Rais Mteule Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameapishwa rasmi leo tarehe 05 Novemba 2020 jijini Dodoma huku akishuhudiwa na maelfu ya wananchi wa Watanzania pamoja na wageni waalikwa kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo Marais, Makamu wa Rais , Mawaziri na viongozi wa dini.
Kabla ya kula kiapo, Dky. Magufuli aliingia Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma majira ya saa nne asubuhi na kisha kuzunguka uwanja kwa ajili ya kuwasalimia wananchi walijitokeza kushuhudia tukio hilo akiwa katika gari ya wazi.
Baada ya kuzunguka uwanja alishuka kwenye gari na kisha kuelekea eneo maalum kwa ajili ya Wimbo wa Taifa pamoja na mizinga 21. Baada ya hapo ikashushwa bendera ya Rais ikiwa ni ishara ya kuhitimisha Muhula wa Kwanza wa uongozi wake katika kipindi cha Awamu ya Tano.
Hata hivyo, baada ya kushushwa Bendera ya Rais, Dkt. Magufuli alielekea kwenye jukwaa maalum kwa ajili ya kula kiapo ambapo Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma ndiye aliyemuapisha na kisha alipewa ngao na wazee wawili mmoja kutoka Tanzania Bara na mmoja kutoka Tanzania Visiwani.
Dkt. Magufuli baada ya hapo alikaa kitini na kisha ikafuata hatua ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan kula kiapo cha kutumikia nafasi hiyo. Walipomaliza kula kiapo ikafuata nafasi ya dua ambayo iliombwa na viongozi wa dini zote.
Baada ya dua hiyo kumalizika Rais Dkt. Magufuli, Makamu wa Rais wakiwa wameongozana na Jaji Mkuu, wazee, viongozi wa dini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali walifanya maandamano kutoka kwenye jukwaaa ambalo lilitumika kwa ajili ya kumuapisha huku gwaride maalum likiwa limetengeneza umbo la Alfa ikiwa ni ishara ya kuanza kwa muhula wa pili wa miaka mitano ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Wakati tukio hilo likiendelea utulivu uwanjani hapo ulikuwa mkubwa, wananchi na wageni waalikwa walikuwa kimya, Rais Dkt. Magufuli alienda eneo maalum kwa ajili ya gwaride hilo lilikuwa katika umbo la Alfa na baadaye mizinga mingine 21 ilipigwa. Baada ya hapo alikagua gwaride hilo huku ndege za kivita zikipita angani.
Rais Dkt. Magufuli baada ya kumaliza kukagua gwaride alienda moja kwa moja jukwaa kuu. Wakati huo wananchi na wageni waalikwa wote walikuwa wamesimama huku shangwe zikirindima. Gwaride liliendelea kutoa burudani na kisha kufuatiwa tena na Wimbo wa Taifa.
Hata hivyo, gwaride maalum ambalo liligawanyika katika sehemu tatu ikiwemo kikosi cha Askari waliobeba Bendera ya Rais. Hata hivyo gwaride likipita mbele ya Rais shangwe zilitawala uwanjani hapo hasa walipoingia makomandoo.
Baada ya gwaride kutoka uwanjani ilifuata hatua ya utambulisho wa wageni waliohudhuria tukio hilo la kihistoria ambalo hutokea kila baada ya miaka mitano. Baadhi ya wageni hao ni Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museven, Rais wa Comorro, Kazar Othaman na Rais wa Zimbabwe Emmason Mnangagwa. Pia, wametambulishwa wawakilishi wa nchi mbalimbali pamoja na mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini Tanzania.
MATUKIO KATIKA PICHA:
Rais Mteule Dkt. John Pombe Joseph Magufuli (anayepunga mkono juu ya gari) akiwasalimia maelfu ya wananchi na wageni mbalimbali waliojitokeza kushuhudia kiapo chake kwa ajili ya kuiongoza Tanzania muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Tano. Sherehe hizo zimefanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma leo tarehe 05 Novemba 2020.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akielekea katika jukwaa baada ya kuapishwa tarehe 5 Novemba 2020 katika Uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni mara baada ya kuapishwa tarehe 05 Novemba 2020 katika sherehe zilizofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Wananchi na Wageni mbalimbali wakifuatilia shughuli za sherehe za Uapisho wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 05 Novemba 2020 zilizofanyika katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma. (Picha zote na Ikulu).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa