Na Benton Nollo,
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Rachel Chuwa ameuhakikishia Ubalozi wa Japan nchini Tanzania kutekeleza na kusimamia vema mradi wa usambazaji maji katika Shule ya Sekondari Kigwe uliofadhiliwa na ubalozi huo kwa shilingi 240 milioni (sawa na Dola za Kimarekani USD 110,746) kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Chuwa aliyasema hayo mara baada ya kusaini Mkataba wa Makubaliano kati yake na Balozi wa Japan nchini Tanzania, Masaharu Yoshida ubalozini Jijini Dar es Salaam tarehe 23 Machi 2018.
Ubalozi huo umetoa msaada wa fedha hizo baada ya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi kuandika andiko la mradi wa maji kwa ajili ya kutatua changamoto kubwa ya uhaba wa maji uliokuwa unaikabili shule hiyo kongwe ambayo pia ina Kidato cha Tano na Sita.
Awali akizungumza baada ya mkataba huo kusainiwa, Balozi Yoshida alieleza kufurahishwa kwake na jitihada zilizofanywa na Halmashauri hiyo za kuandika andiko la mradi husika na kufuatilia majibu ubalozini mara kwa mara, hali iliyosababisha msaada huo kutolewa.
Balozi Yoshida alieleza kuwa fedha hizo zitatumika kujenga tenki moja lenye ujazo wa lita elfu 45 kwa ajili ya kuhifadhia maji, vituo 5 vya kutekea maji, usambazaji wa maji kwenye nyumba 3 za walimu, maabara 3, mabweni 2 ya wanafunzi, ufungaji wa mitambo ya kusukuma maji kwa kutumia nguvu ya jua, usambazaji wa mabomba kutoka kisimani hadi kwenye tenki na ujenzi wa uzio kwenye eneo la nyumba ya mashine.
Akiongea kwa njia ya simu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kigwe, Mwasiti Msokola ameelezwa kufurahishwa na msaada huo kwani utakuwa mkombozi kwa walimu, wanafunzi na jamii inayozunguka shule hiyo pamoja na kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zikitumika kwa huduma ya maji shuleni hapo.
“Kwa kweli kwa niaba ya walimu na wanafunzi, ninayofuraha kubwa shule yetu kupatiwa msaada huo kwani tumekuwa tukitumia shilingi 400,000.00 kila mwezi kupata huduma ya maji hapa shuleni ambapo pamoja na kulipa fedha hizo katika Chombo cha Watumiaji Maji Kijiji cha Kigwe, maji hayo yalikuwa hayatoshelezi mahitaji ya walimu na wanafunzi hasa katika vyoo”. Alisema Msokola na kuongeza;
“Kwa shule yetu kupata msaada huo tutaweza kuboresha mandhari ya shule pamoja na kuanzisha miradi midogo midogo ya kilimo cha bustani za mboga mboga kupitia klabu za wanafunzi”.
Kwa upande wake Abraham Epimack Mlutee, Mwanafunzi wa Kidato cha Sita mchepuo wa HGK shuleni hapo, alieleza furaha yake kwamba huduma hiyo ikikamilika itawapunguzia adha ya kutumia muda mwingi kutafuta maji hali iliyokuwa ikiwasababishia kupoteza muda wa masomo.
“Kwa kweli nimefurahi sana tena sana kaka kwa sababu adha hii ni ya muda mrefu kwani tumekuwa tukitumia muda mwingi kutafuta huduma ya maji pindi yanapokatika na hata muda wa masomo kutupita”. Alisema Mlutee na kuongeza kwamba;
“Nakumbuka mwezi Machi, 2016 ulitokea mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu hapa shuleni na mwalimu mmoja na baadhi ya wanafunzi walikumbwa na ugonjwa huo ambapo kwa undani sababu kubwa ya kutokea mlipuko huo ni ukosefu wa maji safi na salama hapa shuleni. Hivyo, tunapopata taarifa za msaada huo tunafurahi na tunaamini mradi huo ukikamilika hata milipuko ya magonjwa kama kipindupindu hayatatokea”.
Shule ya Sekondari Kigwe ipo Kijiji cha Kigwe, Kata ya Kigwe na ni moja kati ya shule za sekondari 20 zilizopo Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma. Katika Wilaya ya Bahi shule hiyo ni kongwe kwani ilianzishwa tarehe 16 Mei 1992 na mwaka 2011 ilipewa hadhi ya kuwa na wanafunzi wa Kidato cha Tano.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa