Na Benton Nollo, Halmashauri ya Wilaya ya Bahi
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Mhe. Danford Chisomi amewataka Mafundi na Mkandarasi walioshinda zabuni ya ujenzi wa majengo matano katika Zahanati ya Chifutuka na ile ya Utafiti na Uchimbaji wa Kisima cha maji Kijiji cha Nghulugano, kuwalipa vibarua wao kwa wakati na kuwasimamia wakati wote ili miradi hiyo ikamilike kwa ubora na kwa muda uliopangwa kwenye mkataba. Chisomi ameyasema hayo Juni 26, 2018 mara baada ya kusaini mikataba baina ya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na Mafundi watakaojenga majengo matano kwa mfumo wa "Force Account" katika Zahanati ya Chifutuka pamoja na Utafiti na Uchimbaji wa Kisima cha maji Kijiji cha Nghulugano.
"Serikali Kuu tayari imeshatuingizia fedha shilingi 500,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu katika Zahanati ya Chifutuka, hivyo sisi kama Halmashauri kupitia Ofisi ya Mweka Hazina wa Wilaya tutahakikisha mafundi wote wanalipwa kwa wakati na vifaa vinanunuliwa na kupelekwa eneo la mradi haraka ili ndani ya siku 90 majengo yote yawe yamekamilika". Alisema Chisomi na kuongeza kwa kumkumbusha Mweka Hazina kuwakata mafundi hao Kodi ya Zuio ambayo ni asilimia 5 kwa kila malipo watakayohitaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Rachel Chuwa amewataka mafundi hao kusoma vizuri vipengele vyote vya mikataba yao ili waelewe na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
"Ni wajibu wa kila fundi kusoma kwa makini na kuyaelewa vema majukumu anayopaswa kutekeleza kwani ni matarajio ya wananchi kuona miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili waweze kupata huduma kama ilivyokusudiwa na Serikali. Pia, kila fundi ahakikishe kuwa anawasimamia vibarua wake ili kuepuka upotevu wa vifaa hali ambayo itadhoofisha utekelezaji wa mradi". Alisema Chuwa.
Akizungumza kwa niaba ya mafundi wenzake, Nassoro Twaibu Nambinga atakayejenga nyumba ya mtumishi Zahanati ya Chifutuka ameiomba Halmashauri kununua vifaa na kuvipeleka eneo la mradi kwa wakati ili kusiwe na ucheleweshaji wa kazi kwa kisingizio cha vifaa kuchelewa.
Ujenzi wa majengo Zahanati ya Chifutuka unajumuisha jengo la upasuaji ambapo fundi ni Robert N. Makapi na gharama ya ufundi ni shilingi 21,280,000.00, jengo la Wodi ya Akinamama na Watoto fundi ni Hassan R. Mvungi gharama za ufundi ni shilingi 22,750,000.00 na ujenzi wa Jengo la Maabara Fundi ni Sembisa Alfredy gharama ya ufundi ni shilingi 16,600,000.00. Majengo mengine ni Nyumba ya Mtumishi fundi ni Nassoro Nambinga atakayejenga kwa shilingi 14,100,000.00, jengo la Kuhifadhia Maiti fundi ni Hosea L. Shansi kwa gharama ya shilingi 12,500,000.00.
kwa upande wa mradi wa Utafiti na Uchimbaji wa Kisima katika Kijiji cha Nghulugano utakaotekelezwa na Mkandarasi Target Borewells Ltd kwa gharama ya shilingi 30,680,000.00 na mradi utatekeleza kwa muda wa siku 15 kuanzia Juni 26, 2018.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa