Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 12, umeanza kwa kumchagua Mbunge wa Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma, Mhe. Job Yustino Ndugai (Mb) kuwa Spika wa Bunge hilo kwa kura 344 kati ya kura 345 zilizopigwa sawa na asilimia 99.7.
Matokeo hayo yametangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai katika kikao cha uchaguzi huo ambacho kiliongozwa na mwenyekiti wa muda, Mheshimiwa William Lukuvi.
Akizungumza mara baada ya kiapo, Mhe. Ndugai aliwashukuru wabunge kwa ushindi huo wa kishindo huku akiwataka Wabunge wote hususan wapya kusoma Kanuni za kudumu za Bunge pamoja na Sheria mbalimbali zinazohusiana na Bunge.
"Muwe tayari kuchapa kazi kama kuna tatizo lolote msisite kuja kuniona bila wasiwasi wowote mimi nipo kwa ajili yenu wote,” Amesema Ndugai.
Aidha, Ndugai aliongeza kuwa uwepo wa wabunge wengi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) haina maana kwamba Bunge hilo litakuwa Bunge la ‘Ndiyo Mzee’ na kuwataka wabunge hao wasisikilize maneno ya watu badala yake wachape kazi.
"Mimi nakataa kwamba kuwepo Wabunge wengi wa CCM humu ndani haimaanishi ndiyo kila kitu watu wataitikia ndiyo au hapana hapana utekelezaji wa majukumu utafanyika Kama kawaida.” Amesema Mhe. Ndugai na kuongeza;
“Hata hivyo, mkiamua kuwa mabubu ili muonekane mna nidhamu shauri zenu kwani mtatoa majibu kwa wananchi waliowachagua muwasemee mambo yao baada ya miaka mitano,”
Mhes. Ndugai aliwaambia Wabunge wa upinzani kwamba licha ya uchache wao Bungeni lakini wana haki zote kama Wabunge wengine hivyo na wao lazima wasikike.
Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa kwanza wa Bunge la Kumi na Mbili kimeendelea pia na uapisho kwa wabunge wateule.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa