Na Benton Nollo na Bernard Magawa (DMC), Bahi
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda ametoa rai kwa Madiwani wa wilaya hiyo kuhakikisha kuwa katika uongozi wao wanashirikiana na viongozi wa Kata na Vijiji ili kutatua kero zinazowakabili wananchi.
Munkunda ametoa rai hiyo wakati wa uzinduzi wa Baraza Jipya la Madiwani katika Mkutano wa Kwanza uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi tarehe 14 Desemba 2020 kwa ajili ya kuwaapisha Madiwani hao, kumchagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi.
Amesema Madiwani wahakikishe wanayasimamia vema Mabaraza ya Kata katika maeneo yao kwani ndiko chimbuko la maendeleo lilipo ikiwa ni pamoja na kuyaimarisha na kuyasimamia vema mabaraza ya ardhi ya kata ili kutatua migogoro mingi ya ardhi iliyopo katika maeneo yao.
“Kiongozi lazima ujue kuwa upo kwa ajili ya kutatua matatizo ya wananchi, shirikianeni na viongozi wa vijiji na kata kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwani wamewaamini ndiyo maana wamewachagua hivyo, hakikisheni mnawatumikia ipasavyo.” Amesema Munkunda.
Mkuu huyo wa Wilaya pia, amewaagiza Madiwani hao kuhakikisha maeneo yote ya wazi ambayo ni mali ya kijiji yanarudi Serikalini ili yaweze kusimamiwa na kupangiwa matumizi kwa manufaa ya Wananchi wote badala ya kuhodhiwa na watu wachache.
“Hakikisheni maeneo yote ambayo ni mali ya Kijiji yanarudi Serikalini, pia ni marufuku watu kupiga uzio maeneo ya wazi na kujimilikisha jambo hilo haliwezekani, ni lazima Serikali tuwe na benki ya ardhi kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya maendeleo.” Amesema Munkunda.
Awali akifungua Mkutano wa Kwanza wa Baraza Jipya la Madiwani Mwenyekiti ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Bahi, Jeremia Mapogo amewataka Madiwani kuwa na mshikamano ili waweze kupata ufanisi kwenye majukumu waliyopewa.
“Niwapongeze Madiwani wote kwa kuchaguliwa kuwa wawakilishi wa Wananchi, kazi mliyopewa ni nyeti, hakikisheni mnakuwa na mshikamano katika kazi zenu ili muwe na ufanisi.” Amesema Mapogo na kuongeza;
“Mnao wajibu wa kuleta maoni ya wananchi Halmashauri na kurudisha mrejesho kwao ili kwa pamoja tuyasukume maendeleo mbele.”
Akizungumza baada ya kuchaguliwa kuwa Menyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi kwa kipindi cha miaka mitano (2020 – 2025), Donald Simango Mejiti ambaye ni Diwani wa Kata ya Lamaiti amewashukuru Madiwani kwa kuonesha imani kwake na kuomba ushirikiano ili kwa pamoja waweze kuleta maendeleo kwa Wananchi.
“Niwashukuru sana kwa kuonyesha imani kwangu, niombe ushirikiano wenu kwani kamwe hatuwezi kuiendesha Halmashauri bila kuwa na ushirikiano, tuwe na uzalendo na mshikamano ili tuongeze tija katika maendeleo ya wilaya yetu.” Amesema Mejiti.
Katika Uchaguzi huo, Mejiti alichaguliwa kwa kura za NDIYO 29 kati ya kura 30 zilizopigwa sawa na asilimia 96.7, naye Diwani wa Kata ya Chali, Pius Donald Mwaluko amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kwa kura za NDIYO 28 kati ya kura 30 zilizopigwa sawa na asilimia 93.3.
Pamoja na uchaguzi huo pia ulifanyika uchaguzi wa wajumbe wa Kamati za Kudumu za Halmashauri ambapo Diwani wa Kata ya Mpamantwa, Sosthenes Mpandu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji (EAM) ambapo Diwani wa Kata ya Msisi, Mathayo Malilo alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Uchumi na Mazingira (UUM).
Baraza hilo limeketi kwa mara ya kwanza baada ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa tarehe 28 Oktoba 2020, ambapo tangu kuanzishwa kwa Halmashauri hiyo mwaka 2007 hili ni Baraza la Tatu.
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ambaye pia ni Katibu wa Mkutano wa Kwanza wa Madiwani, Dkt. Fatuma Mganga akiwakaribisha Madiwani kwenye mkutano huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Donald Mejiti akiendesha kikao cha Mkutano wa Kwanza wa Baraza la Madiwani mara baada ya kuchaguliwa.
Mbunge wa Jimbo la Bahi, Kenneth Nollo, (Mb) akizungumza wakati wa kikao cha Mkutano wa Kwanza wa Baraza la Madiwani.
Afisa Mipango wa Wilaya ya Bahi, Charles Mduma akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Halmashauri katika kipindi ambacho Madiwani hawakuwepo.
Viongozi meza kuu wakifuatilia kwa makini taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Halmashauri katika kipindi ambacho Madiwani hawakuwepo iliyokuwa ikiwasiilshwa na Afisa Mipango wa Wilaya ya Bahi, Charles Mduma (hayupo pichani).
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Pius Donald Mwaluko akiwashukuru Madiwani baada ya kumchagua kushika wadhifa huo kwa kipindi cha mwaka mmoja (2020/2021).
Baadhi ya Waheshimiwa Madiwani wakila Kiapo cha Uadilifu mara baada ya kula kiapo cha udiwani.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa