Na Benton Nollo, Kigwe
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amewataka Wapangaji wa majengo ya kilichokuwa Kituo cha Ufundi wa Zana za Kilimo kutunza mazingira, wakati huu ambapo Serikali inajipanga kufufua chuo hicho kilichopo Kijiji cha Mapinduzi Kata ya Kigwe wilayani humo.
Munkunda ameyasema hayo baada ya kufanya ukaguzi wa majengo 16 na miundombinu mbalimbali iliyopo kituoni hapo tarehe 02 Aprili 2020.
“Ndugu zangu Wapangaji nimesikitishwa sana kulikuta eneo hili likiwa katika hali ya uchafu uliokithiri ilhali ninyi mpo na kwa baadhi ya majengo wenzenu wengine wanadiriki kuweka mifugo jambo ambali linahatarisha usalama wa majengo haya ambayo ni muhimu kwa matumizi ya baadaye”. Anasema Munkunda na kuongeza,
“Eneo hili lina mali nyingi na ni muhimu sana kwa kukuza uchumi wa Wilaya yetu ya Bahi hivyo, linatakiwa kuwa safi wakati wote”.
Kutokana na changamoto ya wapangaji hao kutolipa Kodi ya Pango kwa wakati na wengine kutolipa kabisa, Munkunda ametoa siku 30 ambapo kuanzia tarehe 01 Mei 2020 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ambayo ndiyo mmiliki wa Kituo hicho itapanga utaratibu mpya wa namna ya kulipa Kodi ya Pango na matumizi ya eneo hilo.
Pia, Munkunda ameuagiza uongozi wa Kijiji cha Mapinduzi na Kijiji cha Kigwe kuhakikisha kuwa mpaka tarehe 30 Aprili 2020 mabati na baadhi ya vifaa vilivyoibiwa kituoni hapo viwe vimepatikana.
Kituo hiki kilijengwa kwa kibali cha Mkurugenzi wa Maendeleo Mkoa wa Dodoma - RDD mwaka 1975 na kilianza kufanya kazi rasmi mwaka 1976 kikisimamiwa na Wizara ya Kilimo na maelekezo ya uendeshaji yalikuwa yakitolewa na Taasisi ya Majaribio ya Zana za Kilimo Arusha - TAMTU (Tanzania Agricultural Machinery Testing Unit).
Mwaka 1980 Shirika la Kijerumani la KUBEL STIFTANG kupitia Mradi wa Maendeleo Mkoa wa Dodoma – DODEP lilianza kutoa ruzuku na kupanua chuo hicho kwa kuongeza nyumba za watumishi.
Aidha, ilipofika mwaka 1996 Kituo kilikabidhiwa kwa Halmashauri ya WIlaya ya Dodoma Vijijini wakati huo ambayo kwa sasa ni Bahi na kwa kuwa Halmashauri hiyo haikuwa na uwezo wa kukiendesha kituo hicho tarehe 04 Desemba 2003 ilikikabidhi kwa mkataba Kituo kwa Shirika la KISEDET (Kigwe Social Economic Development and Trainning).
Ambapo ilipofika tarehe 10 Agosti 2016, shirika la KISEDET liliamua kurudisha Kituo hicho kwa Mmiliki wake ambaye ni Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Majengo yaliyokabidhiwa ni nyumba 16, bweni 1, madarasa 6, jengo 1 la utawala lenye ofisi 5, mabanda ya mifugo 2, mtambo wa Biogas na jengo la karakana.
PICHA NA MATUKIO:
Baadhi ya Majengo ya Kituo cha Ufundi Kigwe yakiwa katika hali ya uchafu.
Pichani juu ni Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda akikagua majengo na zana zilizopo katika Kituo cha Ufundi Kigwe tarehe 02 Aprili 2020 ambapo pia aliambata na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo.
Mkuu wa Wilaya na Bahi, Mwanahamisi Munkunda (mwenye kiremba cha bluu) akiwa katika kikao cha pamoja na wapangaji wa Kituo cha Ufundi Kigwe ambapo pia kilihudhuriwa na wajumbe wa Serikali za Vijiji vya Kigwe na Mapinduzi tarehe 02 Aprili 2020. (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa