Na Benton Nollo na Bernard Magawa (DMC), Bahi.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bahi limepitisha Bajeti ya Halmashauri hiyo yenye thamani ya shilingi bilioni 25 kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Kikao maalum cha Baraza la Madiwani kimefanyika tarehe 12 Februari 2021 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Bahi ambapo Waheshimiwa Madiwani wameiomba Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani ihakikishe kuwa inakamilisha ujenzi wa maboma yote ya shule na zahanati yaliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi ili kurudisha imani kwao kutokana na majitoleo waliyoyafanya katika miradi hiyo.
Akizungumza katika Baraza hilo Diwani wa Kata ya Ibugule, Blandina Magawa amesema kwamba ili kuunga mkono juhudi na nguvu kazi za wananchi ni vema katika bajeti hiyo Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani ijikite zaidi kukamilisha maboma ya madarasa na zahanati yaliyopo kuliko kuanzisha miradi mipya hali ambayo itawapa moyo wananchi kujitoa zaidi.
“Mheshimiwa Mwenyekiti katika kata yangu nina maboma matatu yalijengwa kwa nguvu za wananchi, madarasa mawili na maabara moja ambayo hayajamaliziwa, naiomba Serikali kupitia Halmashauri imalizie majengo haya ili turudishe imani kwa wananchi kwa sababu tuliwaahidi wananchi waanzishe halafu serikali itamalizia, lakini inasikitisha majengo hayo yametelekezwa kwa muda mrefu sana.” Amesema Magawa.
Aidha, Baraza la Madiwani limeiagiza Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini - RUWASA kuhakikisha inakuwa na mipango inayotekelezeka katika kusogeza huduma za maji kwa wananchi na kuacha kuahidi mipango isiyo na matumaini kwani inaleta usumbufu kwa baadhi ya viongozi wa maeneo husika.
Pia, Baraza limeiagiza ofisi ya Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini - TARURA kuhakikisha wanaimarisha miundombinu ya barabara vijijini ili ziweze kutumika kipindi chote cha mwaka kwani barabara nyingi zinaharibika inapofika kipindi cha masika.
Awali akiwasilisha Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya hiyo, Afisa Mipango wa Wilaya, Charles Mduma amesema bajeti hiyo imezingatia mambo yote muhimu ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo, Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020, Sheria ya Bajeti pamoja na maendeleo endelevu.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi inalenga kukusanya na kutumia shilingi milioni 25,084,770,216/= kutoka katika vyanzo mbalimbali.” Amesema Mduma.
Afisa Mipango huyo alifafanua kuwa mapato ya ndani ni shilingi bilioni 1,500,000,000/= (6%), Matumizi ya Kawaida shilingi bilioni 1,000,0024,609/= (4%), Mishahara shilingi bilioni 14,859,440,998/= (59%) na miradi ya maendeleo shilingi bilioni 7,725,304,609/= (31%).
Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Donald Mejiti amewasisitiza wajumbe kuhakikisha kuwa wao kama viongozi, wanasimamia na kudhibiti uanzishwaji wa makazi mapya mbali na huduma za jamii bila kufuata utaratibu badala yake wakae katika vijiji ambako Serikali imewekeza fedha nyingi kujenga miundombinu na huduma mbalimbali ikiwemo shule na zahanati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma Mganga akifafanua jambo wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani kujadili Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Halmashauri ya Bahi kwa mwaka fedha 2021/2022 kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo tarehe 12 Februari 2021.
Afisa Mipango Wilaya ya Bahi, Charles Mduma akiwasilisha Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Halmashauri ya Bahi kwa mwaka fedha 2021/2022 katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo tarehe 12 Februari 2021.
Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Wilaya ya Bahi, ASP Juma Solomoni akibu hoja ya Diwani wa Kata ya Chipanga, Masumbuko Kawindi (hayupo pichani) kuhusu kukiboresha Kituo cha Polisi cha Chipanga ili kiweze kutoa huduma bora kwa wananchi wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichoketi kujadili Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo tarehe 12 Februari 2021.
Baadhi ya Waheshimiwa Madiwani wakichangia hoja wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichoketi kujadili Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Halmashauri ya Bahi kwa mwaka fedha 2021/2022 kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo tarehe 12 Februari 2021.
Meneja wa TANESCO Wilaya ya Bahi, Bryceson Kitila akijibu baadhi ya hoja zinazohusu masuala ya umeme wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichoketi kujadili Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Halmashauri ya Bahi kwa mwaka fedha 2021/2022 kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo tarehe 12 Februari 2021.
Meneja Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini - TARURA, Mhandisi John Chalula akiwasilisha bajeti ya barabara wilayani humo wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichoketi kujadili Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Halmashauri ya Bahi kwa mwaka fedha 2021/2022 kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo tarehe 12 Februari 2021.
Mwakilishi wa Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini Wilaya ya Bahi, Boniface Bihemu akijibu baadhi ya hoja zinazohusu masuala ya maji wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichoketi kujadili Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Halmashauri ya Bahi kwa mwaka fedha 2021/2022 kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo tarehe 12 Februari 2021.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bahi, Sterwart Masima akizungumza wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichoketi kujadili Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Halmashauri ya Bahi kwa mwaka fedha 2021/2022 kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo tarehe 12 Februari 2021.
Baadhi ya Waheshimiwa Madiwani, Wakuu wa Idara na Vitengo wakifuatilia wasilisho la Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Halmashauri ya Bahi kwa mwaka fedha 2021/2022 wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo tarehe 12 Februari 2021. (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa