Na Angela Msimbira, OR - TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Selemani Jafo amesema Serikali inaendelea na taratibu za kuajiri walimu 12,000 wapya kwa Shule za Msingi na Sekondari na zitakapokamilika zitatangazwa.
Jafo ameyasema hayo leo alipokuwa akizungumza kwenye Siku ya TAMISEMI, kueleza mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha miaka mitano katika sekta ya elimu iliyofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Dodoma.
Amesema kuwa kwa kipindi cha miaka mitano walimu zaidi ya 18,000 wameajiriwa na kupelekwa Shule za Msingi na Sekondari na kwamba ajira zingine 12,000 zilizoelekezwa na Rais John Magufuli bado taratibu zake zinaendelea.
“Nafahamu bado kuna changamoto ndio maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli ametoa maelekezo ya kuongeza ajira za walimu na ametoa maelekezo ya ajira zaidi ya 12,000 taratibu zinaendelea zikikamilika Serikali itaongeza ajira zingine kwa shule za msingi na sekondari,”amesema Mhe. Jafo.
Akizungumzia kuhusu mafanikio yaliyopatikana kwa miaka mitano katika Sekta ya Elimu ya Msingi na Sekondari Mhe.Jafo amesema katika kipindi hicho kiasi cha Sh.Trilioni 1.09 zimetolewa kwa ajili ya elimu bila malipo.
Amefafanua kuwa kuwa zaidi ya Sh.Bilioni 502 zimetolewa kwa ajili ya elimu ya Shule za Msingi na Sh.Bilioni 593.9 zimeenda sekondari, jambo ambalo limesaidia watoto wa maskini kupata elimu.
“Mwaka 2016 watoto wengi walifurika kwenye shule zetu wakati zikiwa zimekadiria watoto 200 hadi 400, zingine ziliweza kusajili hadi wanafunzi 1,000, kwa mfano shule ya Nyakanazi na Majimatitu na watoto wengine walisajiliwa wakiwa na miaka 10 kutokana na miaka mitatu nyuma walikosa fursa hiyo,”amesema Jafo.
Ameendelea kufafanua kuwa katika kipindi cha miaka mitano zaidi ya Sh.Bilioni 501 zimetolewa kwa ajili ya kuboresha miundombinu mbalimbali na hadi kufikia mwezi Juni 2020 ujenzi wa shule mpya za Msingi 905 zilikuwa zimekamilika hivyo kuongeza idadi ya shule za Msingi kutoka 16,899 mwaka 2015 hadi 17,804 mwaka 2020.
Pia amesema vyumba vya madarasa 17,215 vimejengwa na kuongezeka kutoka vyumba 108,504 mwaka 2016 hadi 125,719 mwaka 2020, sawa na ongezeko la asilimia 13.7 ambapo ujenzi wa vyumba 3,049 unaendelea na ukikamilika idadi ya vyumba vya madarasa kwa shule za Msingi itafikia 128,768.
Aidha, amesema serikali imejenga shule mpya za Sekondari 228 na hivyo kuongezeka kutoka shule 4,708 mwaka 2016 hadi 5,330 mwaka 2020.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Mhandisi Joseph Nyamhanga, amesema uwekezaji na maboresho yaliyofanyika katika sekta ya elimu kwa shule za msingi na sekondari umesaidia kuongeza kiwango cha ufaulu katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kutoka asilimia 67.84 mwaka 2015 hadi asilimia 81.50 mwaka 2019.
Naye, Naibu Katibu Mkuu, Tamisemi anayeshughulikia Elimu, Gerald Mweli, amesema Mpango wa Elimu bila malipo ulianzishwa mahsusi baada ya utafiti walioufanya mwaka 2014 kuonyesha kuwa Watoto milioni 3.5 wapo nje ya Shule kutokana na kukosa ada.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa