Maafisa Habari, Uhusiano na Mawasiliano Serikalini wapongezwa kwa kutangaza vizuri shuguli za Serikali ikiwemo miradi inayotekelezwa, ambayo itawaletea wananchi maendeleo.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Ally Possi leo jijjini Dodoma wakati akifunga mafunzo ya kimkakati ya Uandishi wa Habari za Serikali ya awamu ya pili kwa Maafisa hao ambapo amewataka kutumia elimu waliyopata kuendelea kuhabarisha umma kwa weledi na kwa usahihi habari zinazohusu Serikali.
“Maafisa Habari mnafanya vizuri katika kutangaza shughuli za Serikali kwa wananchi, naomba muendelee kufanya hivyo kwa kuwa kada yenu ni muhimu katika kufikisha ujumbe wa Serikali kwa wanachi na mtumie kalamu zenu vizuri ili kulinda na kudumisha amani ya nchi yetu”. Alisema Dkt. Possi.
Aidha, Dkt. Possi amewataka waandaaji wa mafunzo hayo kuendelea kutoa mafunzo hayo mara kwa mara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kutumia mifumo tofauti ya ndani na nje ya nchi pamoja na kufanya tathmini ili kuona mabadiliko yaliyopatikana kutokana na mafunzo hayo.
Hata hivyo, Dkt. Possi aliwashauri Maafisa Habari wote wa Serikali kujiunga na Chama cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali (TAGCO) ili kurahisisha mawasiliano miongoni mwao pamoja na kushirikiana katika kazi wanazofanya ikiwemo kubadilishana uzoefu na kusaidiana kijamii na kitaaluma.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari –MAELEZO, Rodney Thadeusi amesema kuwa jukumu la Maafisa Habari wa Serikali ni kutoa taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu Serikali kwa wananchi kwa kutumia njia zote za mawasiliano.
“Maafisa Habari kazi yetu kubwa ni kuisemea Serikali, tusiposema sisi wengine watasema na wengine wanaweza kusema ambayo sio sahihi na wakati mwingine kukosoa hata yale mazuri ambayo Serikali inatekeleza kwa wananchi wake, hivyo tuendelee kutumia taaluma yetu kuitangaza vizuri Serikali”. Alisema Thadeusi.
Naye Makamu Mwenyekiti wa TAGCO, Sara Msika amesema lengo la mafunzo hayo ni kuendelea kuboresha taaluma ya maafisa hao katika kipindi hiki ambacho dunia imekuwa na mabadiliko makubwa katika kada hii ya uandishi wa habari .
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo Afisa Habari kutoka TBC, Catherine Nyoni ameshukuru waandaaji wa mafunzo hayo kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo kwa Maafisa Habari Serikalini ambayo yamesaidia kuboresha taaluma yao pamoja na kubadilishana uzoefu.
Mafunzo hayo ya siku tano yalioandaliwa na Idara ya Habari –MAELEZO pamoja na Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) yamekuwa na mada mbalimbali ikwemo namna ya kutumia mitandao ya kijamii kuhabarisha umma pamoja na uandishi mzuri wa habari za Serikali. Aidha, Mafunzo kama hayo kwa awamu ya kwanza yalifanyika jijini Dodoma tarehe 16 hadi 20 Septemba 2019.
Baadhi ya Washiriki wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa