Benton Nollo, Bahi
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dkt. Fatuma Mganga amesema mabadiliko chanya katika Halmashauri hiyo ni lazima yatokee kwani anaamini uwezo wake wa kiutendaji kwa kushirikiana na watumishi waliopo wataipatia maendeleo wilaya hiyo na kuinua uchumi wa wananchi wa Bahi.
Mganga ameyasema hayo wakati akizungumza kwa lengo la kujitambulisha kwa watumishi wa Halmashauri hiyo waliopo Makao Makuu, kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Bahi tarehe 06 Februari, 2019.
Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa anauhakika baada ya muda mfupi kwa kushirikiana wa Menejimenti na Wataalam mbalimbali waliopo Halmashauri hiyo itapiga hatua kimaendeleo na anaamini hicho ndiyo kitu pekee kitakachohalalisha uwepo wake Bahi.
“Ndugu watumishi kazi pekee iliyonifanya nije hapa ni kuleta mabadiliko, nikiwa hapa na pakaonekana hakuna mabadiliko kuja kwangu hapa ni kazi bure, ni lazima mabadiliko yatokeee hiyo jamani tupende tusipende ni lazima Bahi ya zamani ibadilike. Mimi sijawahi kuwa mahali popote mahali hapo pakawa pa mwisho. Hivyo, tushirikiane vizuri hasa katika suala la ukusanyaji wa mapato kwani mpaka sasa ni nusu mwaka lakini katika suala la ukusanyaji wa mapato Bahi imekusanya mapato kwa asilimia 24 na kiukweli hicho ndicho kipimo pekee ya kumpima Mkurugenzi katika nafasi yake”. Alisema Mganga.
Aidha, aliwataka watumishi kuamini kwamba uwepo wao katika Hamashauri ya Bahi ni neema na fursa ya pekee wao kuonesha kwamba wanaweza kufanya kitu chenye tija na faida kwa wananchi wa Wilaya ya Bahi.
“Binafsi mimi kuletwa Bahi ili nije kushirikiana na ninyi hiyo kwangu ni neema na fursa ambayo tunatakiwa kujua kuwa tunaweza kufanya kitu na tukaleta mabadiliko. Sasa yeyote atakayekuwa anakwaza hizo jitihada kwa kweli hatutahurumiana na wala sitakuonea aibu kwa sababu sisi wote tumeajiriwa na Serikali tuitumikie Serikali, tunapewa mishahara kwa sababu tunatakiwa tutumikie Serikali kwa hiyo mtu yeyote atakayekuwa anapokea mshahara lakini lengo lake halifikiwi huyo hapaswi kuwepo kwa sababu anaihujumu Serikali. Kwa hiyo kwa neno moja tu ninaomba tusaidiane kubadilisha hali ya Bahi. Alisema Mganga.
Kadhalika, Mganga aliwataka watumishi kutambua kuwa wanatakiwa kung’ara katika utendaji wao wa kazi na kusema kuwa hata Mungu hakumuumba mwanandamu kwa mtu wa chini bali alimuumba mwanadamu ili awe nuru katika uso wa dunia hii na kusisitiza kuwa watumishi wanapaswa kukerwa na malalamiko yanayotoka ngazi za juu kutoridhishwa na utendaji wa kazi wa Bahi na badala yake wafanye kazi kwa bidii na kwa kujituma.
Dkt. Fatuma Ramadhani Mganga ni Mkurugenzi mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi aliyeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 27 Januari, 2019 na kuapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam tarehe 29 Januari, 2019.
.......................
Habari katika Picha:
Picha zote hapo juu ni Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi waliopo Makao Makuu wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dkt. Fatuma Ramadhani Mganga (hayupo kwenye picha zote) wakati akijitambulisha kwa watumishi hao kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri tarehe 06 Februatri, 2019. (Picha zote na Benton Nollo)
Kitengo cha Ugavi na Manunuzi
Anuani: S.L.P 2993 DODOMA
Simu: +255 762077589
Simu: +255 762077589
Barua Pepe: ded@bahidc.go.tz
Hakimiliki ©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Bahi. Haki Zote Zimehifadhiwa