Kesho tarehe 05 Novemba 2020 wakazi wa Mkoa wa Dodoma watashuhudia historia mpya ikiandikwa ambapo kwa mara ya kwanza tangu Tanzania ipate uhuru mwaka 1961, sherehe za kuapishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zitafanyika mkoani humo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge amesema maandalizi ya sherehe hizo ambazo wakazi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla watashuhudia kuapishwa kwa Rais Mteule Dkt. John Pombe Magufuli katika uwanja wa Jamhuri yamekamilika.
Dkt. Mahenge amesema kuwa ni heshima kubwa kwa Mkoa wa Dodoma kupata fursa ya kushuhudia tukio hilo la kistoria ambalo hufanyika mara moja ndani ya miaka mitano na anaamini kuwa tukio hilo linatoa fursa kwa wafanya biashara kujipatia kipato ambapo uchumi ndani ya Mkoa wa Dodoma utainuka.
“Haya ni matunda makubwa ya uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli wa kuhamishia Makao Makuu ya Serikali mkoani Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa ndoto ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyoanza kuitekeleza mwaka 1973”. Amesema Dkt. Mahenge.
Amesema kuwa matukio makubwa kama haya yatakuwa yakifanyika mkoani Dodoma na kutoa fursa na hamasa kwa wawekezaji kama vile wa huduma za usafiri, hoteli, nyumba za kulala wageni, kumbi za burudani, mama lishe, machinga na wengine wengi kuwekeza zaidi Dodoma.
Hata hivyo, Dkt. Mahenge ametoa rai kwa wananchi wa Dodoma kutokua sehemu ya bugudha na usumbufu kwa wageni wanaokuja licha ya kuwa Dodoma ni sehemu yenye amani wakati wote hivyo amewataka kuimarisha na kudumisha sifa hiyo ikiwa ni pamoja na kuboresha viwango vya huduma na biashara zao.
“Sherehe hizi zitahudhuriwa na Marais na viongozi wa juu kutoka mataifa mbalimbali, viongozi wastaafu na wafanyabiashara wakubwa hivyo, tukiboresha huduma katika biashara zetu tutawavutia kurudi tena hata baada ya zoezi hili kuisha kwa ajili ya kutembea na kufanya uwekezaji mbalimbali”. Ameongeza Dkt. Mahenge.
Aidha, Dkt. Mahenge amesema kuwa sherehe hizo zitapambwa kwa burudani mbalimbali ikiwa ni pamoja na gwaride maalum lililoandaliwa na vikosi mbalimbali vya ulinzi vya Tanzania, vikundi vya ngoma, pamoja na wasanii wa kizazi kipya kama vile Harmonize, Zuchu, Nandy, Sholo Mwamba na Dulla Makabila.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amewakaribisha na kuwahimiza wananchi wote kuwahi kufika uwanjani mapema ili kuepuka usumbufu na kuongeza kuwa milango itakua wazi kuanzia saa 12 alfajiri.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa