Na Benton Nollo na Bernard Magawa (DMC), Bahi
Baraza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Bahi limeazimia na kuweka utaratibu utakaowalazimu watu wote watakao nunua ardhi na wenye leseni za madini ya ujenzi katika wilaya hiyo kuchangia mapato ya ndani.
Azimio hilo limetolewa katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika tarehe 29 Januari 2021 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Bahi ikiwa ni siku ya pili.
Wajumbe wa baraza hilo wameridhia kuwa katika Kata 22 za wilaya hiyo mtu yeyote atakayehitaji kununua ardhi sasa atatozwa shilingi 100,000/=, kwa ekari moja isipokuwa katika Kata ya Zanka na Mundemu ambapo wahusika watatozwa shilingi 200,000/= kwa ekari moja kila.
Wakati huo huo Baraza hilo limeazimia kwa wamiliki wa leseni za majini ujenzi (mchanga, mawe na kokoto) wao watatozwa shilingi 150,000/= kwa ekari moja kila mwaka.
Baraza hilo limeazimia kwamba fedha zote zitakazopatikana kutoka kwenye vyanzo hivyo zitaelekezwa moja kwa moja katika Mfuko wa Elimu wa Wilaya ya Bahi ili kuwawezesha watoto ambao wazazi wao wanakosa uwezo wa kuwaendeleza kimasomo na kusadia kuboresha huduma za elimu ikiwemo upatikanaji wa madawati na vyumba vya madarasa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika kikao hicho Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi wamesema kumekuwa na wimbi kubwa la uuzaji wa ardhi kiholela wilayani humo kwa kiasi kidogo cha fedha ambacho kiuhalisia haziwasaidii wamiliki wa maeneo hayo badala yake wanunuzi ndiyo wamekuwa wakipata faida kubwa kwani ardhi imekuwa ikipanda thamani kila siku.
“Kuanzia leo, mauziano ya ardhi katika wilaya yetu kwa kata 2 za Mundemu na Zanka mnunuzi atachangia shilingi 200,000/= kwa kila ekari moja atakayo nunua, na kwa kata nyingine zote 20 mnunuzi atachangia shilingi 100,000/= kwa kila ekari moja, na wote wanaomiliki leseni za madini ujenzi kama mchanga, kokoto na mawe katika maeneo yetu wao watachangia shilingi 150,000/= kila ekari kwa mwaka.” Anasema Antony Lyamunda mujmbe na Diwani wa Kata ya Makanda.
“Mheshimiwa Mwenyekiti hivi sasa ardhi katika maeneo yetu ipo mbioni kuisha kutokana na ongezeko la watu na wimbi la uuzaji holela wa ardhi unaofanywa na wananchi wetu kwa sababu ya kutokujua thamani yake…hivyo kuna watu wanawalaghai na wanauza ardhi kwa bei ndogo sana ambapo hata kwa kufanya hivyo shida zao haziishi na wanaendelea kubaki masikini.” Anasema Mathayo Malilo, Diwani wa Kata ya Msisi.
Azimio hilo limetolewa baada ya Afisa Mipango wa Wilaya ya Bahi, Charles Mduma kuwasilisha mapendekezo ya kuongeza vyanzo vya mapato katika wilaya hiyo lakini pia baada ya kuona wananchi wananyonywa na kubaki masikini wakati wanayo rasilimali muhimu inayoweza kuwanufaisha wananchi hususan katika kuimarisha Mfuko wa Elimu wa Wilaya ya Bahi ambao utawasaidia watoto wengi wahitaji wa elimu na hatimaye kuikwamua jamii ya Bahi kielimu.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa