Benton Nollo na Alinikyisa Humbo, Bahi
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Said Jafo (Mb), amefurahishwa na kuupongeza uongozi wa Wilaya ya Bahi kwa jinsi ambavyo wamejitoa kusimamia ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo.
Jafo ameyasema hayo Julai 10, 2019 alipotembalea kukagua maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo inayojengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.5 kwa mfumo wa “Force Account”.
Baaada ya kukagua majengo yote saba, Jafo hakusita kuonesha furaha yake mbele ya viongozi wa wilaya hiyo na kusema kuwa ujenzi unaendelea vizuri sana na alitumia fursa hiyo kuwapongeza kwa ushirikiano mzuri na hasa hatua ya kuimarisha usimamizi ya kuwagawia Wakuu wa Idara na Vitengo majengo.
“Viongozi, watendaji wote na wananchi wa Bahi mimi naomba niwapongeze katika wilaya hazizidi tano zilizonifurahisha zaidi ninyi Bahi mpo na mnawezekana katika tatu bora nyie mpo na kilichonifurahisha zaidi hii kazi mlianza kwa kuchelewa sana ukilinganisha na wilaya nyingine lakini nyie mliochelewa ndiyo mmekuwa wa kwanza zaidi, lakini siyo wa kwanza kwa vile mnamaliza tu, mmekuwa kwanza na majengo mazuri mno”. Anasema Jafo na kuongeza.
“Mimi kama Waziri wa TAMISEMI niliyepewa dhamana na Mheshimiwa Rais katika ujenzi wa hospitali 67, na sasa hivi tumeongeza nyingine 27, hospitali 94 kwa mara ya kwanza katika wilaya najivunia, Wilaya ya Bahi mmefanya kazi nzuri mno”.
Pia, Jafo alieleza kufurahishwa na utekelezaji wa agizo alilolitoa mwanzo kwa wilaya zote 67 kuwa zihakikishe katika majengo saba yanayojengwa yanakuwa na mfumo wa uvunaji wa maji ya mvua pamoja na usimikaji wa mifumo ya kielektroniki ili kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya serikali wakati wa kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.
“Kitu kingine kilichonifurahisha zaidi kwenu, sijui katika wilaya nyingine kama wamezingatia huenda labda kwa sababu hawajamaliza, ni kwamba nimeona mmeweka gata kwa ajili ya uvunaji wa maji ya mvua kwani hili lilikuwa ni agizo langu la kwanza kwamba majengo yote yatakayojengwa lazima kusimikwe mifumo ya ukusanyaji mapato ya kielektroniki na uvunaji wa maji ya mvua hivyo naona hakuna maji yatakayopotea”. Alisema Jafo.
Hospitali ya Wilaya ya Bahi ni miongoni mwa hospitali 67 zinazojengwa na Serikali ya Awamu ya Tano nchini kwa gharama ya shilingi bilioni 1.5 na ipo katika hatua za ukamilishwaji.
Matukio katika picha:
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Said Jafo (Mb), (mwenye tai nyekundu) akitoka kukagua jengo la kuhifadhia dawa ambalo ni miongoni mwa majengo saba yanayojengwa katika ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bahi unaoendelea.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa