Na Benton Nollo na Bernard Magawa (DMC), Bahi
Wananchi wilayani Bahi mkoani Dodoma wamehimizwa kujitolea nguvu kazi katika miradi mbalimbali ya maendeleo inayopelekwa na Serikali ili kuifanya ikamilike kwa wakati badala ya kuiachia serikali ifanye kila kitu wakati wanufaika wakuu wa miradi hiyo ni wananchi wenyewe.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Donald Mejiti katika ziara ya Ukaguzi wa Miradi iliyoifanywa kwa siku mbili (tarehe 18 na 19 Januari 2021) na wajumbe wa Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango (FUM).
“Kuanzia leo tukiletewa mradi wowote na Serikali, lazima wananchi washiriki katika kazi mbalimbali kama vile kuchimba msingi, kumwaga zege, kusogeza udongo, mchanga, matofali na kazi zote za mikono, hatuwezi kuiachia serikali ifanye kila kitu wakati wanufaika wakuu wa miradi hii ni sisi wananchi wenyewe.” Amesema Mejiti na kuongeza:
“Hiki ni kipindi cha kufanya kazi, viongozi na watendaji tusimamie maendeleo kikamilifu na kuhakikisha wananchi wetu wanashirikI kwa wingi katika kutekeleza miradi kwa kujitolea nguvu kazi.
Miradi iliyokaguliwa na Kamati hiyo ni ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa Shule Shikizi ya Lioni, vyumba viwili vya madarasa Shule Shikizi ya Suguta, Shule Shikizi ya Mzogole na Shule Shikizi ya Sanza iliyopo Kijiji cha Mpalanga.
Miradi mingine ni ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, bweni la wavulana na choo chenye matundu 8 Shule ya Sekondari Mundemu, ujenzi wa Zahanati ya Chidilo, na ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, bweni la wavulana na choo chenye matundu 8 Shule ya Sekondari Nondwa na ujenzi wa njia za kutembelea Kituo cha Afya Mundemu zinazojengwa kwa ufadhili wa Shirika la World Vision Tanzania.
Awali, akitoa taarifa ya ujenzi katika kijiji cha Mpalanga kwa Madiwani, Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Maria Dominick amesema ushiriki wa jamii katika miradi hiyo ni mdogo na kuomba uongozi wa juu kuwasaidia kuelimisha wananchi ili washiriki kikamilifu katika miradi hiyo kupitia nguvu kazi ili waweze kuokoa fedha ambazo zinaweza kufanya kazi nyingine za maendeleo.
Akizungumza katika ziara hiyo, mjumbe wa kamati hiyo Arois Sokozi amewahimiza viongozi katika ngazi za vijiji na kata kushikamana na kushirikiana kwa pamoja katika kusimamia miradi hiyo ili kuwa na ufanisi zaidi.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa