Rais mteule wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ally Hassan Mwinyi ameapishwa rasmi kuwa Rais wa Zanzibar ambaye pia atakuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa Awamu ya Nane.
Dkt. Mwinyi amekula kiapo katika Uwanja wa Amani mjini Unguja, mahali ambapo zimefanyika sherehe za kuapishwa kwake tarehe 02 Novemba 2020.
“Mimi Hussein Ali Mwinyi, naapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kwamba nitakuwa mwaminifu kwa Zanzibar na kuitumikia kwa moyo wangu wote na kwamba, nitaihifadhi, nitailinda, nitaitii na kuitetea Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na watu wake kwa mujibu wa sheria iliyowekwa”. Ndivyo Dkt. Mwinyi alivyoapa.
Baada ya kiapo Rais Mwinyi aliahidi kuwa na utendaji kazi wenye viwango bora na kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha huduma za kijamii kwa kuzitumia vyema rasilimali za Zanzibar kwa manufaa ya wananchi wote.
Akitoa ahadi ya kushirikiana na vyama vya upinzani Dkt. Mwinyi alisema; "Ndugu zangu ninawapongeza wagombea wenzangu kwa nafasi ya urais ambao wameyakubali matokeo ya uchaguzi na kuheshimu maamuzi ya wananchi na ninatoa ahadi ya kuwa nitashirikiana nao katika Serikali nitakayoiunda katika kuwatumikia wananchi na kuijenga Zanzibar".
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi alipata wasaa wa kusalimiana na viongozi mbalimbali waliokaa kwenye jukwaa kuu wakiwamo marais wastaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Dkt. Ali Mohamed Shein pamoja na marais wastaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi (ambaye ni baba yake mzazi) na Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dkt. Mwinyi anaanza uongozi wake wa miaka mitano baada ya kuchaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba 27 na 28, 2020 akimrithi mtangulizi wake Dkt. Ali Mohamed Shein ambaye amemaliza muda wake.
Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Hassan Mwinyi (kulia) akisalimiana na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ally Hassan Mwinyi (ambaye pia ni baba yake mzazi) mara baada ya kuapishwa rasmi kuwa Rais wa Zanzibar wa Awamu ya Nane.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa