Benton Nollo, Bahi
Watendaji wa Kata 22 na Watendaji wa Vijiji 59 wilayani Bahi wametakiwa kutotanguliza mbele changamoto, katika suala la ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri.
Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dkt. Fatuma Mganga wakati akifungua kikao kazi cha siku moja kilichowahusisha Watendaji hao na Wakuu wa Idara kwa lengo la kufanya tathmini ya makusanyo kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2019/2020 (Julai hadi Septemba, 2019).
Dkt. Mganga ameyasema hayo baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa ukusanyaji wa mapato kwani kwa kipindi hicho kila Mtendaji wa Kijiji alipaswa kuwa amefikia asilimia 25 au zaidi katika malengo ya makusanyo ya Kijiji husika kwa mwaka huo lakini ni vijiji 12 tu kati ya vijiji 59 ndivyo vimekusanya mapato yake kwa zaidi ya asilimia 25.
Dkt. Mganga alivitaja vijiji vilivyofanya vizuri kuwa ni Mapinduzi (62%), Chikola (34%), Chali Igongo (33%), Ibugule (33%), Chali Makulu (32), Nguji (31%), Kisima cha Ndege (29%) na Mindola (27%). Vijiji vingine ni Chimendeli (26%), Mpalanga (25%), Zejele (25%) na Bahi Makulu (25%).
Pia, Dkt. Mganga hakusita kuvitaja vijiji vilivyofanya vibaya katika ukusanyaji wa mapato kwa kipindi hicho kuwa ni Kigwe, Lukali, Nholi, Chidilo, Mphangwe, Mpamantwa, Ikumbulu na Babayu ambapo vyote kwa kila kimoja makusanyo yake ni chini ya asilimia 10.
"Afisa Utumishi nikuagiza Watendaji wa Vijiji 12 vilivyofanya vizuri wapatiwe barua za pongezi, Watendaji wa Vijiji ambao wamekusanya kwa asilimia 15 hadi 24 waelekezwe kwa barua kuongeza bidii katika ukusanyaji wa mapato na wenye asilimia 0 hadi 14 waandikie barua za kujieleza kwa nini wamekusanya chini ya kiwango ilhali malengo ya makusanyo yaliwekwa kwa kuwashirikisha na yaliafikiwa kwa pamoja kupitia vikao vyetu". Anaagiza Dkt. Mganga na kusisitiza kuwa barua hizo pia ziandikwe kwa mfumo huo huo kwa Watendaji wa Kata.
Aidha, Dkt. Mganga amewatahadharisha watumishi wanaojaribu kuhujumu mifumo mbalimbali iliyowekwa na Serikali kwa ajili ya kukusanya mapato kuwa hatasita kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.
Tathmini ya ukusanyaji wa mapato yanayotokana na Vibali vya Mifugo na Mapato Mengineyo hufanyika kila robo mwaka kwa lengo la kujipima kufikia malengo ya mwaka mzima.
Picha na Matukio
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa