Benton Nollo na Bernard Magawa, Bahi
Mkuu wa Wilaya ya Bahi Mwanahamisi Munkunda amezindua zoezi la Chanjo ya UVIKO 19 wilayani humo na kutoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kuchanjwa ili kuwa salama dhidi ya maradhi hayo hatari.
Akizungumza kabla ya uzinduzi huo uliofanyika kiwilaya tarehe 5 Agosti 2021 katika Hospitali ya Wilaya ya Bahi na baadaye kuwa wa kwanza kupata chanjo hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya amewaasa wananchi kupuuza upotoshaji unaoendelea katika mitandao ya kijamii kuhusiana na chanjo ya UVIKO 19 kwani hauna ukweli wowote kwa sababu wote wanaopotosha siyo wataalamu wa afya, hivyo wafike kwa wingi katika vituo vilivyoainishwa na Serikali ili kuchanjwa.
“Niwaombe Viongozi wenzangu wa dini na Serikali, tuhamasishe wananchi na Waumini wetu wafike vituoni kwa wingi kupata chanjo.” Amesema Munkunda.
Awali, akitoa taarifa ya ugonjwa huo, Mganga Mkuu Wilaya ya Bahi Dkt. Phillipina Philipo amesema wilaya hiyo imepata wagonjwa watano wenye matatizo ya upumuaji ambapo baada ya vipimo wagonjwa watatu kati ya hao watano wamegundulika kuwa na ugonjwa wa UVIKO 19 huku majibu ya wagonjwa wawili yakiwa bado hayajarudi kutoka maabara.
“Katika kukabiliana na ugonjwa huu tumeandaa vifaa tiba na dawa katika vituo vyetu vyote vya kutolea huduma za afya ikiwemo mitungi ya gesi ili kurahisisha matibabu kwa wagonjwa watakao bainika na tatizo hilo. Pia, tunahimiza maeneo yote ya biashara, shule, taasisi mbalimbali na maeneo yote ya mikusanyiko kuwa na maji tiririka kwa ajili ya kunawa mikono pamoja na uvaaji wa barakoa ili kujikinga na janga hili.” Amesema Dkt. Philipina.
Hata hivyo, Dkt. Phillipina amewatoa hofu na kuwahakikishia wananchi wilayani Bahi kuwa chanjo hiyo ni salama kwa matumizi ya binadamu na imethibitishwa na taasisi za kitaifa na kimataifa zinazohusika na sekta ya afya.
Dkt. Phillipina amesema kwamba Wilaya ya Bahi imepokea chanjo Dozi 3,000 ambapo mpaka sasa tayari watu 36 wameshachanjwa na amevitaja vituo vya kutolea chanjo hiyo wilayani Bahi kuwa ni Hospitali ya Wilaya, Kituo cha Afya Mundemu na Kituo cha Afya Chipanga.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa dini walioshiriki uzinduzi huo, Ramadhani Issah ameipongeza na kuishukuru Serikali kwa kuwajali wananchi wake na kuwaletea chanjo hiyo ambayo itawakinga na kuwalinda dhidi ya UVIKO 19 na amewasihi viongozi wenzake wa dini kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo ambao umeitikisa dunia na kugharimu maisha ya watu.
Naye, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Bahi, Sterwat Masima akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa ujasiri na uthubutu katika kuhakikisha inaokoa Wananchi wake katika janga hilo kwa kuwaletea chanjo na kuahidi kuhamasisha wanachama wote wa chama chake kupata chanjo ili wawe salama.
Matukio katika Picha:
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (aliyevaa kilemba chekundu) pamoja na viongozi mbalimbali wilayani humo wakichomwa Chanjo ya UVIKO 19 katika hafla ya uzinduzi wa chanjo hiyo iliyofanyika Hospitali ya Wilaya ya Bahi tarehe 05 Agosti 2021.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (kulia) akizundua rasmi zoezi la Chanjo ya UVIKO 19 kwa hiari katika hafla ya uzinduzi wa chanjo hiyo iliyofanyika Hospitali ya Wilaya ya Bahi tarehe 05 Agosti 2021.
Viongozi na watumishi mbalimbali wilayani Bahi wakifuatilia matukio wakati wa zoezi la uzinduzi wa Chanjo ya UVIKO 19 katika hafla ya uzinduzi wa chanjo hiyo iliyofanyika Hospitali ya Wilaya ya Bahi tarehe 05 Agosti 2021. (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa