ameagiza kufanyika kwa utambuzi wa wakulima wa skimu zote za Bahi kabla ya tarehe 30 Machi 2020 ili eneo lote la kilimo lipate Hati Miliki na kuwasihi Wakulima wanaouza mashamba yao kiholela kwa wageni waache mara moja kwani maeneo hayo ni mali ya Serikali.
Pia, Bashe ameshauri haraka ijengwe ofisi ya kusimamia shughuli za kilimo cha umwagiliaji ambapo amemuagiza Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao, Wizara ya Kilimo, Nyasebwa Chimagu kuchangia shilingi milioni tano katika ujenzi huo na kuwaomba wakulima kuchangia nguvu kazi kwa kushiriki kikamilifu ujenzi huo ikiwa ni pamoja na kuchimba msingi na shughuli nyingine ili ofisi hiyo ikamilike haraka.
Aidha, Naibu Waziri huyo amewatoa hofu wananchi na wakulima kuhusiana na upatikanaji wa mbegu bora za ngano. Pia, kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Bashe amewahakikishia wakulima uwepo wa soko la uhakika.
“Lengo la jambo hili ni kumfanya mkulima alime mara mbili kwa mwaka, niwaambie wananchi kuwa kilimo siyo shughuli inayofanywa na watu masikini tu, bali hufanywa na watu wote. Niwaahidi kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo italeta mbegu kwa wakulima wote wa ngano ili tuanze mara moja shughuli hii, naomba viongozi mnipatie taarifa kila mwezi maendeleo ya mradi huu.” Amesema Bashe.
Awali akitoa taarifa ya majaribio ya kilimo cha zao hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amesema utafiti huo umeonyesha mafanikio makubwa katika eneo hilo na tayari wilaya imeshaandaa hekta 412 za kuanzia ili baada ya wakulima kuvuna mpunga waweze kupanda ngano, zao ambalo linahitajika kwa wingi hapa nchini.
“Majaribio ya ustawishaji wa Ngano yalianza tarehe 06 Augosti 2020 na kufikia tarehe 06 Oktoba 2020 tukavuna mazao yakiwa yamekomaa vizuri kabisa hivyo, Mheshimiwa Waziri Ngano ni zao linalokubali katika maeneo yetu.” Amesema Munkunda.
Kwa upande wake Afisa Mtafiti Mkuu wa Kilimo Taasisi ya Utafiti wa Mazao – TARI, Dkt. Rose Mongi amesema utafiti pamoja na majaribio ya shamba darasa katika Wilaya ya Bahi vimefanyika kwa mafanikio makubwa hivyo, eneo la Bonde la Bahi linafaa kabisa kwa kilimo cha ngano.
“Mheshimiwa Naibu Waziri, majaribio yalilenga kuanzisha kilimo cha ngano katika Wilaya ya Bahi na ngano ilipandwa baada ya kuvuna mpunga, wakulima wameshuhudia mavuno yaliyotokana na zao hilo. Hivyo zao hili litawawezesha kulima mara mbili kwa mwaka na kujiongezea kipato mara mbili.” Amesema Dkt. Mongi.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima walioshiriki zoezi la utafiti, Eliyona Sindato ameipongeza serikali kwa uamuzi huo na kusema kwamba wao kama washiriki wamebaini kuwa gharama za kilimo cha ngano ni ndogo ukilinganisha na kilimo cha Mpunga.
“Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya wakulima wenzangu tumebaini ngano ni zao linalokubali katika ardhi ya Bahi na tumevuna, haina gharama kama tunavyolima mpunga, ngano ya Bahi tumeivuna kwa muda mfupi ukilinganisha na maeneo mengine.” Amesema Sindato.
Naye, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Donald Mejiti amewasihi wananchi kulipokea jambo hilo kama fursa kwao ili waweze kusonga mbele kimaendeleo.
“Wananchi wenzaangu tuchangamkie fursa hii, na nikuahidi Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba hili jambo tumelipokea kwa mikono miwili na tutahamasisha wananchi ili tulime kwa wingi.” Amesema Mejiti.
Wilaya ya Bahi ni miongoni mwa maeneo yanayozalisha kwa wingi zao la mpunga hivyo, kuanzishwa kwa kilimo hiki cha ngano itakuwa fursa nyingine kwa wakulima kujiongezea kipato.
Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utafiti na majaribio kilimo cha zao la Ngano ofisini kwa Mkuu wa WIlaya ya Bahi iliyowasilishwa kwake wakati wa ziara ya siku moja aliyoifanya wilayani Bahi tarehe 15 Desemba 2020.
Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akizungumza na viongozi wa skimu za umwagiliaji za Bahi na wakulima walioshiriki majaribio ya kilimo cha Ngano katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya wilayani Bahi tarehe 15 Desemba 2020.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (katikati) akizungumza kabla ya kumkaribisha Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (kushoto) ili azungumze na wakulima wa skimu za umwagiliaji za Bahi. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma Mganga. Bashe alifanya ziara wilayani Bahi tarehe 15 Desemba 2020.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma Mganga (katikati) akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliyoifanya wilayani Bahi tarehe 15 Desemba 2020. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda na kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Bahi, Jeremia Mapogo.
Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (kulia) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Donald Mejiti (kushoto) wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani Bahi tarehe 15 Desemba 2020.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko - CPB, Dkt. Anselm Moshi akizungumza akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliyoifanya wilayani Bahi tarehe 15 Desemba 2020.
Afisa Mtafiti Mkuu wa Kilimo Taasisi ya Utafiti wa Mazao – TARI, Dkt. Rose Mongi akizungumza akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aliyoifanya wilayani Bahi tarehe 15 Desemba 2020.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Mazao, Wizara ya Kilimo, Nyasebwa Chimagu (kushoto mbele) pamoja na viongozi waandamizi wa wizara hiyo wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe (hayupo pichani) wakati akizungumza na wakulima katika ziara yake aliyoifanya wilayani Bahi tarehe 15 Desemba 2020.
Wakulima walioshiriki katika majaribio ya kilimo cha ngano wakitoa ushuhuda kwa nyakati tofauti juu ya ustawi wa zao hilo mbele ya Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati wa ziara yake aliyoifanya wilayani Bahi tarehe 15 Desemba 2020.
Zao la Ngano iliyovunwa katika mashamba ya majaribio yaliyolimwa Bahi.
Naibu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (aliyevaa suti ya kijivu) akizungumza mara baada ya kutembelea Mto Bubu ambao ndiyo chanzo kikuu cha kilimo cha umwagiliaji katika skimu mbalimbali za Bahi. (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa