Na Benton Nollo na Bernard Magawa (DMC), Bahi
Wito umetolewa kwa Wananchi wa Wilaya ya Bahi kuhakikisha wanaitumia vema ofisi ya Dawati la Jinsia na Watoto ili kupunguza ukatili kwa wanawake na watoto.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda wakati wa uzinduzi wa kituo kipya cha Dawati la Jansia na Watoto kilichojengwa kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake (UN WOMEN) katika ofisi ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi tarehe 17 Desemba 2020.
Munkunda amelipongeza Jeshi la Polisi wilayani humo kwa utendaji mzuri hususan katika kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na makosa ya kijinsia yanayolipotiwa ambapo takwimu zinaonesha kwa mwaka 2019/2020 zaidi ya kesi 60 zilisikilizwa na kupatiwa hukumu.
“Ukatili wa kijinsia una athari kubwa sana katika ukuaji wa uchumi, mtu aliyeathirika kijinsia hawezi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi kwani anakosa kujiamini.” Amesema Munkunda na kuongeza;
“Niwaombe maofisa mtakaofanya kazi katika dawati hili msikae ofisini kusubiri kesi, zifuateni mitaani kwa maana watanzania tulivyolelewa siyo watu wa kesi kesi. Hivyo, andaeni vipindi mbalimbali vya kuelimisha katika shule na maeneo mengine ili waweze kuipata elimu hii.”
Awali akizungumza kabla ya uzinduzi wa jengo hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Bahi, Mrakibu wa Polisi Idd Ibrahimu amesema tayari watumishi sita wameshapatiwa mafunzo kwa ajili ya uendeshaji wa ofisi hiyo.
Naye, Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto Tanzania, Naibu Kamishana wa Polisi Mary Nzuki amesema tangu dawati hilo lianzishwe hapa nchini mwaka 2008 tayari madawati 400 yameshaanzishwa nchini ambapo ameiomba jamii kushirikiana na serikali kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la UN WOMEN, Hodan Addouh amesema wao kama wadau wa maendeleo wanatambua kwa dhati thamani ya ushirikiano wanaoupata kutoka kwa Jeshi la Polisi na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika kutekeleza Mpango wa Taifa wa kupambana na ukiukwaji wa haki za wanawake na watoto.
Aidha, pamoja na kufadhili ujenzi wa jingo hilo, Shirika la UN WOMEN pia limetoa samani zenye thamani ya shilingi milioni 10.7.
Matukio katika picha wakati wa uzinduzi wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Bahi.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda akizungumza katika hafra ya uzinduzi wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Bahi.
Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto Tanzania, Naibu Kamishana wa Polisi Mary Nzuki akizungumza katika hafra ya uzinduzi wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Bahi.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Bahi, Mrakibu wa Polisi Idd Ibrahimu akizungumza katika hafra ya uzinduzi wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Bahi.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa