Tume ya Taifa ya Uchaguzi – NEC, imemkabidhi rasmi cheti cha ushindi Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Pombe Magufuli baada ya kupata ushindi wa asilimia 84.4 katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.
Cheti hicho kimekabidhiwa na Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage Makao Makuu ya ofisi hizo Njedengwa jijini Dodoma leo tarehe 01 Novemba 2020.
Dkt. Magufuli ametumia fursa hiyo kuwashukuru Watanzania huku akiwakumbusha Watanzania kuendelea kuchapa kazi ili kujiletea maendeleo.
Pia, Dkt. Magufuli amewashukuru Watanzania kwa kukipatia ushindi mkubwa chama chake cha Mapinduzi (CCM) katika nafasi ya Urais, Ubunge, Udiwani na kule Zanzibar katika nafasi ya Urais, Uwakilishi na nafasi ya Udiwani.
''Kupata asilimia 84.4 ni imani kubwa sana kwa Watanzania na nasema kwa dhati nina deni kubwa sana kwa Watanzania, imani yao nitaitimiza kwa kufanya kazi sana usiku na mchana”. Amesema Rais Mteule Dkt. Magufuli na kuongeza;
“Siasa sio vita, siasa sio ugomvi, sisi sote ni Watanzania, napenda kuwaahidi nitashirikiana nanyi katika kuhakikisha tunasukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu. Tanzania kwanza mambo mengine baadaye".
Kadhalika, Dkt. Magufuli hakusita kuwashukuru viongozi wa dini ambao kwa kipindi chote cha uchaguzi waliweza kuwaongoza Watanzania kwa dua na sala na hatimaye kumaliza uchaguzi kwa usalama na taifa lao kuendelea kubaki na amani.
Aidha, Dkt. Magufuli amewashukuru wapinzani wake waliokubali matokeo akisema ''Nawashukuru na kuwapongeza kwa kukubali matokeo na kuja kushiriki hafla hii. Hii ni ishara ya kukomaa kwenu kisiasa hongereni sana. Ni kweli kwamba wananchi wametupatia ushindi mkubwa sana, lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya kudharau maoni na ushauri wenu".
Vile vile, kiongozi huyo aliendelea kutoa shukurani zake kwa kusema "Navishukuru pia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kuhakikisha amani na usalama vinatawala katika kipindi chote cha uchaguzi'.
Kwa nafasi ya kipekee Dkt. Magufuli amewashukuru viongozi wa nchi nyingine waliomtumia salamu za pongezi.
Rais Mteule Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuapishwa Alhamisi tarehe 05 Novemba 2020 katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ambapo kwa mujibu wa Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbas aliyezungumza baada ya hafla hiyo amesema kwamba maandalizi kwa ajili ya tukio hilo yamekamilika kwa zaidi ya asilimia 99 na Serikali itaendelea kuwataarifu mara kwa mara.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) akipokea Cheti cha Ushindi wa Kiti cha Urais kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi - NEC, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage (kushoto) mara baada ya kutangazwa mshindi kwa Kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020, hafla hiyo imefanyika Makao Makuu ya NEC Njedengwa jijini Dodoma tarehe 01 Novemba 2020.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan (wa tatu kutoka kulia) akipokea Cheti cha Ushindi wa Kiti cha Makamu wa Rais kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi - NEC, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage (kushoto).
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli (wa pili kushoto) akionesha Cheti cha Ushindi wa Kiti cha Urais alichokabidhiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi - NEC, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage (kushoto) mara baada ya kutangazwa mshindi wa nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 28 Oktoba 2020.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli (katikati) akiwa amesimama na Waliogombea Urais kupitia vyama Mbalimbali vya Upinzani nchini wakati Wimbo wa Taifa ukipigwa katika hafla fupi ya kukabidhi Cheti cha Ushindi kwa Kiti cha Urais zilizofanyika Makao Makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi - NEC Njedengwa jijini Dodoma tarehe 01 Novemba 2020.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa