Na Benton Nollo, Bahi
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge amewaruhusu wakulima wa zao la Ufuta mkoani humo ambao bado wana ufuta nyumbani, kuuza mahali popote ambapo wanaona watapata bei ya kuwafaa.
Dkt. Mahenge ametoa maelekezo hayo ya Serikali akiwa wilayani Bahi ambapo aliwatembelea Wakulima na Wafanyabiashara wadogo wa zao hilo baada ya wakulima hao kuiomba Serikali kuingilia kati bei ya zao hilo kufuatia kuporomoka kwa bei katika mnada ulioendeshwa tarehe 24 Juni 2020 kutoka bei ya shilingi 1,931 mnada wa tarehe 02 Juni 2020 hadi shilingi 1,250.
“Maelekezo yangu baada ya kukaa kikao juzi Jumapili na Wafanyabiashara na Wakuu wa Wilaya wote ni kwamba kuanzia sasa, mwananchi yeyote ambaye bado ana ufuta nyumbani aende akauze anakoona yeye inafaa, hakutakuwa tena na hii zuia zuia isipokuwa tu utatulipia ushuru wetu kwenye geti, mmenielewa ndugu zangu”. Amesema Dkt. Mahenge na kuongeza kuwa;
“Waambieni na wananchi wote kwamba muda uliobaki Serikali imeamua kuwaachia wananchi wafanye juhudi zake, kama unamuuzia mfanyabiashara muuzie kama unapeleka mwenyewe mjini peleka, lakini kama ipo chini ya tani moja unapeleka bila malipo ikizidi tani moja unalipa ushuru”.
Dkt. Mahenge amewaeleza wakulima hao kuwa zipo sababu tatu ambazo kimsingi ndizo zilizosababisha kushuka kwa kasi kwa bei ya zao ufuta katika mkoa wa huo kuwa ni athari za Ugonjwa wa Corona ambapo wanunuzi wakubwa duniani bado nchi zao hazijafungua mipaka yao hivyo imekuwa vigumu kupeleka ufuta katika nchi hizo.
Sababu ya pili, Dkt. Mahenge ameitaja kuwa Mkoa wa Dodoma huwa wa kwanza kuanza kuvuna ufuta lakini kutokana na mvua nyingi zilizonyesha mwaka huu (2020) mavuno yalichelewa kuanza na wakulima wakajikuta wanaanza kuvuna mwezi Mei na Juni ilhali mikoa ya kusini nayo ndiyo msimu wa kuvuna zao hilo na hata katika nchi za Malawi na Ivori Coast nazo ndiyo msimu wa mavuno hivyo, kufanywa ufuta kuwa mwingi sokoni.
Dkt. Mahenge ameainisha sababu ya tatu ya kushuka kwa bei ya zao hilo kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2020 uzalishaji wa ufuta ulikuwa mkubwa kwani wakulima wamevuna vizuri kwa kuwa mvua zimenyesha vizuri na za kutosha.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amemueleza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuwa katika mnada uliofanyika tarehe 24 Juni 2020 kwa dakika 15 wilaya hiyo ilikuwa na tani 78.2 ambapo bei ya mnunuzi aliyejitokeza alinunua kwa shilingi 1,250 kwa kilo moja jambo ambalo halikuwaridhisha wakulima na kuamua kutouza shehena hiyo.
“Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kwa kuona kuwa tumeshafanya minada miwili na huu wa leo ni wa tatu na bei haituridhishi kwa sababu tulianza na bei ya 1,820 tulikataa, tukaja 1, 520 nayo tulikataa na hii ya leo ya shilingi 1,250 imekuwa mbaya zaidi…hivyo, kama kiongozi baada ya kuona hali inakuwa mbaya nikaamua kuchukua hatua kwa kushirikiana na wakulima kutafuta mnunuzi nje ya mnada na ambapo tumempata na atachukua mzigo huo kwa shilingi 1,400 na wakulima wameridhia”. Amesema Munkunda.
Naye Tito Chifungo, ambaye ni mkazi na mkulima wa ufuta katika Kijiji cha Mundemu ameishukuru Serikali na kuridhika na jitihada ilizochukua katika kushughulikia suala hilo hali ambapo kwa niaba ya wakulima wenzie wameridhishwa na uamuzi wa Serikali kuwaruhusu kuuza zao hilo mahali popote wanapopataka.
Zao la Ufuta katika Mkoa wa Dodoma ni kwa mara ya kwanza katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020 liliingia katika Mfumo wa Stakabadhi Ghalani.
Pichani ni Zao la Ufuta unaolimwa wilayani Bahi.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge (wa kwanza kushoto) akizungumza na wakulima wa Ufuta katika Ghala la Bahi ambalo limekuwa likitumika katika uuzaji wa zao hilo kwa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani alipotembelea na kuzungumza nao tarehe 24 Juni 2020. Dkt. Mahenge amewaruhusu wakulima wa zao hilo mkoani humo ambao bado wana ufuta nyumbani, kuuza mahali popote ambapo wanaona watapata bei ya kuwafaa kutoka na kushuka kwa bei ya zao hilo na kuwaathiri wakulima.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda katikati) akimueleza Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge (wa kwanza kushoto) hali halisi juu ya mwenendo wa uuzaji wa zao la ufuta kwa Mfumo wa Stakabadhi Ghalani wilayani humo pamoja na changamoto zake. Dkt. Mahenge amewaruhusu wakulima wa zao hilo mkoani humo ambao bado wana ufuta nyumbani, kuuza mahali popote ambapo wanaona watapata bei ya kuwafaa kutoka na kushuka kwa bei ya zao hilo na kuwaathiri wakulima. (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa