Na Benton Nollo, Bahi
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo pamoja na Viongozi wa Wilaya ya Bahi, wamewatembelea na kuwajulia hali wananchi wa Vitongoji vya Bweseti na Chiwona vilivyopo katika Mji wa Bahi ambavyo vimeathiriwa na mafuriko na mvua yenye upepo mkali tarehe 15 Januari 2020.
Dkt. Mahenge katika ziara yake hiyo aliyoifanya tarehe 21 Januari 2020, alichangia shilingi milioni 3 kwa ajili ya kugharamia mahitaji mbalimbali muhimu kwa wahanga.
"Nitumie fursa hii kuwaagiza wananchi wote kuhama katika eneo hili (Bweseti) ambalo kimsingi ni hatarishi kwa sababu ndipo Mto Bubu unapotapika maji yake...na nimeambiwa na viongozi wa Wilaya kuwa eneo hili awali halikuwa la makazi bali wakulima wa mpunga walilitumia kujenga vibanda wakati wa msimu wa kilimo lakini ninyi mmefanya makazi". Anasema Dkt. Mahenge na kuongeza;
Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Bahi fanyeni maandalizi ya kuwahamisha wananchi hawa katika eneo hili na wapelekwe katika eneo lisilo na athari za mafuriko lakini pia naziagiza Halmashauri zote za Dodoma najua zipo katika maandalizi ya Bajeti, ziweke mpango wa ujenzi wa mabwawa mapya na hata kuyafufua yale yaliyojengwa wakati wa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ili kuvuna maji haya na kwa kufanya hivyo mafuriko yanaweza kupungua".
Pia, Dkt. Mahenge àmewasihi wananchi kutunza mazingira ili kuepuka athari zinazoletwa na mabadiliko ya tabia ya nchi.
"Ndugu zangu, haya yote yanatokea ni kwa sababu sisi binadamu tunaharibu mazingira yetu kwa kukata miti na kuchoma moto, mvua kubwa kama hizi zinaponyesha mkusanyiko wa maji unakuwa mkubwa na hatimaye huleta madhara". Anasema Mahenge.
Dkt. Mahenge amewataka wananchi wa Bahi pamoja na wahanga hao kuendelea na shughuli zao za uzalishaji mali na hasa shughuli za kilimo kwa kuwa ndiyo msimu husika.
Kadhalika, amewasihi wananchi kuzitumia mvua hizo kulima mazao ya chakula na mazao ya biashara, kwamba hata kama mafuriko yametokea lakini bado wananchi wana jukumu la kuzalisha chakula cha kutosha na kuongeza kuwa baadaye hataruhusu maombi yoyote ya kupatiwa chakula na serikali kwa sababu ya njaa kwa kuwa mvua msimu huu zinanyesha kiwango cha kutosha kuzalisha chakula cha kutosha.
Picha za Matukio wakati wa ziara hiyo:
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge (wa pili kutoka kushoto) akiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo pamoja na Viongozi wa Wilaya ya Bahi, wamewatembelea na kuwajulia hali wananchi wa Vitongoji vya Bweseti na Chiwona vilivyopo katika mji wa Bahi ambavyo vimeathirika na mafuriko na mvua yenye upepo mkali tarehe 21 Januari 2020.
Baadhi ya askari wa kikosi cha Jeshi la Akiba/Mgambo wilayani Bahi waliohusika katika kazi ya kujenga mahema kwa ajili ya kuandaa makazi ya muda ya wananchi waliokumbwa na mafuriko kwenye vitongoji vya Mji wa Bahi. Mahema hayo yametolewa na Shirika la Red Cross Tanzania kwa Kata za Chali na Bahi ambazo ndizo zilizoatiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa