Na Benton Nollo, Bahi
Serikali wilayani Bahi imewaahidi Wakulima wa mpunga wilayani humo kuwa ipo tayari kufanya mazungumzo na taasisi za kifedha kuona namna ambavyo wakulima hao watafanikiwa kurejesha fedha walizokopa baada ya zaidi ya ekari 11,000 za mashamba ya mpunga zilizokuwa katika hatua ya uvunaji kufunikwa na maji kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha kwenye mikoa ya jirani (Manyara na Arusha).
Mashamba yaliyokumbwa na athari hiyo ni katika Skimu za Bahi Makulu (ekari 9,000), Bahi Sokoni (ekari 2,347) na Nguvumali (ekari 371) ambapo kwa baadhi ya wakulima wanalazimika kuvuna mpunga kwa kutumia mitumbwi.
Akizungumza na Wakulima wa skimu hizo Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda aliyekuwa kaambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo amesema atashirikia na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kuzungumza na benki zilizowakopesha wakulima hao ili kuona namna nzuri ambayo itawasaidia wakulima kurejesha mikopo.
“Viongozi wa AMCOS ili tulishughulikie suala hili ipasavyo ni vema sisi kama Serikali tukapata haraka orodha ya mashamba na wakulima kwa kiasi walichokopa, wamerejesha shilingi ngapi na kiasi gani bado…pia, natambua kuna baadhi ya wakulima wamekopeshwa na watu binafsi…tafadhali wasiwasumbue wananchi kwa kuwa hali halisi wanaiona na atakayewasumbua nipatiwe taarifa haraka”. Amesema Munkunda.
Munkunda ambaye alitumia usafiri wa gari, pikipiki na mtumbwi kwa takriban kilomita 20 kuwafikia wakulima hao na kujionea athari waliyoipata, amewatia moyo kwamba pamoja na athari hiyo, amewaagiza Wataalam wa Kilimo kupanga mikakati ya kuyatumia maji hayo kwa ajili ya shughuli nyingine za kilimo cha umwagiliaji hasa zao la vitunguu ambavyo kwa sasa vina soko zuri pamoja na mboga mboga kama mazao mbadala ya biashara.
“Kuvunjika kwa koleo siyo mwisho wa ujenzi…najua maisha ya wananchi wengi wa Bahi Sokoni na Bahi Makulu yamekuwa bora kutokana na kilimo cha mpunga, nafahamu mmechukua mikopo kwa ajili ya mashamba haya, tutazungumza na benki kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa ili tuone namna ya kuusogeza mbele muda wa marejesho”. Amesema Munkunda.
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) Bahi Makulu, Hilary Ndugai amesema Skimu ya Bahi Makulu ni kubwa sana na yote imefunikwa na maji yaliyoletwa na Mto Bubu ambao chanzo chake ni mikoa ya Manyara na Arusha.
“Hali hii imefuta matumaini yetu wakulima wa Bahi, hasa ikizingatiwa kuwa tulichukua mikopo ili tulime na tunatakiwa kurejesha wakati wa mavuno, mpunga ulikuwa tayari umeshakomaa, tulikuwa tunasubiri tu kuvuna, lakini sasa kama mnavyoona maji ni mengi na yamefunika mpunga wote”.
Naye Makamu Mwenyekiti wa AMCOS hiyo, Ally Mahimbu, aliiomba Serikali kuzungumza na taasisi za fedha zilizowakopesha ili kutoa unafuu kwenye urejeshaji wa mikopo hiyo kutokana na kupata athari ya mvua.
“Kutokana na athari hizi za mafuriko nina uhakika kuna watu watashindwa kurejesha, tunaomba Serikali izungumze na benki kusogeza mbele utaratibu wa kurejesha kidogo kidogo hata baada ya msimu huu kuisha”. Amesema Mahimbu.
Akitoa taarifa kwa Mkuu wa Wilaya, Mtendaji wa Kijiji cha Bahi Makulu, Lightness Swai amesema katika msimu wa kilimo wa mwaka 2019/2020 wakulima walilima ekari 9,000 za mpunga na zote zimefunikwa na maji.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mpamantwa, Sostheness Mpandu alisema msimu wa kilimo uliopita wakulima walipata hasara kutokana na kupata mvua chache, na mwaka huu walijipanga na kulima tena kwa kuwa mvua zilikuwa nyingi na za kutosha lakini mwaka huu (2020) wamepata hasara kwa maji ya mto kufunika mashamba yote.
Hali hiyo imetokana na Bwawa la Sulungai ambalo ndiyo ukomo wa mto huo kujaa maji na kufikia kiwango chake sha mwisho hivyo, kusababisha maji yanayoletwa na Mto Bubu kufunika mashamba ya mpunga.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (mwenye kilemba chekundu) akishuka kwenye pikpiki ili kuwafikia Wakulima wa Mpunga katika Skimu ya Nguvu Mali Block namba 04 tarehe 08 Mei 2020 ambao baadhi ya mashamba yao yamefunikwa na maji yanayoletwa na Mto Bubu kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika mikoa ya Arusha na Manyara.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (mwenye kilemba chekundu) pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo wakiangalia uharibifu wa miundombinu uliotokana na maji yaliyoletwa na Mto Bubu kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika mikoa ya Arusha na Manyara.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (mwenye kilemba chekundu) pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo wakitumia usafiri wa mtumbwi ili kuwafikia Wakulima wa Mpunga katika Skimu ya Nguvu Mali Block namba 04 tarehe 08 Mei 2020 ambao baadhi ya mashamba yao yamejaa maji yaliyoletwa na Mto Bubu kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika mikoa ya Arusha na Manyara. Kwa kuwa zao hilo lilisha komaa, inawalazimu kuvuna kwa kutumia mtumbwi hali ambayo inaongeza gharama kubwa kwa mkulima.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (mwenye kilemba chekundu) pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo wakimsikiliza Afisa wa Kilimo, Solomon Chapa (wa kwanza kushoto) wakati akitoa maelezo ya namna wakulima walivyopata athari na maji hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (mwenye kilemba chekundu) akiangalia mpunga ulioanikwa ili kukausha maji baada ya kulowana na maji ya Mto Bubu yaliyofunika mashamba yao.
Mustapha Hussein ambaye ni mkulima katika Skimu ya Nguvumali block namba 04 iliyopo Kijiji cha Bahi Sokoni akishusha Mpunga wake kwenye mtumbwi na kuuanika kabla ya kuusafirisha kwenda nyumbani.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda akizungumza na wakulima wa Skimu ya Bahi Sokoni na Nguvumali tarehe 08 Mei 2020.
Baadhi ya wakulima wakizungumza na kumshukuru Mkuu wa WIlaya ya Bahi (hayupo pichani) kwa uamuzi wake pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya, kuiwatembelea na wamesema kitendo hicho kimeonesha kwa Serikali inawajali na ipo karibu nao hasa katika kipindi hiki kigumu kwao.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa