Na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge Juni 06, 2018 amekutana na kufanya Mazungumzo na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Nchi ya Uganda Mhe. Monica Azuba Ntege Ofisini kwake Jijini Dodoma ambapo Waziri huyo amepongeza jitihada za Serikali ya Tanzania za Ujenzi wa Reli ya Kisasa ya Umeme ya Mwendo Kasi - SGR.
Waziri Ntege amesema kuwa mradi huo wa Reli ya Kisasa ya Umeme inayojengwa na Serikali ya Tanzania ina umuhimu mkubwa kwenye shughuli za kiuchumi na usafirishaji wa mizigo ikitokea Bandari ya Dar es Salaam kuelekea ukanda wa Ziwa Victoria kupeleka mizigo hiyo nchini Uganda na kuwa inaweza pia kuhudumia nchi nyingine za jirani kama Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo - DRC.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Uganda, Mhe. Monica Azuba Ntege (kulia) akisisitiza jambo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Dkt. Binilith Mahenge (kushoto) wakati wa mazungumzo baina ya viongozi hao wawili yaliyofanyika Jijini Dodoma Juni 06, 2018. Wengine ni Maafisa kutoka serikali ya uganda na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Dodoma. Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Pia, Waziri Ntege amepongeza ushirikiano mzuri uliopo baina ya Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania na Rais Yoweri Kaguta Museven wa Uganda na kusema kuwa ushirikiano huo utazinufaisha nchi hizi mbili kwenye nyanja mbalimbali za uchumi na maendeleo na kuongeza kuwa ipo haja ya Serikali yao ya Uganda kukaa na kuwafahamisha Wafanyabiashara wa Uganda namna watakavyonufaika na Reli ya Kisasa ya Umeme ya Mwendo Kasi - SGR inayojengwa hapa Tanzania mara itakapokamilika ujenzi wake.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Dkt. Binilith Mahenge amemfahamisha Waziri Ntege kuwa Jiografia ya Mkoa wa Dodoma kuwa katikati ya nchi inatoa urahisi wa kuzihudumia nchi za jirani kama Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo - DRC ukilinganisha na mikoa kama Dar es Salaam.
Dkt. Mahenge ameongeza kuwa miradi ya ujenzi inayotekelezwa na Serikali kama huo wa Reli ya Kisasa ya Umeme na Mradi wa Uwanja wa Ndege wa Kisasa wa Kimataifa wa Msalato ambao tayari Serikali inatarajia fedha za ujenzi wake zitatoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na Mpango wa Mamlaka ya Bandari TPA kujenga Bandari Kavu Mkoani Dodoma. Alisema kwa pamoja miradi hii inazidi kuuongezea Mkoa wa Dodoma uwezo wa kuzihudumia nchi hizo za jirani kwa shughuli za kibiashara na uchumi. Tanzania na Uganda ni miongozi mwa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Dkt. Binilith Mahenge (kushoto) akisisitiza jambo kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wa Uganda, Mhe. Monica Azuba Ntege (kulia) na ujumbe alioambatana nao wakati wa mazungumzo mafupi baina ya viongozi hao Juni 06, 2018 Jijini Dodoma. Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa