Na Benton Nollo, Bahi
Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeitaka jamii kushirikiana na Serikali katika kuwabaini na kuwatambua Wananchi wenye uhitaji ili kuondoa udanganyifu katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF III) Awamu ya Pili unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Wito huo umetolewa Julai 29, 2020 na Mtaalam wa Utafiti na Maendeleo wa TASAF, Tumpe Lukongo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari mara baada ya kutoa mafunzo kwa Wakuu wa Idara na Wawezeshaji wa Ngazi ya Halmashauri, Wilaya ya Bahi kuhusiana na zoezi la uhakiki wa Walengwa wa kaya maskini.
Lukongo amesema TASAF III Awamu ya Kwanza imeisha na sasa wapo katika utekelezaji wa TASAF III Awamu ya Pili ambapo kwa sasa wanafanya uhakiki wa wanufaika ili kupata masijala safi ya walengwa kabla ya kuanza utekelezaji wa mpango huo.
“Rais Dkt. John Magufuli wakati anazindua TASAF III Awamu ya Pili alituelekeza kwamba kabla hatujaanza utekelezaji tufanye, uhakiki na kusafisha Daftari la Kaya Maskini ili tuwapate walengwa wanaostahili na tulishaanza kutekeleza maelekezo hayo nchi nzima na sasa tunamalizia Mkoa wa Dodoma, Singida, Kigoma, Lindi na Mtwara". Alisema Lukongo.
Amesema ili zoezi hilo lifanikiwe kwa ufanisi ni muhimu Wananchi washirikiane na Serikali katika ngazi zote, kinyume na hapo jitihada za serikali za kuondoa umaskini zinaweza zisifike kwa walengwa.
“Jamii ndio inamjua mtu maskini, inamjua mtu anayehitaji msaada zaidi ya wengine, hivyo ikishirikiana na serikali kwa ukweli na uwazi itasaidia kuondoa changamoto ya udanganyifu ambayo imekuwepo katika baadhi ya maeneo.” Aliongeza Lukongo.
Amesema lengo la uhakiki huo ni kuwa na orodha halisi ya walengwa kwenye masijala ya kaya za walengwa kwa kuondoa waliofariki, aliyehama, kiongozi wa kijiji, kaya ya mjumbe wa kamati ya usimamizi wa jamii na kaya ambayo haikufika kuchukua malipo yake mara mbili mfululizo.
Ili kuondoa changamoto ya udanganyifu amesema wameboresha dodoso la utambuzi na namna ya udodosaji ambapo mwanzo walikuwa wanatumia wahusika ngazi ya jamii lakini kwa sasa wanatumia wawezeshaji ngazi ya Halmashauri ambao wanapewa mafunzo ya kutumia vishkwambi kuingiza taarifa badala ya makaratasi.
Ametaja mafanikio yaliyofikiwa katika utekelezaji wa TASAF III Awamu ya Kwanza, kuwa ni pamoja na maisha ya walengwa kuboreka, walengwa wengi kujishughulisha na shughuli za kuongeza kipato, kupata uwezo wa kusomesha watoto wao, kuboresha afya na lishe.
Kiongozi wa Timu ya Uhakiki ya TASAF, Abasi Salehe akizungumza wakati wa Mafunzo ya kujenga uwezo kuhusu kipindi cha pili cha TASAF III na uhakiki wa Kaya kwa Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Wawezeshaji Ngazi ya Halmashauri tarehe 29 Julai 2020.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Denis Komba akisisitiza jambo wakati wa Mafunzo ya kujenga uwezo kuhusu kipindi cha pili cha TASAF III na uhakiki wa Kaya kwa Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Wawezeshaji Ngazi ya Halmashauri tarehe 29 Julai 2020.
Mratibu wa TASAF Wilaya ya Bahi, Joseph Kileo akizungumza wakati wa Mafunzo ya kujenga uwezo kuhusu kipindi cha pili cha TASAF III na uhakiki wa Kaya kwa Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Wawezeshaji Ngazi ya Halmashauri tarehe 29 Julai 2020.
Afisa Ufuatiliaji wa TASAF Wilaya ya Bahi, Amani Christian akizungumza wakati wa Mafunzo ya kujenga uwezo kuhusu kipindi cha pili cha TASAF III na uhakiki wa Kaya kwa Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Wawezeshaji Ngazi ya Halmashauri tarehe 29 Julai 2020.
Baadhi ya Washiriki wakifuatilia kwa makini Mafunzo ya kujengewa uwezo kuhusu kipindi cha pili cha TASAF III na uhakiki wa Kaya yaliyofanyika kwa Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Wawezeshaji Ngazi ya Halmashauri tarehe 29 Julai 2020 kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi.
Mwezeshaji wa Mafunzo kutoka TASAF, Grace Kibonde akitoa maelezo kuhusu Kipindi cha Pili cha Mpango wa TASAF III kwa Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na Wawezeshaji Ngazi ya Halmashauri tarehe 29 Julai 2020 kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi.
Mwezeshaji wa Mafunzo kutoka TASAF, Grace Kibonde (wa kwanza kushoto) akiwaelekeza washiriki wa Mafunzo namna ya kutumia Vishkwambi kwa ajili ya zoezi la uhakiki wa Walengwa wa Kaya Maskini katika Halmashaurinya Wilaya ya Bahi tarehe 29 Julai 2020. (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa