Benton Nollo, Jackson Matulanga na Ester Miraji (SAUT), Bahi
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb) ametoa wito kwa wafugaji wote nchini kubadilisha fikra zao za namna ya ufugaji wa kienyeji na kuwa wa kisasa ili uweze kuwanufaisha na kuongeza pato la taifa.
Waziri Ndaki ametoa wito huo wilayani Bahi mkoani Dodoma wakati akizungumza na Wafugaji kwenye Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji Wilaya ya Bahi uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri hiyo tarehe 27 Agosti 2021 ambapo Waziri huyo alikuwa Mgeni Rasmi.
Ndaki amesema kwamba Tanzania licha ya kuwa ya pili kwa kuwa na mifugo mingi barani Afrika lakini mchango wake katika pato la taifa umekuwa mdogo.
“Wafugaji tuna mifugo mingi, lakini maisha yetu jamani jamani…mavazi yake…nyumba yake anayokaa, we unataka tu waongezeke, sawa, wataendelea kuongezeka lakini kwa faida ya nani?” Amesema Ndaki na kuongeza;
“Hivi sasa Wafugaji lazima tuanze kufuga kibiashara, tubadilishe fikra, tukibadilisha fikra mchango wetu kiuchumi katika taifa letu utakuwa mkubwa…kutoka ngazi ya familia mpaka ngazi ya taifa.”
Awali, akizungumza Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda ameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kudhibiti uuzaji holela wa dawa za mifugo kwa kuwa una athari kubwa katika ustawi wa mifugo.
“Mheshimiwa Waziri suala la uuzaji holela wa dawa za mifugo ni tatizo kubwa, mbona hatukuti panado zimepangwa minadani kama nyanya? Lakini, wafugaji hawa pia kwa sababu wanaishi na ng’ombe muda mrefu nao wanajiona kuwa ni madaktari, wananunua dawa minadani…anazunguka nayo mnadani siku nzima ikiwa kwenye koti, akifika nyumbani na wakati mwingine amelewa…anafikia kuwachoma hivyo hivyo…mazingira ya utaratibu huu yanasababisha athari kubwa sana kwa mifugo.” Amesema Munkunda.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Bahi, Kenneth Nollo ameiomba Serikali kupitia Wizara hiyo kutenga maeneo maalum ya malisho kwa kupanda nyasi kwa kuwa suala hilo ndiyo msingi wa ufugaji wa kisasa na wenye tija kwa wafugaji.
“Binafsi nimewahi kusafiri kutoka Lusaka mpaka Viktoria, maeneo yote ya malisho yamewekwa uzio na maeneo ya malisho yanaonekana, kwa hivyo na sisi hebu tufike wakati tuseme huu ukanda tunateua kwa ajili ya mifugo.” Amesema Mheshimiwa Nollo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania Jeremiah Wambura ameiomba wizara hiyo kuanzisha mnada mkubwa wa kimataifa wilayani Bahi kutokana na kwamba wilaya hiyo ndiyo wilaya pekee mkoani Dodoma inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo hasa ng’ombe ukilinganisha na wilaya nyingine za mkoa huo.
“Mheshimiwa Waziri nasema hivyo kwa sababu mahali Wilaya ilipo pamekaa kimkakati na ni rahisi kufikika…wao kwa maana ya Halmashauri waangalie sasa eneo maalum zuri na tunaamini wewe utatusaidia…eneo hilo litengwe liwe ni eneo maalum la kupokelea mifugo na kunenepeshwa pale ili ilingane na soko la kimataifa na kisha kupelekwa katika mnada huo.” Amesema Wambura.
Akishukuru kwa niaba ya Wafugaji hao, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Donald Mejiti amesema mifugo ni utajiri mkubwa hasa ukifuga kisasa na kwa tija ya kunufaika na mifugo hiyo.
“Anachosema Mheshimiwa Waziri na ni kweli tubadilishe fikra zetu, mifugo ni utajiri lakini tufuge kulingana na mahitaji ya mlaji, shida tuliyonayo sisi tunafuga tunavyotaka sisi, halafu tumpelekee mlaji…ukifuga unavyota wewe unakuwa umeshapishana na mahitaji ya mlaji…walaji wanataka chanjo, walaji wanataka josho na wanataka malisho bora…tuanze kufikiri na kutambua kwamba tuna utajiri mkubwa ambao utatupatia fedha za kigeni.” Amesema Mejiti.
Mkutano wa Wafugaji wilayani Bahi hufanyika mara moja kila mwaka kwa lengo la kujadili changamoto zinazowakabili wafugaji na kuzipatia ufumbuzi.
Matukio Katika Picha:
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb) (aliyevaa tai nyekundu) akiwasili Bahi na kusalimiana na viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Bahi kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji wilayani humo uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb) akizungumza wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji wilayani Bahi uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb) (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (kushoto) wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji wilayani humo uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb) (kushoto) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Wafugaji Wilaya Ibrahim Jamal (kulia) wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji wilayani humo uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda akizungumza wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji wilayani humo uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb).
Mbunge wa Jimbo la Bahi, Kenneth Nollo (Mb) akizungumza wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji Wilaya ya Bahi uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb).
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Donald Mejiti akizungumza wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji Wilaya ya Bahi uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb).
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Athumani Masasi akizungumza wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji Wilaya ya Bahi uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb).
Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Jeremiah Wambura akizungumza wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji Wilaya ya Bahi uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb).
Katibu wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Joshua Lugaso akizungumza wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji Wilaya ya Bahi uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb).
Mwenyekiti wa Wafugaji Wilaya ya Bahi, Ibrahim Jamal akizungumza wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji Wilaya ya Bahi uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb).
Katibu wa Wafugaji Wilaya ya Bahi, Mazengo Michael Mazengo akiwasilisha changamoto zinazowakabili Wafugaji Wilaya ya Bahi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb) wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji wilayani humo uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021. Ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb).
Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania, Daniel Mushi akizungumza wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji Wilaya ya Bahi uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb).
Wataalam mbalimbali wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa nyakati tofauti wakizungumza wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji Wilaya ya Bahi uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb).
Meneja wa Bemki ya NMB Tawi la Bahi, Wilbert Mwalusito akitoa elimu juu ya umuhimu wa Bima ya Mifugo kwa Wafugaji walioshiriki Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji Wilaya ya Bahi uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb).
Viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Bahi, Wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Watumishi na Wafugaji wakisikiliza kwa makini uwasilishaji wa mada mbalimbali wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji Wilaya ya Bahi uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb).
Viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Bahi, Wataalamu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Watumishi na Wafugaji wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb) (aliyevaa tai nyekundu waliokaa) baada ya Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji Wilaya ya Bahi uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021 ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri huyo.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (Mb) akiagana na viongozi wa Wilaya ya Bahi baada ya Mkutano wa Mwaka wa Wafugaji wilayani Bahi uliofanyika kwenye viwanja vya Halmashauri tarehe 27 Agosti 2021.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa