Benton Nollo, Bahi
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amezindua rasmi ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bahi na kuuagiza uongozi wa Halmashauri pamoja na kamati zote zinazohusika na usimaminzi wa ujenzi wa mradi wa hospitali hiyo, kuhakikisha kuwa inakamilika ifikapo tarehe 30 Mei, 2019.
Munkunda alitoa agizo hilo tarehe 12 Januari 2019 wakati akizindua eneo linalotarajiwa kujengwa hospitali hiyo.
Alisema kutokana na maandalizi yote ya msingi ikiwemo ununuzi wa vifaa vya ujenzi (Bati,Nondo na Mchanga) kuwa yameshakamilika hakuna sababu inayoweza kukwamisha ujenzi huo.
‘’Naagiza, nataka mradi huu kwa sababu kila kitu kipo tarehe 30 mwezi wa tano mwaka huu tuwe tumekwisha kamilisha majengo yote saba kwanini nasema hivyo , nasema hivyo nikiamini kabisa nguvu ya wananchi tunayo, maamuzi ya viongozi tayari yamekwisha fanywa kuanzia ngazi ya Mhe. Rais sasa tunasubiri nini, na taratibu zote za kisheria ambazo tulipaswa kuzifuata zimekwisha kamilika’’. Alieleza Munkunda.
Pia, Munkunda alizitahadharisha Kamati hizo pamoja na Vijana wa Jeshi la Akiba (Mgambo) kutoa taarifa kwa mtu yeyote au kamati yoyote itakayobainika ikihujumu fedha za ujenzi wa mradi huo endapo atabainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Katika hatua nyingine, Munkunda aliwataka wananchi wa Wilaya ya Bahi kuwa na ushirikiano ili kuweza kuileta Bahi maendeleo kama ilivyo sera ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. John Pombe Magufuli.
‘’Niwaombe Ushirikiano huo mliouonyesha kwenye ujenzi wa Kituo chetu cha Afya na mpaka sasa tumeanza shughuli zote zinazofanyika kwenye kile kituo hasa upasuaji tuzifanye hapa kwenye hospitali yetu ya Wilaya’’. Alisema Munkunda.
Akizungumza awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri wa Wilaya ya Bahi, Leo Mavika alisema Wilaya ya Bahi ni miongoni mwa Wilaya 68 zilizobahati kupewa fedha na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
"Kwetu ni bahati si wilaya zote zimepata, tuwashukuru viongozi akiwemo Mhe. Rais na Serikali ya Awamu ya Tano kwa ujumla wake. Lakini, pia tumshukuru sana Mhe. Mbunge kwa juhudi zake kubwa za kuweza kufuatilia na kuipigania Wilaya ya Bahi kuweza kuipatia maendeleo". Alisema Mavika.
"Bahi tunayoizungumzia leo ina barabara za lami, ina Kituo cha Afya kinachofanya na upasuaji. Bahi tunayoizungumza leo sasa tunajenga Hospitali ya Wilaya kwangu mimi ambaye naikumbuka historia ya Bahi kwa miaka ya nyuma kwanza naona kama ni ndoto, pili naiona ni bahati na tatu naishia tu kumshukuru Mwenyezi Mungu, sasa nimeyasema haya ili kuwaomba Wananchi wa Bahi waweze kutoa ushirikiano wa dhati katika kuhakikisha hospitali hii inajengwa na inakamilika kwa wakati". Alisema Mavika.
Wilaya ya Bahi ni miongoni mwa Wilaya 68 nchini zilipokea fedha shilingi 1,500,000,000 (Bilioni moja na milioni mia tano) kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambayo kimsingi ikikamilika itapunguza adha ya wananchi wa Bahi kutumia gharama kubwa za matibabu Dodoma Mjini.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa