Na Benton Nollo, Bahi
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeamua kujenga Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bunge (Bunge Girls Secondary School) ambayo itajengwa Kikombo, Jijini Dodoma na kabla ya kumalizika kwa Bunge la 11, shule hiyo itakuwa imekamilika ujenzi wake na kukabidhiwa Serikalini mwezi Juni, 2020.
Taarifa hiyo imetolewa na Mratibu wa Kamati ya Ujenzi wa shule hiyo, Neema Kiula ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Bahi tarehe 10 Januari 2020 akiambatana na baadhi ya wajumbe wanne wa Kamati hiyo waliofika wilayani humo kwa lengo la kujifunza jinsi Wilaya ya Bahi ilivyofanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa njia mfumo wa “Force Account” hasa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na ukarabati wa madarasa katika Shule za Sekondari za Chikola, Mundemu, Mpamantwa na Mwitikira.
“Lengo la ziara yetu ni kwamba tumekuja kujifunza na kupata uzoefu wa namna mlivyoweza kutumia Mfumo wa “Force Account” kutekeleza miradi mikubwa ya Serikali ambayo kimsingi mliletewa fedha ninyi mkatekeleza” Alisema Kiula na kuongeza kuwa;
“Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bunge ambayo itakabidhiwa Serikalini mwezi Juni 2020 kabla ya kumalizika kwa Bunge la 11, hivyo lengo la kuja Bahi ni kupata uzoefu wa kutumia mfumo huo ili tuutumie kukamilisha mradi huu mkubwa”.
Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda aliishukuru Kamati hiyo kwa kuichagua wilaya hiyo kuja kujifunza ni dhahiri kwamba Serikali na mhimili huo unatambua kazi nzuri ya usimamizi wa miradi unaofanywa na wataalam wake.
“Kubwa kuliko yote hapa ni ushirikiano na mshikamano tuliokuwa nao baina yetu, mfano katika ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bahi baada ya kupokea fedha tuliutambulisha mradi kwa wananchi na waliupokea vizuri sana na wakatoa ushirikiano”. Alisema Munkunda.
Munkunda amesema kuwa jambo jingine lililofanya miradi hii itekelezwe vizuri ni uwazi katika manunuzi ya bidhaa zilizokuwa zikihitajika, hali hiyo ilijenga morali kwa wataalam na wananchi kujituma zaidi.
“Pia, pamoja na muongozo wa usimamizi wa ujenzi uliotolewa na Wizara mfano Hospitali ya Wilaya, sisi tulijiongeza tukayagawa majengo yote kwa Wakuu wa Idara hivyo kila jengo katika majengo yote saba, lilisimamiwa na Wakuu wa Idara wawili hivyo kukawa na ushindani wa ndani”. Alimsema Munkunda.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Charles Mduma aliwaeleza wajumbe wa Kamati hiyo kuwa jambo jingine lilopunguza gharama ni kuwatumia mafundi wa kawaida (Direct Firce Account) kwa kila hatua ya ujenzi ambao walisimamiwa na Mhandisi badala ya kumuweka fundi mmoja kwa hatua zote za ujenzi ambapo mkakati huo ulisaidia kuokoa shilingi milioni 70 yaani angetumika fundi mmoja malipo yaliyokuwa yanahitajika ni shilingi milioni 300 lakini kwa mfumo huo zilitumika shilingi milioni 230.
Mduma amesema kuwa manunuzi yote ya vifaa kama vile saruji, marumaru, mabati, mbao, gypsum, rangi, vifaa vya umeme na nondo vilinunuliwa viwandani moja kwa moja bila kutumia mawakala ambapo mkakati huo ulisaidia kupata bei halisi ya vifaa na kupunguza gharama za ujenzi.
Pia, Mduma amesema kuwa Manunuzi ya vifaa ambavyo siyo vya viwandani kama vile madirisha ya aluminiamu, milango, grili za milango yamefanyika kwa kuunda kamati za wajumbe ambazo zilitafuta bei za ushindani za soko. Amesema kwamba mfano ununuzi wa madirisha ya vioo, bei zilitafutwa na kamati tatu tofauti ambazo zilipelekea kushuka kwa bei kutoka milioni 60 kwa madirisha 306 hadi shilingi milioni 48 hivyo kuokoa shilingi milioni 12 katika eneo hilo.
Kadhalika, Mduma aliieleza kamati hiyo kuwa kulikuwa na vikao vya ujenzi mara tatu kwa wiki yaani Jumatatu, Jumatano na Ijumaa saa 01:30 asubuhi eneo la mradi ambapo kila Wakuu wa Idara waliopangiwa jengo walitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi zilizopangwa kufanywa kwa siku mbili na mpango kazi wa siku mbili zinazofuata. Mkakatri huo ulisaidia kubaini mapema changamoto za mafundi na vifaa na kutafua ufumbuzi haraka.
Picha za Matukio:
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (kulia) akiwaonesha Wajumbe wa Kamati ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bunge majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Bahi yaliyojengwa kwa Mfumo wa "Force Account" baada ya wajumbe hao kutembelea majengo hayo tarehe 10 Januari 2020.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Charles Mduma akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bahi iliyojengwa kwa Mfumo wa "Force Account", kwa Wajumbe wa Kamati ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bunge baada ya wajumbe hao kutembelea majengo hayo kwa lengo la kujifunza matumizi ya mfumo huo tarehe 10 Januari 2020.
Wajumbe wa Kamati ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bunge, wakimsikiliza kwa makini Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi (hayupo pichani), wakati akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bahi iliyojengwa kwa Mfumo wa "Force Account", ambapo wajumbe hao walitembelea majengo hayo kwa lengo la kujifunza matumizi ya mfumo huo tarehe 10 Januari 2020.
Mratibu wa Kamati ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bunge, Neema Kiula akizungumza baada ya kupokea taarifa ya Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bahi iliyojengwa kwa Mfumo wa "Force Account", ambapo wajumbe hao walitembelea majengo hayo kwa lengo la kujifunza matumizi ya mfumo huo tarehe 10 Januari 2020.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Bahi na Wakuu wa Idara walikiwa pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bunge ambao walikuja kujifunza matumizi ya Force Account katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali tarehe 10 Januari 2020.
Wajumbe wa Kamati ya Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Bunge na Wakuu wa Idara wakitembelea majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Bahi ambayo yamejengwa na kukamilika kwa kutumia Mfumo wa "Direct Force Account". Wajumbe hao walikuja kujifunza matumizi ya Mfumo huo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali tarehe 10 Januari 2020.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa