Na Benton Nollo na Bernard Magawa DMC, Mundemu
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda ameiagiza Kamati ya Ujenzi ya Shule ya Sekondari Mundemu kukamilisha haraka ujenzi wa majengo inayoyasimamia kabla ya mwezi Januari 2021 ili yaweze kutumiwa na wanafunzi wa Kidato cha Kwanza 2021.
Munkunda ameyasema hayo tarehe 01 Desemba 2020 alipotembelea shuleni hapo kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa mawili, bweni moja na choo chenye matundu 8 ambapo Serikali kupitia programu ya Lipa Kulingana na Matokeo – EP4R imetoa shilingi milioni 128.6 kujenga majengo hayo.
“Mmepata bahati ya kupokea fedha za ujenzi shuleni kwenu, hakikisheni mnakamilisha mapema ili watoto wa Kidato cha Kwanza watakapochaguliwa kujiunga na masomo shuleni hapa wakute majengo haya yapo tayari kwa matumizi.” Amesema Munkunda.
Munkunda baada ya kukagua majengo hayo ameipongeza kamati hiyo kwa usimamizi mzuri unaozingatia viwango vya ujenzi wa majengo ya serikali na thamani ya fedha inaonekana.
Aidha, Munkunda ameiagiza kamati hiyo kuhakikisha kuwa inaongeza kasi ya ujenzi kwa kuwasimamia mafundi kwa karibu na kwamba ifikapo tarehe 20 Desemba 2020 majengo yote yawe yamekamilika ili watoto watakao chaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza 2021 shuleni hapo waweze kuyatumia.
Awali akisoma taarifa za maendeleo ya ujenzi wa majengo hayo Mkuu wa Shule hiyo, Reubeni Nchimbwi amesema mwezi Juni 2020 shule yake ilipokea fedha hiyo lakini utekelezaji ulichelewa kuanza kutokana na kufungwa kwa mifumo ya Serikali baada ya mwaka wa fedha 2019/2020 kuisha.
Naye, Diwani Mteule wa kata hiyo, Msafiri Mtati amesema kata yake imejipanga kuhakikisha majengo hayo yanakamilika kwa wakati na wameandaa mkakati maalum wa usimamizi.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (aliyevaa kilemba) akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ujenzi ya Shule ya Sekondari Mundemu (hawapo pichani) katika ziara yake aliyoifanya tarehe 01 Desemba 2020.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (aliyevaa kilemba) akikagua ujenzi wa miundombinu unaoendelea Shule ya Sekondari Mundemu katika ziara yake aliyoifanya tarehe 01 Desemba 2020.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Mundemu, Reuben Nchimbwi akisoma taarifa ya ujenzi wa bweni moja, madarasa mawili na choo chenye matundu 8 unaoendelea shuleni hapo katika ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Bahi (hayupo pichani) aliyoifanya tarehe 01 Desemba 2020.
Diwani Mteule wa Kata ya Mundemu, Msafiri Mtati akiishukuru Serikali kwa kutoa shilingi milioni 128.6 kwa ajili ya ujenzi wa bweni moja, madarasa mawili na choo chenye matundu 8 katika Shule ya Sekondari Mundemu jambo ambalo litawasaidia wanafunzi wa Kidato cha Kwanza mwaka 2021. Mtati ametoa shukrani hizo katika ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Bahi (hayupo pichani) aliyoifanya tarehe 01 Desemba 2020. (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa