Na Benton Nollo, Ibihwa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo ameipongeza Taasisi ya Dkt. Msuya Foundation kwa kusaidia ukarabati wa Viti 76 na Meza 45 vya Shule ya Sekondari Ibihwa wilayani Bahi wakati akipokea samani hizo tarehe 18 Juni 2020 alipofanya ziara ya siku moja wilayani hapa.
Waziri Jafo ameipongeza taasisi hiyo inayoongozwa na Dkt. Ombeni Msuya kwa moyo wao wa uzalendo waliouonesha kwenye shule hiyo ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali za kuinua elimu nchini.
Msaada huo uliotolewa na taasisi hiyo umeifanya Shule ya Sekondari Ibihwa kuwa na jumla ya viti 255 na meza 255 kwa wanafunzi 255, hivyo kuifanya shule hiyo kutokuwa na upungufu wa samani kwa wanafunzi wake.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa samani hizo na Dkt. Msuya, Waziri Jafo amesema kitendo kilichofanywa na taasisi hiyo ni cha kizalendo na kinapaswa kuungwa mkono na kwamba serikali itaendelea kushirikiana naye katika kuwahudumia watanzania.
Jafo ameipongeza taasisi hiyo kwa namna ambavyo imekua ikiguswa kushirikiana na serikali kuleta maendeleo ambapo hata katika janga la Corona walikabidhi vifaa vya kujikinga na Ugonjwa huo wilayani Mwanga, Kilimanjaro pamoja na maeneo mengine nchini.
"Nikushukuru sana Dkt. Msuya, nafahamu ulikuja na utafiti wako kuangalia jinsi gani changamoto tulizonazo tunaweza kuzifanyia kazi ili kukuza sekta yetu ya elimu na ukaja na majibu ya kufanyia ukarabati samani zetu na leo unatukabidhi hapa kwa ajili ya watoto wetu kutumia”. Anasema Waziri Jafo na kuongeza;
“Hii si kwa sababu una kipato kikubwa sana bali ni moyo wa kizalendo na wenye imani ulionao kwa watanzania wenzako. Ungeweza kupeleka kwenu Mwanga lakini ukasema hapana, hawa watoto wa Bahi nao ni watanzania wenzangu, nakupongeza na nikusihi uendelee na moyo huohuo".
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Dkt. Ombeni Msuya amesema waliguswa na kazi kubwa inayofanya na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika kuwatumikia watanzania hivyo nao wakaona wamuunge mkono kwenye sekta ya elimu.
Amesema watanzania wanapaswa kuwa na utaratibu wa kufanya ukarabati wa samani kwenye taasisi kwani fedha nyingi zinaweza kuokolewa kwa kutengeneza samani zilizoharibika kuliko kununua mpya.
"Mheshimiwa Waziri tunashukuru sana kwa namna ambavyo Wizara yako na uongozi wa Wilaya kupitia Mheshimiwa DC ulitupa ushirikiano katika kufanikisha jambo hili, tunaamini samani hizi zitakuwa msaada kwa watoto wa kitanzania wenye ndoto za kufanikiwa kupitia elimu”. Amesema Dkt. Msuya na kuongeza;
“Serikali yetu chini ya Rais Magufuli imefanya kazi kubwa kwenye kila nyanja, ni jukumu letu kama watanzania kuonesha uzalendo wetu katika kumuunga mkono, niahidi hapa kwamba taasisi yetu itaendelea kukarabati samani kwenye shule zetu nchini lengo likiwa kumtia moyo Rais kwa kazi kubwa anayofanya".
Amesema kukamilika kwa ukarabati maana yake wanafunzi 76 ambao walikua hawana viti sasa watapata na wengine 45 waliokua hawana meza sasa watanufaika ma meza hizo.
"Ukarabati huu Mheshimiwa Waziri pia unaokoa fedha nyingi, tulipata taarifa kutoka kwa Mkuu wa Shule kwamba ununuzi wa kitu kimoja unagharimu shilingi elfu 60 sasa ukiangalia idadi ambayo sisi tumekarabati utaona tumeokoa kiwango kikubwa cha fedha ambacho kitaenda kufanyia shughuli nyingine”. Anafafanua Dkt. Msuya nakuongeza;
“Hivyo, tunachotaka kusema leo ni kwamba kuna uwezekano mkubwa katika taasisi zingine zote kuchukua uamuzi wa kukarabati maana ni nafuu. Pia, sisi tumetumia shilingi 934,000 hivyo, nitoe rai kwa watanzania kuwa na utaratibu huu".
Naye Mkuu wa Shule hiyo, Aldin Mnaro ameishukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kufungua shule zote tarehe 29 Juni 2020, ambapo alieleza kuwa tayari wameshaanza kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi huku wakichukua tahadhari ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na Virusi vya Corona.
" Niipongeze serikali kwa kazi kubwa inayofanya katika sekta ya elimu, lakini pia niishukuru Taasisi ya Dkt. Ombeni Msuya kwa ukarabati huu walioufanya ambao sasa unaifanya Shule yetu isiwe na upungufu wa samani na tunaahidi kuvitunza kwa muda mrefu zaidi, " Amesema Mwl. Mnaro.
Picha na Matukio:
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo (Mb) akizungumza kabla ya kupokea Viti 76 na Meza 45 vya Shule ya Sekondari Ibihwa ambavyo vimekarabatiwa na Taasisi ya Dkt. Msuya Foundation wakati wa ziara yake shuleni hapo tarehe 18 Juni 2020.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo (Mb) (katikati), Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Mwanahamisi Munkunda (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma Mganga (kushoto) wakimsikiliza Mkuu wa Shule ya Sekondari Ibihwa (hayupo pichani) wakati akisoma taarifa ya shule hiyo kabla ya Waziri huyo kupokea viti 76 na meza 45 vya shule hiyo ambavyo vimekarabatiwa na Taasisi ya Dkt. Msuya Foundation wakati wa ziara yake shuleni hapo tarehe 18 Juni 2020.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Dkt. Msuya Foundation, Dkt. Ombeni Msuya akizungumza kabla ya kukabidhi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo (Mb) (hayupo pichani) viti 76 na meza 45 vya Shule ya Sekondari Ibihwa ambavyo vimekarabatiwa na Taasisi hiyo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Ibihwa, Aldin Mnaro akisoma taarifa ya shule hiyo kabla Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Selemani Jafo (Mb) (hayupo pichani) hajapokea viti 76 na meza 45 vya shule hiyo ambavyo vimekarabatiwa na Taasisi ya Dkt. Msuya Foundation wakati wa ziara yake shuleni hapo tarehe 18 Juni 2020.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Selemani Jafo (Mb) (katikati aliyevaa tai nyekundu) akifurahi kuona madarasa yaliyokamilika vema kwa gharama ya shilingi milioni 25 zilizotolewa na Serikali kujenga miundombinu hiyo katika Shule ya Sekondari Ibihwa wilayani Bahi. Waziri Jafo katika ziara yake hiyo aliyoifanya tarehe 18 Juni 2020 pia, alipokea viti 76 na meza 45 vya shule hiyo ambavyo vimekarabatiwa na Taasisi ya Dkt. Msuya Foundation.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Selemani Jafo (Mb) (kulia) akiwasili katika Shule ya Sekondari Ibihwa kwa ajili ya kukagua miundombinu na maandalizi ya kuwapokea wanafunzi kufuatia tamko lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli la shule zote nchini kufunguliwa tarehe 29 Juni 2020 baada ya kufungwa kwa takriban miezi miwili. Pia, Waziri Jafo alitumia fursa hiyo kupokea viti 76 na meza 45 vya shule hiyo ambavyo vimekarabatiwa na Taasisi ya Dkt. Msuya Foundation. (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa