Na Benton Nollo, Bahi
Viongozi wa Baraza la Wazee Wilaya ya Bahi wametakiwa kushirikiana na Serikali ya wilaya hiyo kupata takwimu sahihi za wazee ili kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbli zikiwemo za afya.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda wakati wakifunga mkutano wa uchaguzi wa Viongozi wa Baraza la Wazee Wilaya ya Bahi tarehe 18 Agosti 2020 kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo.
Munkunda amewataka viongozi hao kuhamasisha jamii wakiwemo wazee kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii Iliyoboreshwa – ICHF ili kuwa na uhakika wa upatikanaji wa huduma za afya wakati wote.
Amesema uwepo wa takwimu sahihi unasaidia wilaya katika utoaji wa huduma wanazostahili kuzipata.
“Mimi niwaombe Wazee wetu bado tunahangaika kupata takwimu ya wazee wetu kwenye Wilaya Bahi. Tunatumia hapa senza ya mwaka 2012 lakini inatupa idadi ambayo siyo rasmi sana na ndiyo maana unakuta uandaaji wa vitambulisho vya wazee tunapata tabu”. Anasema Munkunda na kuongeza;
“Ninyi mkatusaidie kuwa na idadi kamili ya sensa ya Wazee wa Wilaya ya Bahi, manaake wewe Mwenyekiti wa Baraza la Wazee kwenye Kata utusaidie kwenye kata yako tujue kuna wazee wangapi na wale wazee hali zao zikoje kuna wazee ambao hawawezi kula hata milo mitatu kwa siku”.
Aidha, Munkunda ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa wazee kuwa mabalozi wazuri wa kulinda amani kwa kutokubali kutumika hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaenda kufanya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani Oktoba 28, 2020.
“Amani iliyopo Bahi uzuri wake umaujua ninyi kwa sababu ni ndiyo mnaoijua kwa kuwa tangu mnakuwa mnaiona na kuiishi. Kwa hiyo tukaongee na vijana wetu wasitumike vibaya kwenye uchaguzi, wakati wa uchaguzi yanasema mengi…vivyo hivyo wakati wa kupiga kura tutoke tukapige kura”. Anasema Munkunda.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma Mganga amewaomba wazee hao kutoa ushirikiano kwa viongozi waliowachagua ili kuleta ufanisi katika utendaji kazi wao.
“Wazee ni hazina, Wazee ni kitivo cha busara na hekimahatutegemei tusikie eti kuna mvurugano kwenye Baraza la Wazee, sasa mimi ntakuja kuwashauri nini, kwa sababu nyie wazee ndiyo mnaotakiwa mtukanye sisi, tukisikia kuna mvurugano ina maana ya kwamba wazee tumeacha nafasi yetu…hapa jambo ni moja tu, viongozi tukawatumi wazee wa Wilaya ya Bahi”. Anasema Dkt. Mganga na kuongeza;
“Viongozi tukasimame kwenye nafasi yetu kutetea maslahi ya wazee wenzetu na iwapo itatokea fursa ya kuwawakilisha wilaya yetu twendeni tukaiwakilishe Wilaya ya Bahi kana kwamba kuna wazee mahiri, wazee wanaojitambua, wazee wanaotetea haki za wenzao”.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa Mama na Mtoto kutoka Shirika la World Vision Tanzania, Daud Gambo ameahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya shirika hilo na Serikalina kusisitiza kuwa uwepo wa Baraza hilo unapaswa kuigwa na Wilaya nyingine.
Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti wa Baraza la Wazee aliyechaguliwa, Catherine Majenge ameahidi kushirikiana na wazee wenzake katika kubeba jukumu la kushighulika na tabia zilizoshindikana katika jamii.
“Wanasema kidole kimoja hakivunji chawa mkiniachia huu mzigo sitaufikisha popote naomba sana sana kama kweli mmenichagua kwa upendo, mkaniamini na mimi naendelea kuwaamini na kuwaombea yale tuliyoyaazimia na viongozi wanayotushauri tuyafanyie kazi tushirikiane wote kuleta maendeleo na kufanya mapinduzi yaliyo mazuri katika wilaya yetu ya Bahi.” Anasema Majenge.
Majenge amesema baraza hilo lina wajibu wa kurekebisha tabia za watoto walioshindikana pamoja na kutunza utamaduni katika eneo hilo.
Viongozi wengine waliochaguliwa ni Makamu Mwenyekiti John Msihi, Katibu Francis Mayawu, Katibu Msaidizi Yohana Chibago, Mtunza Hazina Pius Chitalya na Wawakilishi wa Wazee katika Baraza la Madiwani ni Mwalimu Dina Ngosi na Dominick Muhila.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda akizungumza wakati akifunga mkutano wa Uchaguzi wa Baraza la Wazee la wilaya hiyo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi tarehe 18 Agosti 2020.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma Mganga akizungumza wakati wa mkutano wa Uchaguzi wa Baraza la Wazee la wilaya hiyo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi tarehe 18 Agosti 2020.
Meneja Mradi wa Mama na Mtoto kutoka Shirika la World Vision Tanzania, Daud Gambo wakati wa mkutano wa Uchaguzi wa Baraza la Wazee la Wilaya ya Bahi kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi tarehe 18 Agosti 2020.
Baadhi ya Wazee wakizungumza wakati wa Mkutano wa Uchaguzi wa Baraza la Wazee la Wilaya ya Bahi kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi tarehe 18 Agosti 2020.
Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Bahi, Liberatha Sunday akitoa muongozo wa muundo wa Baraza la Wazee la Wilaya wakati wa Mkutano wa Uchaguzi wa Baraza la Wazee la wilaya hiyo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi tarehe 18 Agosti 2020.
Picha za hapo juu ni matukio mbalimbali ya mchakato wa uchaguzi, wakati wa Mkutano wa Uchaguzi wa Baraza la Wazee la Wilaya ya Bahi kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi tarehe 18 Agosti 2020.
Baadhi ya Wazee wakipiokea vitambulisho kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (kushoto) kwa niaba ya wazee katika maeneo wanakotoka wakati wa Mkutano wa Uchaguzi wa Baraza la Wazee la Wilaya ya Bahi kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi tarehe 18 Agosti 2020.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Wilaya ya Bahi, Catherine Majenge akitoa neno la shukrani kwa wajumbe wa baraza hilo mara baada ya wajumbe wa mkutano huo kumchagua kushika wadhifa huo wakati wa Mkutano wa Uchaguzi wa Baraza la Wazee la Wilaya ya Bahi kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya hiyo tarehe 18 Agosti 2020. (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa