Na Benton Nollo
Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda amewataka viongozi wa Vijiji, Kata na Tarafa zote katika Wilaya ya Bahi kuhakikisha kuwa wanawahamasisha wananchi kuchangia chakula kwa ajili ya wanafunzi hasa wa Kidato cha Nne ili waweze kujiandaa vema na mtihani wa Kidato cha Nne mwaka 2018. Munkunda ameyasema hayo katika Kijiji cha Mtitaa alipokuwa akizungumza na viongozi wa Tarafa ya Mtitaa wakati wa ziara yake ya kujitambulisha tarehe 28 Agosti, 2018.
Munkunda aliwaeleza viongozi hao kuwa ili Wilaya ya Bahi isonge mbele kimaendeleo suala la elimu linatakiwa kuwekewa mkazo na mkakati madhubuti kwani kwa kufanya hivyo sekta nyingine zote zitaboreka kwa kuwa vijana watakuwa wamejikwamua kielimu.
"Ndugu zangu ili Wilaya ya Bahi isonge mbele, sekta ya elimu ni eneo muhimu sana la kulitazama na kuliendeleza kwa kuliwekea mkakati madhubuti. Wazazi wahamasishwe kuandaa Kambi za wanafunzi kujisomea ili kuongeza ufaulu na kupunguza ziro katika Shule zetu za Sekondari". Alisema Munkunda na kuongeza kuwa,
"Mimi kama kiongozi wenu ningependa kufahamu mkakati wenu katika kuboresha na kukuza sekta ya elimu katika wilaya yetu kwamba nyinyi kama viongozi mmejipa vipi, mmejipanga kuongeza ziro au mmejipanga kupunguza ziro? Na mipango yenu ni ipi? Watoto wameanza makambi kama watoto wameanza makambi au kama hawajaanza mmeshawahamasisha kwa kiasi gani ili waanze hayo makambi na je wazazi nao wameshahamasishwa kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao? Hivyo, nategemea kupata hizo taarifa ili nipate kujua hali halisi ya shule za Sekondari zilizopo Tarafa ya Mtitaa".
Picha Namba 1
Picha Namba 2
Picha namba 1 na 2 hapo juu ni baadhi ya viongozi wa Tarafa ya Mtitaa wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (hayupo kwenye picha zote) aliyekuwa akizungumza nao kwenye kikao cha ndani kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Kituo cha Kilimo Mtitaa tarehe 28 Agosti, 2018.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Rachel Chuwa ambaye aliambatana na kiongozi huyo, alisema kuwa dhana ya elimu bila malipo haimaanishi wazazi wasishiriki mipango ya kuinua kiwango cha elimu kwa watoto wao hivyo uongozi wa vijiji uhamasishe kuhakikisha kuwa shule zinakuwa na chakula kwa ajili ya wanafunzi wanapata huduma ya chakula wawapo shuleni ili kurahisisha maandalizi ya wanafunzi kujiandaa katika masomo yao.
Pia, aliwahimiza viongozi hao kusimamia suala la wananchi kujiunga na CHF Iliyoboreshwa ambayo kwa sasa ni shilingi 30,000.00 kwa watu sita (6) badala ya shilingi 10,000.00 kwani huduma za afya zimeongezwa. Kadhalika, aliwakumbusha viongozi kuwahimiza wananchi kujenga vyoo bora na kuvitumia ili kujikinga na magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Rachel Chuwa akisisitiza jambo wakati akizungumza na viongozi wa Tarafa ya Mtitaa tarehe 28 Agosti, 2018
Aidha, pamoja na suala la elimu, DC Munkunda alisisitiza suala la Watendaji wa Vijiji na Kata kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuzuia mianya ya upotevu wake, kuwahamasisha wananchi kutambua fursa za uwekezaji zilizopo katika maeneo yao ili wawekeze kwa lengo la kujikwamua na umaskini na kukuza uchumi katika familia zao na kwa kufanya hivyo uchumi kwa Wilaya ya Bahi utakuwa.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa