Benton Nollo na Rosemary Celu (DMC), Mundemu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Ummy Mwalimu (Mb) ametoa wito kwa Halmashauri zote nchini kuja kujifunza Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ambayo imetumia vema asilimia 40 ya mapato ya ndani katika kutatua kero za wananchi.
Waziri Ummy ameonesha kuridhishwa na ubora wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo wakati wa ziara yake ya siku moja alipotembelea wilayani Bahi tarehe 08 Mei 2021 kukagua miradi hiyo na kuzungumza na Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango pamoja na Timu ya Menejimenti ya Halmashauri - CMT.
Akiwa katika Shule ya Sekondari Mundemu, Waziri Ummy alikagua ujenzi wa bweni, madarasa mawili yenye ofisi katikati na choo chenye matundu 8 yaliyojengwa kwa kutumia fedha za Awamu ya Nane za Mradi wa Lipa Kulingana Matokeo - EP4R mwaka 2020.
Akiwa shuleni hapo, Waziri Ummy alionyesha kuridhishwa na usimamizi wa fedha za miradi hiyo kwani thamani ya fedha inaonekana.
“Bahi mmepokea shilingi milioni 128 na mmefanikiwa kujenga bweni, madarasa mawili na matundu ya vyoo na miradi yote imekamilika tena kwa ubora unaotakiwa hongereni sana viongozi wa Bahi”. Amesema Waziri Ummy na kuongeza;
“Kuna halmashauri nyingine wameshindwa kukamilisha ujenzi wa bweni kwa milioni 80 sasa niwatake wote waje kujifunza Bahi namna bora ya usimamizi wa fedha za miradi ya maendeleo."
Katika hatua nyingine Waziri Ummy ameridhishwa na upelekaji wa asilimia 40 ya fedha za mapato ya ndani kwenye miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo ambayo kimsingi inatatua kero mbalimbali za wananchi.
“Mpaka sasa Bahi mmekusanya zaidi ya shilingi milioni 900 na kwenye miradi mmepeleka shilingi milioni 380 hiki ndicho ninachotaka kukiona kwenye Halmashauri zote, upelekaji wa fedha za miradi unapewa kipaumbele."
"Kizuri zaidi kwa Bahi ni kuwa fedha unaona zimeenda kwenye ujenzi wa zahanati, madarasa, mabweni yaani miradi ile halisi ya maendeleo na sio kulipana posho za safari na vikao fedha zimefanya kazi za maendeleo."
Wakati wa ziara hiyo, Waziri Ummy ameahidi kupeleka Gari la Wagonjwa kwa ajili ya Kituo cha Afya Mundemu pamoja na shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bwalo la chakula katika Shule ya Sekondari Mundemu.
Aidha, kufuatia ukongwe wa Shule ya Sekondari Mundemu na kwa kuwa inafanya vizuri katika matokeo ya Kidato cha Nne pamoja na miundombinu iliyoboreshwa, Waziri Ummy ameahidi kuipandisha hadhi shule hiyo kwamba kuanzia Julai 2022 itapangiwa wanafunzi wa Kidato cha Tano.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge ameshukuru na kumpongeza Waziri Ummy kuchagua mkoa huo kuwa wa kwanza kufanya ziara tangu ateuliwe kushika wadhifa huo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Sita, Samia Suluhu Hassan.
“Mheshimiwa Waziri uniruhusu kwa niaba ya wananchi wote wa Dodoma nikushukuru kwa ziara yako…katika wilaya zangu saba, Halmashauri nane, wilaya hii wanafanya kazi vizuri…wako vizuri kwenye elimu, wako vizuri kwenye afya, wako vizuri kwenye asilimia 10, wako vizuri kwenye mapato”. Amesema Dkt. Mahenge na kuongeza;
“Inawezekana wakawa hawana mapato makubwa lakini utekelezaji wa taratibu, sheria na kanuni wanaongoza katika Halmashauri zangu zote, ukienda kwenye asilimia 10 wanazipeleka zote kama walivyopanga, ukienda kwenye asilimia 40 za maendeleo wanazipeleka zote kama walivyopanga, lakini siri yao kubwa ni mshikamano wa pamoja katika kutekeleza majukumu yao”.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amesema kwamba Shule ya Sekondari Mundemu ni shule maalum kwa masomo ya sayansi katika wilaya hiyo kwani inapokea watoto kutoka katika kata zote 22 za Bahi wanaofanya vizuri masomo ya sayansi katika Mtihani wa Darasa la Saba lakini pia kwa sababu hiyo haiwaachi watoto wa Kata ya Mundemu.
“Kata zote 22 za Wilaya ya Bahi zina watoto hapa…tuliamua kufanya hivi makusudi ili kuendelea kulea vipaji vya sayansi, kwahiyo watoto wote bora katika masomo ya sayansi tunawaleta hapa…lakini pia hatuwaachi watoto wa kata hii kwa sababu ni shule yao.” Amesema Munkunda.
Awali akisoma taarifa ya mradi wa EP4R Awamu ya Nane, Mkuu wa Shule ya Sekondari Mundemu, Reuben Nchimbwi amesema kuwa shule yake ilipokea shilingi milioni 128.8 tarehe 26 Juni 2020 ambapo kwa kutumia Force Account mradi ulianza kutekelezwa kwa kuunda kamati za manunuzi, ukaguzi na mapokezi na kamati ya ujenzi ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha jamii na wadau mbalimbali.
Pamoja na mambo mengine Waziri Ummy ameweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Bweni la Wanafunzi Shule ya Sekondari Mundemu, amekagua Barabara ya Mundemu – Msisi – Lamaiti – Bankolo – Mkakatika – Bahi yenye urefu wa kilomita 38 inayosimamiwa na TARURA ambayo imeharibiwa na mvua za masika na kisha amekagua utoaji wa huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Bahi ambapo napo ameweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Hospitali hiyo.
Matukio katika Picha:
Picha zote juu ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu (Mb) akikagua Bweni la Wanafunzi (lililopewa jina la Mshikamano) na Madarasa Mawili wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya wilayani Bahi tarehe 08 Mei 2021. Miundombinu hiyo imejengwa kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo - EP4R Awamu ya Nane mwaka 2020.
Picha zote juu ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu (Mb) alipotembelea Hospitali ya Wilaya ya Bahi kukagua utoaji wa huduma wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya wilayani Bahi tarehe 08 Mei 2021.
Picha zote juu ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ummy Mwalimu (Mb) alipotembelea kukagua Barabara ya Mundemu – Msisi – Lamaiti – Bankolo – Mkakatika – Bahi yenye urefu wa kilomita 38 inayosimamiwa na TARURA ambayo imeharibiwa na mvua za masika wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya wilayani Bahi tarehe 08 Mei 2021. (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa