Na Benton Nollo na Bernard Magawa (DMC), Bahi
Halmashauri ya Wilaya ya Bahi imetoa mikopo kwa vikundi 25 vya wajasiriamali wadogo wadogo yenye thamani ya shilingi milioni 83.1 ambayo ni asilimia 10 ya makusanyo yake ya ndani kwa mujibu wa sheria.
Mikopo hiyo yenye lengo la kuwasaidia wajasiriamali kukuza mitaji na kuongeza vipato vyao ili waweze kujikwamu na umaskini, imetolewa Makao Makuu ya Halmashauri hiyo tarehe 20 Januari 2021.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mikopo hiyo mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda ameishauri kwamba pamoja na kuwakopesha fedha hizo pia, Halmashauri itoe kipaumbele kwa wajasiriamali hao katika shughuli mbalimbali zinazotokea kama vile huduma za chakula katika mikutano na matukio mbalimbali badala ya kuwapa kazi hizo watu kutoka maeneo mengine ili kuwajengea uwezo wa kurejesha kwa wakati mikopo hiyo.
“Serikali ya awamu ya tano imejipanga kuwasaidia wanyonge mkiwemo ninyi wajasiriamali, tunatamani kila kijana wa Bahi awe na kazi ya kufanya hivyo niwaombe muwe mabalozi wazuri katika zoezi la ukusanyaji wa ushuru mbalimbali ili asilimia kumi ya mapato hayo iendelee kurudi kwenu na kuwafikia wengi zaidi.” Amesema Munkunda na kuongeza:
“Niwaombe mliokopeshwa jengeni utamaduni wa kurejesha kwa wakati ili fedha hizi ziendelee kuzunguka na kunufaisha wengi zaidi, na ambao hawatarejesha mikopo tutawashughulikia kama wanavoshughulikiwa wahujumu uchumi kwani utakuwa umeihujumu Halmashauri na wananchi wote kwa sababu fedha hizo zinapaswa kuzunguka kwenda kwenye vikundi vingine na siyo kubaki kwenye kikundi kimoja.”
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Donald Mejiti amewashauri wajasiriamali hao kujiunga na Mfuko wa Afya wa Jamii Iliyoboreshwa (CHF) ili kujihakikishia matibabu pindi wanapougua na kupunguza gharama za matibabu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wilaya ya Bahi Dkt. Fatuma Mganga amewaasa wajasiriamali hao kutafuta fursa ili waweze kuinua vipato vyao kwa haraka badala ya kubaki wakisubiri ziwafikie mahali walipo.
Awali akitoa taarifa kwa Mgeni rasmi, Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Bahi, Denis Komba amesema vikundi 33 vimehudhuria. Ambapo kati ya hivyo vikundi vilivyopewa mikopo ni 25 vikijumuisha wanawake, vijana na wenye ulemavu ambavyo vinajishughulisha na ufugaji, mama ntilie, ushonaji wa nguo, kilimo cha mbogamboga na matunda pamoja na boda boda.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa