Na Benton Nollo, Halmashauri ya Wilaya ya Bahi
Mkuu wa Wilaya Bahi mkoani Dodoma, Mhe. Elizabeth S. Kitundu, amewataka viongozi kuihamasisha jamii kutumia nishati mbadala ili kulinda misitu na kuhifadhi mazingira.
Aidha, aliwataka wananchi kuepukana na matumizi ya mifuko ya plastiki ambayo inachafua mazingira kwa kiasi kikubwa.
Mhe. Elizabeth, aliyasema hayo katika maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kiwilaya yalifanyika katika Kijiji cha Mundemu Juni 05, 2018.
"Tatizo la uchafuzi wa mazingira bado ni kubwa hivyo, nawasihi sana wananchi kuzingatia kutotupa hovyo takataka za plastiki ili kulinda afya za wananchi na wanyama, lakini pia pale kunapokuwa na uharibifu wa mazingira sheria zitumike kwa wanaokiuka", alisema Elizabeth.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mhe. Elizabeth Kitundu (kushoto), akimsikiliza Salome Tarimo, alipotembelea shambani kwake kukagua miti mbalimbali ya matunda.
Kwa upande wake, Afisa Ardhi, Maliasili na Mazingira, Chediel Mrutu, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, alikumbusha athari zitokanazo na mifuko ya plastiki ikiwa ni pamoja na pale inapozama ardhini hukaa zaidi ya miaka 100 bila kuoza, hivyo husababisha kuchafuka kwa ardhi.
"Kutokana na hali hiyo, ni wakati muafaka sasa kwa wananchi wa Wilaya ya Bahi kutunza mazingira na kusema hapana kwa matumizi ya mifuko hii ili kuweza kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwenye mazingira tunayoishi hasa sehemu zote zile zinazokuwa kwa kasi kubwa,"alisema Mrutu.
Afisa Ardhi, Maliasili na Mazingira, Chediel Mrutu, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bahi katika maadhimisho hayo.
Aidha, aliwataka viongozi wilayani humo kumchukulia hatua mtu yoyote atakayekutwa akichoma au kuuza mkaa hovyo kwa kumtoza faini au kumfikisha mahakamani kulingana na mujibu wa Sheria ya Usimamizi waMazingira Namba 20 ya mwaka 2004 na sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002 kama zinavyoagiza.
Kauli mbiu ya Kimataifa ni "Pinga Uchafuzi wa Mazingira unaotokana na Plastiki" na Kauli mbiu ya Kitaifa katika maadhimisho hayo ni "Mkaa gharama, Tumia Nishati Mbadala".
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Mundemu wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya hiyo (hayupo pichani). Picha zote na Benton Nollo.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa