Na Benton Nollo
Wataalam na Wadau wa afya mkoani Dodoma wametakiwa kusimamia vema ukarabati wa Vituo vya Afya unaoendelea hivi sasa mkoani humo ili vituo hivyo wiweze kuanza kutoa huduma za uzazi na mtoto mapema. Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Wilaya ya Bahi, Jeremia Mapogo aliyekuwa Mgeni Rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya hiyo kwenye ufunguzi wa kikao cha siku mbili kinachofanyika kimkoa wilayani humo kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga kwa kipindi cha Aprili hadi Juni, 2018.
Mapogo alifafanua kuwa uboreshaji wa vituo hivyo kwa kiasi kikubwa utafanya lengo la mkoa wa Dodoma kupunguza vifo hivyo kutoka 60/100,000 mpaka 55/100,000 ya vizazi hai ifikapo Desemba, 2018 ambapo kwa sasa kiwango cha vifo Kimkoa ni 60/100,000 ya vizazi hai hali ambayo takwimu hizi inaonyesha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya kama mkoa ili kuweza kufikia malengo yaliyopangwa.
Aidha, Mapogo alieleza kuwa pamoja na mikakati ambayo Wataalam hao wamejiwekea, pia anatambua kuwa kuna changamoto nyingi zinazozuia kufikia malengo ya kupunguza vifo hivyo ambayo alizitaja kuwa ni; Mwitikio hafifu kutoka kwa wananchi, yaani (akina mama kutozalia katika vituo vya huduma za afya), pamoja na kuchelewa kuanza kliniki chini ya umri wa miezi mitatu (3), Vituo vichache vya kutolea huduma za afya kwani bado hatujafikia lengo la serikali la kila kijiji kuwa na Zahanati na kila Kata kuwa na Kituo cha Afya, Matumizi madogo ya njia za uzazi wa mpango katika jamii, Upungufu wa wataalamu wa afya kuendana na Ikama, Upungufu wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya huduma za afya, Upungufu wa magari ya kubebea wagonjwa hususani wagonjwa wa dharura kama wajawazito,Mwitikio hafifu wa elimu ya uzazi na mtoto inayotolewa kwa jamii nzima na changamoto nyinginezo kwa kila Wilaya.
Mapogo aliwapongeza wataalam hao kuwa pamoja na changamoto hizo lakini bado wameonesha mikakati ambayo wamejiwekea katika kutekeleza azma ya serikali ya awamu ya tano ya kupunguza vifo vya akinamama vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga mkoani Dodoma kwa kuhakikisha wajawazito na wenza wao wanahudhuria kliniki mara mama apatapo ujauzito, kuongeza kiwango cha kujifungulia katika vituo vya huduma za afya kutoka asilimia 81 hadi asilimia 85 ifikapo Desemba, 2018.
Pia, kuongeza mahudhurio ya kliniki kwa wazazi baada ya kujifungua kutoka asilimia 48 hadi asilimia 80 ifikapo Desemba, 2018, kuendelea kuboresha huduma za chanjo kufikia kiwango cha asilimia 95 kwa watoto ifikapo Desemba, 2018, kuendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na CHF iliyoboreshwa, kuhakikisha Hospitali zote 8 zilizopo katika Mkoa wa Dodoma zinatoa huduma ya njia ya kangaroo kwa watoto wanaozaliwa njiti ifikapo Desemba, 2018 na kuhakikisha vituo vya afya 8 kati ya 36 vinatoa huduma ya dharura ya upasuaji kwa akina mama wajawazito ifikapo Desemba, 2018.
Kadhalika, Mapogo alieleza kuguswa na kuhamasika na mikakati iliyowekwa ili kutekeleza lengo la kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga, na kwa upande wa serikali aliahidi kusimamia utekelezaji wa mikakati hiyo.
"Ndugu zangu Wataalam napenda kuwatia moyo muendelea kupambana na changamoto nilizozitajwa awali na nyinginezo, ili tuweze kufikia malengo tuliyojiwekea na kuinua kiwango cha huduma za afya katika nyanja zote, kwa Mkoa wetu wa Dodoma". Alisema Mapogo na kuongeza kuwa
"Kama mlivyojiwekea taratibu za vikao hivi vya kujadili vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga kila robo mwaka kwa kupokezana kila wilaya, endeleeni hivyo hivyo kwani vikao hivi vinatoa picha halisi ya hali ilivyo katika mkoa wetu na kutusaidia kujitathimini kama mkoa na kwa sababu mkoa wetu tuna mikakati mizuri ya kupunguza vifo hivyo, basi tutarajie wageni wengi kuja kujifunza kwetu ili na wenyewe waweze kufaidika kutoka kwetu".
Aidha, akizungumza wakati akimkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Mzee Nassoro alisema kuwa kikao hicho kinahusisha wadau katika sekta ya afya na wataalam wa afya kutoka ngazi ya mkoa na wilaya zote saba (7) za mkoa wa Dodoma.
Kwa picha na matukio tazama hapo chini:
Mganga Mkuu Wilaya ya Bahi, Dkt. Philipina Philipo akizungumza wakati wa Mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bahi tarehe 09 Oktoba, 2018. (Picha na Benton Nollo)
Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Dodoma, Dkt. Mzee Nassoro akizungumza wakati wa Mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bahi tarehe 09 Oktoba, 2018. (Picha na Benton Nollo)
Wataalamu na Wadau wa Sekta ya Afya wakifuatilia moja ya mawasilisho katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bahi tarehe 09 Oktoba, 2018. (Picha na Benton Nollo)
Wataalamu na Wadau wa Sekta ya Afya wakifuatilia moja ya mawasilisho katika mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bahi tarehe 09 Oktoba, 2018. (Picha na Benton Nollo)
Wataalamu na Wadau wa Sekta ya Afya wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi (wa pili kushoto waliokaa) mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bahi tarehe 09 Oktoba, 2018. (Picha na Benton Nollo)
Wataalamu na Wadau wa Sekta ya Afya wakiwa katika picha ya pamoja na mgeni rasmi (wa pili kushoto waliokaa) mara baada ya ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bahi tarehe 09 Oktoba, 2018. (Picha na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa