Na Benton Nollo na Bernard Magawa (DMC), Bahi.
Mbunge wa Jimbo la Bahi, Kenneth Nollo (Mb) amekabidhi mabati 130 kwa ajili ya kupaua vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu Shule ya Sekondari Bahi ambayo yanajengwa katikati ya vijiji vya Nagulo Bahi na Uhelela.
Nollo amekabidhi mabati hayo tarehe 12 Februari 2021 shuleni hapo ambayo ni miongoni mwa mabati 780 yenye thamani ya shilingi milioni 24.3 yaliyonunuliwa kwa fedha za Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kuezeka madarasa 12 katika Shuke za Sekondari Mpinga (mabati 260), Ilindi (mabati 130), Mpamantwa (mabati 130), na Chibelela (mabati 130).
Akizungumza kabla ya kukabidhi mabati hayo, Nollo amewapongeza viongozi wa wilaya, Kata ya Bahi, Serikali za vijiji hivyo na wananchi kwa namna walivyojitoa katika michango ya fedha pamoja na kujitolea nguvu kazi kuhakikisha majengo hayo yanaenda kukamilika kwa wakati.
“Kwa jinsi nilivyolikuta jengo hili, na kwa jinsi mlivyoshirikiana viongozi na wananchi katika ujenzi huu kupitia michango ya hali na mali, na mimi najiona bado nina deni jingine kwenu, hivyo pamoja na kutoa mabati haya leo bado kwa kutumia nguvu zangu na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nitajitahidi kuongeza majengo walau mawili au matatu ili kuboresha shule hii.” Amesema Nollo.
Akizungumza katika makabidhiano ya Mabati hayo Diwani wa Kata ya Bahi, Augustino Ndonu amemshukuru Mbunge kwa kutoa mabati yote ya jengo hilo ambalo limejengwa kusaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Bahi ambayo inahudumia vijiji vitatu vya kata hiyo yenye idadi kubwa ya wanafunzi wanaofaulu kujiunga na masomo ya Sekondari.
Aidha, Ndonu amemhakikishia Mbunge huyo pamoja na Serikali kuwa atahakikisha kila fedha ya serikali inayopelekwa katika kata yake ataisimamia vizuri na kuona inafanya kazi kama ilivyokusudiwa na siyo vinginevyo.
Awali, akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo Mkuu wa Shule ya Sekondari Bahi, Kudra Kitabuge amesema ujenzi huo ulianza tarehe 05 Januari 2021 kwa nguvu za wananchi pamoja na Serikali za vijiji mara baada ya kupokea agizo la kuanza kwa ujenzi huo kutoka ngazi ya wilaya.
“Hata hivyo, tarehe 08 Januari mwaka huu tulipokea kiasi cha shilingi milioni 12.5 kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bahi kwa ajili ya kusaidia ujenzi huu katika kuwalipa mafundi pamoja na vifaa mbalimbali hadi kufikia hatua hii ya upauaji, Mheshimiwa Mbunge tunakushukuru sana kwa kutupatia mabati haya ambayo yatasaidia kufunika jengo lote.” Amesema Kitabuge.
Mbunge wa Jimbo la Bahi, Kenneth Nollo (Mb) (aliyevaa suti ya kijivu) akikabidhi mabati 130 ya kuezekea vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu Shule ya Sekondari Bahi (Nagulo) tarehe 12 Februari 2021. Mabati hayo ni miongoni mwa mabati 780 yaliyonunuliwa na fedha za Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kuezeka madara 12 ambayo ujenzi wake unaendele katika Shule za Sekondari Mpinga, Ilindi, Mpamantwa na Chibelela.
Mbunge wa Jimbo la Bahi, Kenneth Nollo (Mb) (aliyevaa suti ya kijivu) akizungumza kabla ya kukabidhi mabati 130 ya kuezekea vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu Shule ya Sekondari Bahi (Nagulo) tarehe 12 Februari 2021. Mabati hayo ni miongoni mwa mabati 780 yaliyonunuliwa na fedha za Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kuezeka madara 12 ambayo ujenzi wake unaendele katika Shule za Sekondari Mpinga, Ilindi, Mpamantwa na Chibelela.
Baadhi ya viongozi wa Serikali za vijiji vya Bahi Sokoni, Nagulo Bahi na Uhelela wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Bahi, Kenneth Nollo (Mb) (hatupo pichani) kabla ya kukabidhi mabati 130 ya kuezekea vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu Shule ya Sekondari Bahi (Nagulo) tarehe 12 Februari 2021. Mabati hayo ni miongoni mwa mabati 780 yaliyonunuliwa na fedha za Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kuezeka madara 12 ambayo ujenzi wake unaendele katika Shule za Sekondari Mpinga, Ilindi, Mpamantwa na Chibelela.
Muonekano wa jengo la vyumba viwili vya madarasa na ofisi moja ya walimu Shule ya Sekondari Bahi (Nagulo) ambalo ujenzi wake unaendelea litaezekwa kwa mabati 130 yaliyokabidhiwa na Mbunge wa Jimbo la Bahi, Kennth Nollo (Mb) (hayupo pichani) tarehe 12 Februari 2021. Mabati hayo ni miongoni mwa mabati 780 yaliyonunuliwa na fedha za Mfuko wa Jimbo kwa ajili ya kuezeka madara 12 ambayo ujenzi wake unaendele katika Shule za Sekondari Mpinga, Ilindi, Mpamantwa na Chibelela. (Picha zote na Benton Nollo).
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa