Benton Nollo na Bernard Magawa
Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru 2021, Luteni Josephine Mwambashi ameipongeza Kamati ya Ujenzi ya Shule ya Sekondari Bahi kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa pamoja na miundombinu ya TEHAMA ambapo thamani ya fedha imeonekana.
Luteni Mwambashi ameyasema hayo tarehe 25 Julai 2021 ambapo Mwenge wa Uhuru ulifika shuleni hapo kwa ajili ya uzinduzi wa jengo hilo ambalo limejengwa kwa fedha za Serikali kupitia Programu ya Lipa Kulinga na Matokeo EP4R Awamu ya Tisa 2021.
Akizungumza baada ya kukagua jengo hilo pamoja na miundombinu ya TEHAMA, ameipongeza Kamati ya Ujenzi hasa kwa kujiongeza na kujenga ofisi ya walimu katikati licha ya kwamba ramani ya wizara haikuwa na ofisi ya walimu hivyo, kwa kufanya hivyo wametatua changamoto ya uhaba wa ofisi kwa walimu shuleni hapo na ameagiza madarasa hayo yatunzwe ili yaweze kuwanufaisha wanafunzi katika kujifunza.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amemshukuru Kiongozi wa Mbio Maalumu za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2021 kwa kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo na kuuzindua rasmi.
“Mradi huu utakuwa chachu kwa Wanafunzi wetu kujifunza TEHAMA kwa vitendo wawapo shuleni hapa, nikuhakikishie Ndugu Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kuwa majengo haya pamoja na miundombinu yake vitatunzwa vizuri na ninafurahi kukutaarifu kuwa katika Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu wa 2021 wanafunzi wetu watafanya kwa vitendo mtihani wa taifa wa somo la TEHAMA kwanza mara ya kwanza.” Amesema Munkunda.
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Kiongozi wa Mbio Maalumu za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2021, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bahi, Eliakimu Solomoni amesema mradi huo umegharimu shillingi milioni 58 hadi kukamilika kwake ambapo kati ya hizo shilingi milioni 40 zimetolewa na Serikali na shilingi milioni 18 zimetolewa na wahisani pamoja na nguvu ya wananchi.
“Ndugu kiongozi wa Mbio Maalumu za Mwenge wa Uhuru kitaifa, lengo la mradi huu ni kuwawezesha wanafunzi kupata stadi na ujuzi wa kutumia mfumo wa Teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji wa masomo hasa kufanya majaribio kwa vitendo.” Amesema Solomoni.
Wilaya ya Bahi imekuwa ya kwanza katika Mkoa wa Dodoma kuanza kukimbisa Mwenge wa Uhuru 2021 ukitokea Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
Matukio Katika Picha:
Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2021, Luteni Josephine Mwambashi akizungumza kabla ya kuzindua jengo la madarasa mawili, ofisi ya walimu na miundombinu ya TEHAMA katika Shule ya Sekondari Bahi tarehe 25 Julai 2021.
Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2021, Luteni Josephine Mwambashi (kushoto) akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (kulia) aliyekuwa akimshukuru kiongozi huyo baada ya kuzindua jengo la madarasa mawili, ofisi ya walimu na miundombinu ya TEHAMA katika Shule ya Sekondari Bahi tarehe 25 Julai 2021.
Muonekano wa jengo la madarasa mawili na ofisi ya walimu lililozinduliwa na Kiongozi wa Mbio Maalum za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2021 tarehe 25 Julai 2021 ambalo ujenzi wake umegharimu shilingi milioni 58 ambapo kati ya hizo shilingi milioni 40 zimetolewa na Serikali kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo - EP4R Awamu ya Tisa 2021 na shilingi milioni 18 zimechangiwa na Wahisani na Nguvu za Wananchi.
Mwenge wa Uhuru 2021 ukiwasili Shule ya Sekondari Bahi tarehe 25 Julai 2021.
Wakimbiza Mwenge Maalum wa Uhuru Kitaifa 2021 wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya Mwenge huo kukabidhiwa wilayani Bahi katika Kijiji cha Uhelela tarehe 25 Julai 2021. Kutoka kushoto ni Luteni Ramadhani Ally Msham, Koplo Rehema Ali Haji, Private Dismas Egno Mvula, Luteni Mussa Hassan Mussa na Luteni Geofrey Jume Aron.
Picha za juu ni mapokezi ya Mwenge wa Uhuru 2021 Kijiji cha Uhelela tarehe 25 Julai 2021. (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa