Na Benton Nollo, Nondwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo (Mb) amewapongeza viongozi wa Wilaya ya Bahi kwa uamuzi wao wa kutumia mapato ya ndani kujenga shule mpya ya Sekondari Kata ya Nondwa ambayo awali haikuwa na shule ya sekondari.
Waziri Jafo ameyasema hayo tarehe 18 Juni 2020 wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani Bahi kukagua maandalizi ya kuwapokea wanafunzi kufuatia tamko lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuwa shule zote nchini zifunguliwe tarehe 29 Juni 2020.
Kufuatia juhudi hizo, Waziri Jafo amemuelekeza Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Bahi, Hellen Mselemu kuwa wakati taratibu za kuisajili shule hiyo zinaendelea ahakikishe kuwa anapanga walimu mara moja katika shule hiyo ili shule zitakapofunguliwa tarehe 29 Juni 2020, wanafunzi wa Kidato cha Kwanza wanaotoka katika kata hiyo kwenda Shule za Sekondari za Magaga iliyopo Kata ya Chifutuka na Chikopelo iliyopo Kata ya Chali waanze kusoma hapo.
“Siwezi kukubali nakuja hapa, kazi nzuri iliyofanyika, halafu watoto waendelee kuteseka wale wataanza hapa, Afisa Elimu leta walimu hapa, shule ianze kutoa matunda. Tunataka hii kazi iliyofanywa na wananchi wa hapa iweze kuzaa matunda kuanzia mwanzo, Afisa Elimu hiyo ni kazi yako kubwa…huku mkihangaikia zoezi la usajili”. Amesema Waziri Jafo na kuongeza;
“Ninyi mmekuwa wilaya ya mfano, kujenga madarasa kama hayo kwa kutumia mapato ya ndani, wengine hawawezi…ninyi Bahi mmetumia fedha za ndani kujenga madarasa…tena Mkurugenzi nikusifu sana, hata madeni ya madiwani huna, wengine madeni ya madiwani wanayo na miundombinu hawajajenga…ninyi Bahi mmefanya kazi ya mfano… hii maana yake DC umesimamia vizuri Wilaya yako na Mkurugenzi umesimamia vizuri Halmashauri yako”.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amemueleza Waziri Jafo kuwa wilaya imejipanga kuifanya shule hiyo kuwa ya mfano kwani awali wanafunzi waliokuwa wanatoka kata hiyo walikuwa wakiongoza kwa utoro kutokana na kutembea umbali wa takriban kilomita 20.
“Tunajua vyumba hivi vinne vya madarasa na ofisi mbili za walimu ni majengo ya awali ya kuanzia kwani tunatambua ili shule ikamilike inatakiwa kuwa na madarasa ya kutosha…na sisi kama wilaya tumejipanga tunataka Shule ya Sekondari Nondwa iwe shule ya mfano wa matumizi mazuri ya fedha za mapato ya ndani” Anasema Munkunda.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amemuhakikishia Waziri Jafo kuwa walimu katika Shule za Sekondari wapo wa kutosha na tayari viti na meza 100 vya kuanzia vimeshatengenezwa na mpaka tarehe 29 Juni 2020 mazingira ya wanafunzi wa Kidato cha Kwanza kuanza kusoma yatakuwa yamekamilika.
Akizungumza awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma Mganga amemueleza Waziri Jafo kuwa Halmashauri hiyo kwa mwaka huu wa fedha (2019/2020) mpaka mwezi Mei, 2020 imeshakusanya mapato ya ndani kwa asilimia 86 na tunajitahidi ili tufikie asilimia 90.
“Tumeamua kupungua matumizi ya kawaida, ili fedha nyingi tuzielekeze katika miradi ya maendeleo kwa sababu tuna changamoto nyingi ambazo tukiiachia Serikali Kuu peke yake haiwezi… na kupunguza huko matumizi ya kawaida, tumeweza kulipa madeni yote ya stahili za madiwani”. Anasema Dkt. Mganga.
Kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nondwa, Bernald Majuto na Mwenyekiti wa Kijiji cha Zejele, Samsoni Mkwawi wameishukuru Serikali kwa mchango huo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kusimamia ukusanyaji wa mapato katika vijiji hivyo ili shule hiyo ikamilike na kuondoa adha ya wanafunzi kusafiri umbali mrefu kufuata masomo.
Ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Nondwa mpaka sasa umegharimu shilingi milioni 72 ambapo kati ya hizo Halmashauri kupitia fedha za mapato ya ndani imechangia shilingi milioni 55 kumalizia ujenzi wa madarasa manne (4) na ofisi mbili (2) za walimu huku shilingi milioni 17 inatokana na michango ya wananchi wa Vijiji vya Nondwa na Zejele.
Picha na Matukio:
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Selemani Jafo (Mb) (katikati) akizungumza kwa furaha baada ya kukagua vyumba vinne vya madarasa na ofisi mbili za walimu Shule mpya ya Sekondari Nondwa, majengo ambayo yamejengwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2019/2020 alipotembelea shuleni hapo tarehe 18 Juni 2020.
Muonekano wa madarasa katika Shule Mpya ya Sekondari Nondwa iliyojengwa kwa mapato ya ndani shilingi milioni 72.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma Mganga akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Selemani Jafo (hayupo pichani) aliyetembelea Shule ya Sekondari Nondwa ambayo imejengwa na Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Selemani Jafo (hayupo pichani) aliyetembelea Shule ya Sekondari Nondwa ambayo imejengwa na Halmashauri kupitia mapato yake ya ndani.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Zejele, Samsoni Mkwawi akimshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI (hayupo pichani) baada ya ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa manne (4) na ofisi mbili (2) za walimu kwa ajili ya shule mpya ya Sekondari Nondwa tarehe 18 Juni 2020.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Nondwa, Bernald Majuto akimshukuru Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI (hayupo pichani) baada ya ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa manne (4) na ofisi mbili (2) za walimu kwa ajili ya shule mpya ya Sekondari Nondwa tarehe 18 Juni 2020.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa