Na Benton Nollo, Bahi
Wananchi wilayani Bahi wametakiwa kupanda miti na kutunza mazingira kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bahi, Jeremia Mapogo wakati akizindua Kampeni ya Upandaji Miti wilayani humo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo tarehe 24 Desemba 2019, zoezi ambalo limefanyika katika Kijiji cha Bahi Sokoni.
Mapogo amesema kuwa miti ni rasilimali muhimu sana kwa mustakabali wa uhai wa binadamu na viumbe vingine duniani, hivyo inatakiwa kulindwa na kuhifadhiwa.
Amesema kuwa hali ya hewa ya Bahi imekuwa na ukame mkubwa kwa sababu kasi ya watu kuharibu mazingira kwa kukata miti ovyo ni kubwa mno.
“Ndugu zangu wananchi, mtakubaliana na mimi kuwa tumekuwa wabinafsi sana kwa kujijali sisi tuliopo duniani leo, tunakata miti ovyo ili kukidhi mahitaji yetu ya sasa bila kupanda miti mingine ya kutosha ili pia kizazi kijacho kije kunufaika nayo”. Amesema Mapogo na kuongeza.
“Hebu tujiulize leo, hivi babu na bibi zetu wasinge tunza mazingira, si tungekuwa kwenye jangwa la hatari. Basi kama ndivyo, tutambue kuwa tunawajibu mkubwa wa kutunza miti ya asili iliyopo na kupanda mingine mipya”.
Mapogo ametoa wito kwa wafugaji wanaoachia mifugo yao kiholela na kuchungisha miti ambayo inanunuliwa na kutunzwa kwa gharama kubwa na kutoa onyo kwamba yeyote atakayebainika kufanya hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Aidha, akizungumza awali Afisa Mazingira Wilaya ya Bahi, Agnetha Maseko amesema kuwa lengo la wilaya hiyo kwa mwaka 2019/2020 ni kupanda miti milioni 1.5 lakini mpaka sasa Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS) imeipatia wilaya hiyo miche ya miti elfu 50.
Maseko amesema tayari imeshagawanywa katika Kata 22 za wilaya hiyo na kila kata imepata miche 2,272.
Picha na Matukio:
Katibu Tawala Wilaya ya Bahi, Jeremia Mapogo akizungumza na wananchi waliojitokeza kushiriki uzinduzi wa Kampeni ya Upandaji Miti wilayani humo kwa mwaka 2019/2020 uliofanyika katika Kijiji cha Bahi Sokoni tarehe 24 Desemba 2019. Mapogo alimuwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo.
Afisa Mazingira Wilaya ya Bahi, Agnetha Maseko akitoa taarifa ya utunzaji wa Mazingira wilayani humo kwa mgeni rasmi na wananchi waliojitokeza kushiriki uzinduzi wa Kampeni ya Upandaji Miti wilayani humo kwa mwaka 2019/2020 uliofanyika katika Kijiji cha Bahi Sokoni tarehe 24 Desemba 2019.
Baadhi ya Wataamu na wananchi wakimsikiliza mgeni rasmi (hayupo pichani) baada ya kushiriki uzinduzi wa Kampeni ya Upandaji Miti wilayani humo kwa mwaka 2019/2020 uliofanyika katika Kijiji cha Bahi Sokoni tarehe 24 Desemba 2019. (Picha zote na Benton Nollo)
Halmashauri ya Wilaya ya Bahi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 687748878
Simu: +255 687748878
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa