Na Benton Nollo,
Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango (FUM) leo wameanza ziara ya siku tatu ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo pamoja na mambo mengine pichani ni baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo wakikagua ujenzi wa Bwawa lililojengwa kwa Programu ya Kutoa Ajira ya Muda (PWP - Public Works Programme) katika Kijiji cha Ibihwa, Kitongoji cha Mapinduzi ambao kimsingi uliibuliwa na Wananchi kupitia Mkutano Mkuu wa Kijiji.
Akieleza katika ziara hiyo Mratibu wa TASAF Wilaya ya Bahi, Joseph Kileo alisema kuwa mradi huo uliibuliwa kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya uhaba wa maji kwenye Kijiji hicho hasa wakati wa kiangazi.
Kileo aliwaeleza wajumbe kuwa ukubwa wa bwawa hilo ni mita za mraba 5,600 (5,600M3) ambapo urefu ni mita 70, upana ni mita 40 na kina ni mita 2 na ujazo wa maji ni lita 5,600,000. Aliongeza kuwa mradi huo ulitekelezwa na Walengwa 357 kwa kutumia mikono kwa gharama ya shilingi 47,925,600.00 ikiwa vifaa ni shilingi 410,000.00 na ujira wa Walengwa shilingi 47,515,600.00 kwa muda wa siku 60 (Miezi Minne ambapo kila mwezi siku 15 zilitumika kufanya kazi). Hivyo, mradi ulianza tarehe 12 Septemba, 2017 na kukamilika tarehe 15 Desemba, 2017.
Akizungumza na Mwandishi wetu Mwenyekiti wa Kijiji cha Ibihwa, Abubakar Omari aliishukuru Serikali kupitia TASAF Awamu ya Tatu kwa kuleta fedha kwa Walengwa hao na hatimae jitihada hizo zimewezesha ujenzi wa bwawa hilo ambalo alisema limejaa maji ya kutosha ambayo yatatumiwa na wananchi kwa shughuli mbalimbali wakati wa kiangazi ambapo maji yanakuwa ya shida katika eneo hilo.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa