Serikali mkoani Dodoma imeomba maonesho ya Nanenane kitaifa kwa mwaka 2021 yafanyike Dodoma ili kuyapa heshima Makao Makuu ya nchi na kutoa fursa kwa wananchi wengi kujionea maarifa yatokanayo na maonesho hayo katika kuboresha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
Ombi hilo limetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge alipokuwa akiongea na wananchi katika Maonesho ya Nanenane Uwanja wa Nanenane uliopo Nzuguni jijini Dodoma.
“Nikuombe Mheshimiwa Waziri, Dodoma ni Makao Makuu yetu sote na itajengwa na watanzania wote. Namna moja wapo ya kujenga na kuharakisha ustawi wa Makao Makuu ni pamoja na mchango wa kufanyia shughuli mbalimbali za kitaifa Makao Makuu. Tumeshuhudia sherehe za Uhuru zikifanyikia hapa, tumeshuhudia sherehe za Muungano zikifanyikia hapa, itapendeza sana Mheshimiwa Waziri ukitupelekea maombi kwamba na sherehe hizi za Nanenane za kitaifa ziweze kufanyikia Makao Makuu hii itatangaza sana na kuleta wawekezaji katika Mkoa wetu na Makao Makuu ya nchi”. Amesema Dkt. Mahenge akimuomba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika Ufunguzi wa maonesho hayo Kanda ya Kati.
Pia, Dkt. Mahenge amewashawishi wananchi kutembelea maonesho hayo ili wanufaike nayo.
“Katika maonesho haya hasa kwenye mabanda, kuna vitu vingi vinaoneshwa ambavyo ni fursa kwenu wana Dodoma ambao tupo karibu kuliko mikoa yote kwenda kuyaona. Na kama tunataka kumuunga mkono Mheshimiwa Rais lazima tuanze kuzalisha kwa nguvu zetu zote na kwa wingi ili tuweze kunufaika na miundombinu inayojengwa katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu”. Amesema Dkt. Mahenge.
Aidha, aliwashukuru wadau wote waliochukua maeneo kwa ajili ya kuonesha shughuli zao katika Nanenane.
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa